Ad

Mabunge yatakiwa kuongeza Bajeti Kupunguza vifo vya Mama na Mtoto

Na Ripota wa TBN, Arusha.

Mabunge duniani yametakiwa kuimarisha usimamizi wa bajeti na utekelezaji wa sera za afya ili kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga, pamoja na kuongeza upatikanaji wa huduma za afya ya uzazi na chanjo kwa watoto.

Wito huo umetolewa wakati wa mdahalo kuhusu afya ya mama na mtoto ulioandaliwa na Serikali ya Tanzania kwa wajumbe wa Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), unaoendelea katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC).


Akifungua mdahalo huo Oktoba 8, 2026, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mussa Azzan Zungu, amesema mabunge yana wajibu wa kutunga sheria, kutenga fedha za kutosha na kusimamia matumizi yake ili kuhakikisha rasilimali zinafika kwenye huduma za afya na jamii zinazozihitaji.

Zungu amesema afya na ustawi wa wanawake, watoto na vijana ni msingi wa maendeleo ya taifa, akisisitiza umuhimu wa kuimarisha upatikanaji wa huduma za mama na mtoto mchanga, afya ya uzazi, lishe na huduma za vijana. Ameongeza kuwa hatua za kisiasa zinapaswa kuleta matokeo ya kudumu kwa kuondoa vikwazo vinavyozuia wananchi kupata huduma hizo.

Amesema Bunge lina jukumu la kuendeleza sheria, kuhakikisha fedha za kutosha zinatengwa na kusimamia utekelezaji kuhakikisha rasilimali zinafika kwenye huduma za mstari wa mbele na kwa jamii.

“Kipaumbele chetu kiwe kwenye upatikanaji sawa wa huduma, ikiwemo huduma za mama na mtoto mchanga, afya ya uzazi, lishe, na afya na ustawi wa vijana.

Kwa upande wake, Mshauri wa Rais anayeshughulikia masuala ya afya, ustawi wa jamii, wanawake na watoto, Ummy Mwalimu, aliyemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, amesema vifo vya kina mama katika nchi wanachama wa Umoja wa Afrika vilipungua kwa asilimia 42 kati ya mwaka 2000 na 2023. Hata hivyo, amesema bara hilo bado linachangia takribani asilimia 70 ya vifo vya kina mama duniani na haliko kwenye kasi ya kufikia lengo la vifo 70 kwa kila vizazi hai 100,000 ifikapo mwaka 2030.

Mwenyekiti wa Kundi la Kijiografia la Afrika la IPU, Ali Kolotou Tchaïmi, na Spika wa Bunge la Afrika Kusini, Angela Thokozile Didiza, wameeleza umuhimu wa uongozi wa kisiasa na usimamizi wa serikali kuhakikisha ahadi za afya zinawafikia wananchi, hususan wanawake, watoto na makundi yaliyo katika mazingira hatarishi..

Post a Comment

أحدث أقدم