Pages

October 6, 2013

WAHAMIAJI HARAMU WA KIAFRIKA 114 WAFARIKI DUNIA KATIKA KISIWA CHA LAMPEDUSA NCHINI ITALIA.


 

  Wahamiaji haramu wengi wao wanaotoka pembe ya Afrika.


Miongoni mwa waliofariki yupo mtoto wa miaka 3 na mama mjamzito. 


Na Margreth Itala. 

IDADI YA WAAFRIKA waliofariki imefikia 114 mpaka sasa,150 wameokolewa na wengine 250 hawajulikani walipo, ajali hiyo imetokea jana ambapo boti iliyokuwa imejazwa na wahamiaji kutoka Afrika, kuzama karibu na kisiwa cha Lampedusa nchini Italia.

Kufuatia ajali hiyo, rais wa Italia Giorgio Napolitano ametoa rai ya kuimarisha ulinzi katika pwani za Afrika kaskazini ili kuzuwia wahamiaji kujaribu kuingia barani Ulaya. 


Napolitano ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa na Umoja wa Ulaya kushirikiana kukomesha usafirishaji haramu wa binaadamu, na kusisitiza kuwa haikubaliki kwamba Frontex, wakala wa Umoja wa Ulaya anaeshughulikia usalama wa mipakani haupewi vitendea kazi vya kutosha ili kuweza kuingilia kati pasipo kuchelewa. 

karibu abiria 500, wengi wao wakiwa raia wa Eritrea walipanda boti hiyo nchini Libya, na askari wanaolinda pwani wamesema manusura 151 wameokolewa baada ya boti hiyo yenye urefu wa mita 20 kushika moto na kuzama yapatayo kilomita moja kutoka kisiwani Lampedusa.

Taarifa zilizoifikia Fahamutz zinaeleza kuwa idadi kubwa ya waliofariki ni wanawake na watoto, pia chanzo cha habari kimesema kuwa wengi wa wahamiaji hao waliokuwa katika boti hiyo hawajui kuogelea.

Meya wa mji wa Lampedusa Giusi Nicolini ameielezea ajali hiyo kama maafa makubwa, na kuongeza kuwa miongoni mwa waliofariki alikuwepo mtoto mwenye umri wa miaka mitatu na mama mjamzito. 


Kisiwa cha Lampedusa kiko karibu zaidi na Afrika kuliko Italia bara, kikiwa umbali wa kilomita 113 kutoka pwani ya Tunsia, na ndiyo kimekuwa kituo cha mwisho kwa boti zinazosafirisha watu kwa njia za magendo.

Pichani, mhamiaji haramu mwanamke aliyenusurika katika ajali hiyo akipatiwa huduma katika hospitali mjini Lampedusa.
Meli za ulinzi wa pwani, boti za uvuvi na helikopta zilikuwa zinafanya msako katika bahari hiyo kutafuta manusura.


Chanzo cha ajali
Waziri wa mambo ya ndani wa Italia, Angelino Alfano aliwaambia waandishi wa habari kuwa boti hiyo ilianza kuzama baada ya kuzimika kwa injini yake moja, na abiria hawakuwa na simu kuweza kuomba msaada, na kwa hivyo waliwasha moto mdogo ili kuomba msaada kwa meli zilizokuwa zinapita.

Waziri Alfano ameongeza kuwa kwa kuwa gesi ilikuwa imechanganyika na maji yaliyoingia katika meli hiyo, moto ulisambaa katika meli yenyewe, na kuwalaazimu abiria kukimbilia upande mmoja, hatua iliyosababisha meli hiyo kupinduka na kuwamwaga abiria baharini. Hii ilikuwa ajali ya pili kutokea wiki hii karibu na Italia.


Siku ya Jumatatu wanaume 13 walizama wakati wakijaribu kuufikia mji wa Sicily,pale meli yao ilipopinduka ikiwa imebakiza mita chache kutia nanga. Papa Francis ambaye alitembelea kisiwa cha Lampedusa mwezi Julai katika ziara ya kwanza ya upapa nje ya jiji la Rome, alielezea kusikitishwa kwake na roho nyingi zilizoteketea katika ajali hiyo.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...