Ad

BASATA yataja fursa za mikopo na Akili Mnemba (AI) kuinua uchumi wa wasanii nchini.


Filbert Rweyemamu,Arusha

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limewataka wasanii na mafundi sanifu nchini kujisajili kwa wingi ili kunufaika na Mfuko wa Utamaduni na Sanaa unaotoa mitaji na mikopo wezeshi, huku likihimiza matumizi ya teknolojia mpya ikiwemo Akili Mnemba (AI) ili kupenya kwenye soko la kimataifa.

Mkurugenzi Msaidizi wa Sanaa za Ufundi kutoka Baraza la Sanaa Tanzania (Basata) Bona Leon Masenge amesema hayo  wakati akifunguza Tamasha la Sanaa Arusha lililoenda sambamba na Tamasha la Kimataifa la Utalii Tanzania (TITF) jijini hapa.

Akizungumza katika tamasha hilo lililounganisha mashirika ya Hakimiliki Tanzania(Cosota), Brela na Bodi ya Filamu Tanzania, Masenge amesema kuwa uchumi wa ubunifu ni sekta rasmi inayobeba historia na ajira za maelfu ya vijana na wanawake nchini, hivyo haupaswi kutazamwa kama sehemu ya burudani au mapambo pekee.

"Serikali imeweka mazingira wezeshi kupitia Mfuko wa Utamaduni na Sanaa ili wasanii wapate mitaji,ili kunufaika na fursa hizi ni muhimu wasanii wetu na mafundi watambulike na wajisajili na taasisi husika ikiwemo Basata," amesema Masenge.

Kuhusu changamoto ya upatikanaji wa masoko ya uhakika ya bidhaa zao, amesisitiza umuhimu wa wasanii hao kushiriki kwenye matamasha ya ndani na nje ya kibiashara na kuwahimiza wasanii kutumia mifumo ya kiteknolojia na AI ili kuboresha chapa zao na kuongeza tija ya uzalishaji wa bidhaa za mikono.

Aidha, Basata imetoa wito kwa sekta binafsi na taasisi za kifedha nchini kuacha kuwatazama wasanii kama watu wanaohitaji misaada bali wawaone kama wajasiriamali na washirika halisi wa kibiashara wenye uwezo mkubwa wa kukuza uchumi wa nchi.

Masenge amewataka wananchi kujenga utamaduni wa kupenda na kununua bidhaa za ndani, akieleza kuwa kukuza vipaji vya nyumbani kutaifanya nchi kugeuza utamaduni wake kuwa chanzo kikuu cha maendeleo bila kusubiri sifa kutoka kwa wageni wa nje ya nchi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tanzania International Tourism Festivals (TITF),Ibrahim Othman amesema serikali imezindua ajenda ya Taifa ya Maendeleo ya Mafundi na Uchumi wa Ubunifu mkakati wa miaka mitano unaolenga kuifanyia mapinduzi makubwa sekta ya sanaa na utamaduni nchini.

Amesema ajenda hiyo mpya inayobebwa na nguzo sita kuu, inatarajiwa kuzalisha takribani  Sh1.3 trilioni kila mwaka, huku ikilenga kutengeneza ajira 600,000 kwa vijana na wanawake ifikapo mwaka 2030.

Ameongeza kuwa tamasha hilo la siku tano la sanaa na utamaduni linaloshirikisha wasanii zaidi ya 100, amesema tamasha hilo si maonesho tu ya kawaida, bali ni sura mpya ya juhudi za serikali kuinua uchumi wa wananchi wa chini.

“Jukwaa hili limekuwa ngazi ya kitaifa ambapo mafundi kutoka mikoa yote ya Tanzania, wakiwemo wasusi wa jamii za kimasai, wachongaji na wachoraji sasa wanaweza kusimama bega kwa bega na wawekezaji, wanunuzi na mabalozi wa sanaa,” amesema Othman 

Tamasha hilo limewaleta pamoja wabunifu wa sanaa za aina mbalimbali kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Zanzibar pamoja na nchi jirani wakionesha bidhaa zao kwaajili ya wanunuzi wa ndani na wageni.


Mwonekano wa kazi za Sanaa za mikono zinazooneshwa kwenye Tamasha la Sanaa Arusha.


Post a Comment

أحدث أقدم