Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Ndugu Baraka Leonard, amesema Bunge la Tanzani lipo tayari kujifunza na kushirikishana uzoefu kutoka mabunge mengine Duniani.
Katibu wa Bunge ameeleza hayo Oktoba 7, 2026 wakati akitoa hotuba katika Mkutano wa Makatibu wa Bunge wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU). Makatibu hao wanashiriki Mkutano wa 153 wa IPU unaoendelea jijini Arusha katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa Arusha (AICC).
“Tunatambua kuwa hakuna Bunge linalojua kila kitu, mbinu yetu ni kujifunza kutoka kwa wengine na kushirikishana uzoefu,” amesema.
Akizungumia mifumo mbalimbali ya kibunge, amesema hakuna mfumo mmoja ulio bora zaidi ya mwingine na kwamba tofauti ya mifumo hiyo ya kibunge ndiyo inayofanya Umoja huo wa Makatibu wa Bunge kuwa muhimu.
“Tunapotazama mifumo tofauti ya kibunge iliyopo hapa, tunakumbushwa kuwa hakuna mfumo mmoja ulio bora zaidi. Wengine mna mfumo wa mabunge mawili, wengine kama Tanzania tuna Bunge moja.Tofauti hii ndiyo inayofanya umoja huu kuwa muhimu sana.
“Tunakutana si kupanga ni mfumo gani bora zaidi, bali kuelewa ni nini kinachofanya kazi, kwa nini kinafanya kazi na ni mafunzo gani tunaweza kuyachukua,” amesema katibu wa Bunge.
Amesema Umoja wa Makatibu wa Bunge unatoa fursa ya kipekee ya kujifunza kutoka kwa kila Bunge kuhusu taratibu za kibunge, jinsi taasisi za kibunge zinavyohifadhi mwendelezo, kusaidia Wabunge, kukabiliana na mabadiliko na kubaki na ufanisi katika mazingira yanayobadilika kwa kasi.
Akizungumzia kuhusu mabadiliko kwenye Mabunge amesema, Bunge la Tanzania linafanyia kazi mazingira ya mabadiliko ya haraka ikiwemo mabadiliko katika ya matarajio ya wananchi, mabadiliko ya kiteknolojia na kuogeza uwazi.
“Bunge la Tanzania limeingia katika mfumo wa kidijitali kupitia mfumo wa Bunge Mtandao (e-Parliament), ambao unawawezesha Wabunge kupata nyaraka kwa njia ya mtandao na kufanya kazi bila karatasi.
“Pia tumeongeza upatikanaji wa shughuli za Bunge kwa umma. Vikao vya Bunge hurushwa kupitia Televisheni ya Bunge na mitandao ya kijamii. Bunge letu lipo wazi kwa wananchi wanaotaka kufuatilia shughuli moja kwa moja, hasa wanafunzi,” amesema.
Katibu wa Bunge aliwakaribisha wageni wote Arusha ambao ni washirika katika usimamizi wa shughuli za kibunge.
“Mimi na timu yangu tumeandaa kila kitu kuhakikisha mkutano huu unatoa mazingira muafaka ya kubadilishana uzoefu, kujifunza na kushirikiana kitaalamu.
“Arusha kwa muda mrefu imehusishwa na diplomasia, majadiliano, ushirikiano wa kikanda na ushiriki wa kimataifa, Mkutano huu pia unakuja katika wakati muhimu sana katika historia ya taasisi za kibunge nchini Tanzania,” amesema.
==


Post a Comment