Pages

March 15, 2015

MATUMIZI YA UZAZI WA MPANGO MKOA WA ARUSHA NI ASILIMIA 38 TUU

Mkuu wa wilaya ya Monduli,Jowika Kasunga akifungua Mkutano wa Wadau wa afya ya mkoa wa Arusha kwa niaba ya Mkuu wa mkoa huo,kushoto ni Katibu Tawala wa mkoa wa Arusha,Adoh Mapunda na Mganga Mkuu wa Mkoa,Dk Frida Mokiti.


Mkuu wa wilaya ya Karatu,Omari Kwaangw’(kushoto)akiteta jambo na Mkuu wa wilaya ya Monduli,Jowika Kasunga kabla ya kuanza mkutano wa Wadau wa sekta ya afya mkoa wa Arusha.

Mkuu wa wilaya ya Arusha,Christopher Kangoye(kushoto)akizungumza jambo na Diwani wa Kata ya Ngarenaro jiji la Arusha,Isaya Doita kwenye mkutano wa wadau wa afya mkoa kilichojadili mikakati ya kukabiliana na changamoto katika sekta hiyo.
Wadau wa afya mkoa wa Arusha wakiwa kwenye mkutano wa kujadili mafanikio na changamoto zinazoikabili sekta hiyo jijini Arusha.Picha na Filbert Rweyemamu
Filbert Rweyemamu
Arusha.Ukosefu wa elimu ya afya ya uzazi na namna bora ya matumizi ya njia sahihi za uzazi wa mpango unasababisha ongezeko la idadi ya watu ambalo haliendani na shughuli za kiuchumi jambo ambalo linaweza kusababisha madhara ya kijamii.

Changamoto hiyo imeelezwa kuwa ni kikwazo kikubwa cha maendeleo ndani ya jamii kwa kuwa ongezeko la idadi ya watu haliendani na hali ya uchumi hivyo wananchi  kushindwa kupata huduma bora za afya.

Akizungumza katika kikao cha wataalam wa afya mkoa wa Arusha,Mkuu wa wilaya ya Monduli,Jowika Kasunga kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Arusha,Felix Ntibenda alisema kuwa jitihada  za makusudi zinahitajika kwa wataalam wa huduma za afya kutoa elimu kwa wananchi ili kutumia njia sahihi za uzazi wa mpango.

Kasunga alisema kutokana na takwimu za mwaka 2014 matumizi ya njia za uzazi wa mpango ni asilimia 38  wakati lengo la kitaifa ni kufikia asilimia 60.

“Jambo la matumizi ya uzazi wa mpango ni muhimu iwapo wananchi hawatotumia njia za uzazi wa mpango kutasababisha  ongezeko la idadi ya watu katika familia ambapo halilingani na  uchumi hivyo ni vyema wakaangalia namna mpya ya kusaidia ,”alisema Kasunga

Hata hivyo  alitaja changamoto nyingine kuwa ni pamoja na upungufu wa vyumba vya dharura vya Upasuaji katika wilaya mbalimbali  hali ambayo inachangia vifo vya wagonjwa  pindi wanapohitaji huduma hizo huku kiwango cha unyonyeshaji kwa kipindi cha miezi sita ya mwanzo kimkoa  kiko chini ya asilimia 21 wakati lengo la kitaifa ni asilimia 80. 

Alitaja changamoto nyingine ni idadi ndogo ya mahudhurio ya wajawazito kwenye vituo vya afya chini ya wiki 12 za ujauzito yako chini ya kiwango kwa halmashauri zote pia idadi ndogo ya wajawazito kujifungulia kwenye vituo vya afya.

Hata hivyo alisema kuwa juhudi za makusudi zinahitajika kwa wadau wote wa afya katika kuhakikisha kuwa wanaboresha huduma bora ya afya na kutazama namna ambavyo wanaweza kuendana na kasi ya maendeleo.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa mkoa wa Arusha  Frida Mokiti alisema kuwa kumekuwepo na mafanikio katika wilaya za Longido na halmashauri ya Meru  kutokana na ushirikiano na wadau wa sekta ya afya kukutana na wazee wa mila za kimasai ambao wanaweza kuleta matokeo chanya katika jamii.

Mokiti alisema kuwa jamii inaweza kubadilika ikiwa kama elimu hii ya afya ya uzazi itatolewa pia kwa viongozi mbali mbali ya mila kwa kuwa wanamchango mkubwa katika jamii.

Hata hivyo alisikitishwa na mkoa na asilimia 5.6 ya waliojiunga kwenye mfuko wa afya ya jamii jambo ambolo linakwamisha huduma za afya kwa wananchi.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...