Mkuu
wa bandari ya Mtwara, Nelson Mlali (Kulia) akitoa maelezo kwa
Wakurugenzi wa Bodi wa TPA wa Kamati za TEHAMA na Utekelezaji pamoja na
ya Uwekezaji na Maendeleo ya Biashara mara baada ya wajumbe wa kamati
hizo kufanya ziara ya kikazi bandari ya Mtwara hivi karibuni.
Na Mwandishi Wetu
Mamlaka
ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imenunua vitendea kazi vipya na
vya kisasa kwa ajili ya bandari ya Mtwara ili kuongeza ufanisi.
Vifaa
hivyo ambavyo tayari baadhi vimeshawasili bandarini hapo ni pamoja na
mzani wa kisasa ‘Movable Weigh Bridge’ wenye uwezo wa kupima hadi tani
100 ambao tayari unatumika.
Vifaa
vingine vilivyonunuliwa na vinavyotarajiwa kuwasili kuanzia mwezi
Januari, 2018 ni pamoja na ‘Reach Stalker’ mbili mpya zenye uwezo wa
kubeba tani 40 kwa wakati mmoja.
Mkurugenzi
Mkuu wa TPA, Mhandisi Deusdedit Kakoko ameyasema hayo wakati wa
majumuisho ya ziara za Kamati za Bodi za Wakurugenzi wa TPA
zinazoshughulikia TEHAMA na Utelekezaji na ile ya Uwekezaji na Maendeleo
ya Biashara.
Wakurugenzi
wa Bodi za Kamati hizo ambazo ziliongozwa na Mwenyekiti, Dkt. Jabiri K.
Bakari, ni pamoja na Jayne K. Nyimbo, Renatus Mkinga, Aziz M. Kilonge
na Jaffer S. Machano.
Kamati
hizo zilitembelea miradi mbalimbali iliyopo Bandari za Mtwara na Lindi
na kutoa maelekezo kadhaa ambayo ni muhimu katika kuendeleza bandari
hizo ili kuongeza huduma zake.
Akizungumzia
vifaa vipya vilivyowasili na vinavyotarajiwa kuwasili hivi karibuni,
Mhandisi Kakoko amesema ununuzi wa vifaa hivyo ni utekelezaji wa mipango
ya kuifanya bandari hiyo kuwa ya kisasa zaidi.
“Ununuzi
wa vifaa tunaofanya sasahivi utasaidia kuboresha na kuimarisha zaidi
utendaji kazi wa bandari ya Mtwara na kuongeza ufanisi zaidi,” amesema
Mhandisi Kakoko.
Mhandisi
Kakoko ameongeza kwamba vifaa vingine ambavyo mchakato wa manunuzi
umeshafanyika ni pamoja na mzani mwingine wa pili wa kisasa ‘Movable
Weigh Bridge’ wenye uwezo wa kupima hadi tani 100 pia.
Amevitaja
vifaa vingine kuwa ni pamoja na boti maalum za kuhudumia mafuta
‘Mooring Boat’ moja na boti moja ya ulinzi ‘Pilot Boat’.
Mbali
ya vifaa hivyo, bandari ya Mtwara pia itapokea ‘Terminal Tractors’ 9 -
matrekta maalumu yanayovuta ‘matrela’ yaliyopakiwa kontena au makontena
yakiwa bandarini.
Bandari
ya Mtwara pia inatarajia kupokea mashine maalum ya kubebea makontena
‘Empty Container Handler’, folklift mbili moja ya tani 16 na nyingine
tani 20 pamoja na ‘Automatic Glab moja ya tani 15.
Kama
sehemu ya ziara hiyo, Mhandisi Kakoko pia alifanya kikao na maofisa wa
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mtwara na kuwaagiza kukutana na
Mawakala wa Forodha wa Mtwara ili kuwaelimisha umuhimu wa kutoa mizigo
ya wateja kwa wakati.
Awali
akitoa maelezo kwa Kamati ya Bodi ya Wakurugenzi wa TPA
inayoshughulikia TEHAMA na Utelekezaji, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA
(Miundombinu) Mhandisi Karim Mattaka amesema vifaa hivyo vitawasili
bandari ya Mtwara kuanzia mwezi ujao.
“Tunatarajia
kuanza kuwasili kwa vifaa hivyo hapa Mtwara kuanzia mwezi ujao
(Januari, 2018) ili kuharakisha mpango kazi wetu wa kubadili bandari
hii,” amesema.
Naye
Mkuu wa Bandari ya Mtwara, Bw. Nelson Mlali amesema kwamba kuna
ongezeko la mizigo la wastani wa asilimia 16.5 kwa mwaka kwa kipindi cha
miaka mitano.
“Katika
mwaka 2016/2017, Bandari ya Mtwara imehudumia wastani wa tani 377,590
za mizigo ambazo ni sawa na asilimia 93 ya uwezo wa bandari, ambapo
uwezo wake ni kuhudumia tani 400,000 kwa mwaka” amesema.
Bw.
Mlali amesema kwamba ongezeko hilo limechangiwa zaidi na ongezeko la
uzalishaji wa Korosho ambalo ndilo zao kuu la biashara kwa mikoa ya
kusini.
Amesema
kwamba zao la Korosho ambalo hulimwa zaidi na wakazi wa mikoa ya kusini
hupitishwa katika bandari ya Mtwara na kusafirishwa moja kwa moja
kwenda nchi za Vietnam na India.
Kwa
mwaka huu pekee bandari ya Mtwara ambayo ina uwezo wa kuhudumia meli
zenye urefu hadi wa mita 211 imefanikiwa kusafirisha wastani wa tani
160,000 za Korosho hadi kufikia Disemba, 2017.
Mkuu
huyo wa bandari ya Mtwara amepongeza juhudi zilizofanywa na Serikali ya
Awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli kuagiza Korosho
zote zisafirishwe kupitia bandari ya Mtwara.
Mbali ya Korosho bandari ya Mtwara pia uhudumia shehena nyingine za mizigo kama vile, saruji, vifaa mbalimbali na mafuta
No comments:
Post a Comment