Ad

BRELA yaibukia Arusha, yaanika siri ya kulinda bidhaa sokoni dhidi ya wajanja

 

Msaidizi wa Usajili Mkuu kutoka Kurugenzi ya Miliki Bunifu ya BRELA,Nassoro Mtavu  

Filbert Rweyemamu,Arusha

Wakati ushindani wa kibiashara ukizidi kushika kasi nchini, Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imewatahadharisha wafanyabiashara, wasanii na wabunifu kuhusu hatari ya kuacha alama zao za biashara bila kusajiliwa, hatua inayoweka rehani utambulisho wa bidhaa zao sokoni. 


Onyo hilo limetolewa leo Oktoba 9, 2026 na Msaidizi wa Usajili Mkuu kutoka Kurugenzi ya Miliki Bunifu ya BRELA, Nassoro Mtavu, wakati akizungumza na washiriki wa Maonyesho ya Kimataifa ya Utalii wa Sanaa na Utamaduni yanayoendelea jijini Arusha. 


Mtavu amekiri kuwa mwamko wa usajili wa alama za biashara na huduma nchini Tanzania bado upo chini, hali inayowafanya wazalishaji wengi kupoteza haki ya kulinda majina, nembo au utambulisho wa bidhaa zao pale zinapogezwa au kuchanganywa na za watu wengine sokoni. 


"Kwenye eneo hili, mfanyabiashara mwenyewe ataamua kusajili ili kulinda kampuni yake, jina la biashara, alama au uvumbuzi wake," amesema Mtavu. 


Amefafanuzi kuwa sheria inampa mjasiriamali uhuru wa kuchagua kama anataka biashara yake itambulike kisheria kama kampuni au kwa jina la biashara tu kulingana na malengo yake. 


Mtaalamu huyo ameweka wazi tofauti ya kisheria iliyopo kati ya usajili na utoaji wa leseni, akibainisha kuwa wakati usajili wa alama au jina la biashara ni uamuzi wa hiari wa mfanyabiashara, sheria inakataza kabisa mtu yeyote kuendesha kiwanda au kufanya biashara bila kuwa na leseni halali. 


Katika maonyesho hayo, BRELA imeweka kambi kutoa elimu kwa umma kuhusu huduma zake, zikiwemo usajili wa kampuni za ndani na nje, majina ya biashara, hakimiliki za uvumbuzi, pamoja na utoaji wa leseni za viwanda na leseni za biashara za kundi A zenye wigo wa kitaifa na kimataifa.


 Wasanii wanufaika wa warsha iliyotolewa na BRELA jijini Arusha

Mmoja wa wananchi waliohudhuria Tamasha hilo kwenye uwanja wa General Tyre jijini Arusha na kunufaika na elimu inayotolewa na BRELA,Sarah Lengai amesema elimu waliyoipata imempa ufahamu mzuri atakaoutumia kwaajili ya kuanzisha biashara yake kwa kuzingatia sheria za nchi.

 

mwisho

Post a Comment

أحدث أقدم