Pages

January 19, 2018

KURASA ZA MAGAZETI YA TANZANIA NA UINGEREZA IJUMAA JANUARI 19,2018

DK. MAHIGA AHIMIZA MAZINGIRA MAZURI KUVUTIA WAWEKEZAJI

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Dk.Augustine Mahiga amesema kuwa ili kufikia uchumi wa viwanda ni muhimu kutengeneza mazingira mazuri ya kuwavutia wawekezaji katika sekta mbalimbali zikiwamo za sheria, kodi, ajira,vvivutio vya uwekezaji na kilimo.

Dk.Mahiga, ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam wakati anazungumza na waandishi wa habari baada ya kumaliza kuzindua kongamano la siku mbili lililoandaliwa na Ubalozi wa India nchini Tanzania kwa kushirikisha nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) pamoja na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).

Lengo la kongamano hilo pamoja na mambo mengine washiriki wamezungumzia namna ya ushiriki wa sasa na siku zijazo unavyoweza kuleta amani katika nchi wanachama wa jumuiya hizo.Kauli mbiu ya kongamano katika kongamano hilo inasema "Amani, utulivu na maendeleo".

Dk. Mahiga amefafanua jambo hilo si jipya kuzungumzwa isipokuwa bado halijaeleweka na hivyo linatakiwa kuzunguzwa Tanzania pamoja EAC.

“Tunamkakati madhubuti wa kujenga viwanda katika EAC na SADC. Sasa kusema nataka viwanda ni kingine, kuvuta viwanda ni kingine, kufanya viwanda vizalishe na vistawi ni jambo lingine.

"Na ukisema unataka viwanda mazingira yapo?  unataka kufanikisha viwanda je  utaalam upo? hapo sasa kupitia mambo hayo matatu unaweza kuendesha viwanda,” amesema Dk.Mahiga.

Ameongeza katika kongamano hilo watazungumzia kinadharia kuhusu amani na jumuiaya hizo zinavyochagia kuleta amani katika nchi na namna mchanganyiko wa amani unavyoweza kuleta maendeleo katika mataifa hayo yanayoshirikiana.

Amewakumbusha washiriki wa kongamano hilo kuwa "Hapa tumekumbuka mchango wa mwanaharakati mkubwa Mahatma Ghandhi aliyeliyesisimua dunia kutokana na mapambano yake na Waingereza ili kuleta uhuru wa wa India na viongozi wengi wa Afrika waliiga mfano huo na hata Hayati Mwalimu Jualias Nyerere aliwahi kusema kuwa alijifunza kutoka kwake.

Pia Dk. Mahiga amesema nchi ya India ni kubwa na ina watu zaidi ya Sh.bilioni 1.2 na wana amani na wamekuwa wakifanya uchaguzi kwa demokrasia na kubwa zaidi wamejiimarisha kiuchumi na kuwa miongoni mwa nchi ambazo uchumi wake upo imara na kueleza ipo haja kwa nchi nyingine kuiga kutoka Taifa hilo.

"Amani inaweza kutazamiwa ndani ya nchi kama unatengeneza taasisi za  ushirikishi na uwajibikaji na si tu kudumisha amani bali kuleta utulivu wa kisiasa,"amesema Dk.Mahiga.

Naye aliyewahi kuwa Balozi wa Kwanza nchini India mwaka 1994 na Waziri Mkuu Mstaafu, Dk. Salim Ahmed Salim, amesifu uhusiano wa kidiplomasia uliopo kati ya Tanzania na India na hayo ni matunda ya Hayati Mwalimu Nyerere na Waziri Mkuu wa kwanza wa India  Jawaharial Nehru.

Kwa upande wa Balozi wa India nchini, Sandeep Arya, amesema pamoja na kujadili masuala ya ushirikiano Serikali ya India itatumia fursa ya kongamano hilo kukusanya maoni, mapendekezo na taarifa ambayo yatatolewa na washiriki waliopo na pamoja na wadau hasa wamasuala ya ulinzi, amani na maendeleo ili kila Taifa lifikie malengo ya kitaifa na kuboresha maisha ya wananchi wake.

Ameelezea namna ambavyo India imekuwa ikishirikiana na nchi zilizopo Bara la Afrika ikiwamo Tanzania katika kufanikisha upatikanaji wa maendeleo kwenye nyanja mbalimbali.
 Waziri Mkuu Mstaafu, Dk. Salim Ahmed Salim akizungumza leo jijini Dar es Salaam kwenye Kongamano la siku mbili lililoandaliwa na Ubalozi wa India nchini Tanzania kwa kushirikisha nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) pamoja na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Dk.Augustine Mahiga akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati akifungua rasmi Kongamano la siku mbili ambalo limeandaliwa na Ubalozi wa India nchini Tanzania.Kauli mbiu ya kongamano hilo ni Amani, Utulivu na Maendeleo.

MAAZIMIO YA MKUTANO KATI YA SMZ NA SMT KUSHUGHULIKIA MELI ZINAZOPEPERUSHA BENDERA YA TANZANIA KWA TUHUMA ZA KUSAFIRISHA SILAHA NA MADAWA YA KULEVYA, TAREHE 17 JANUARI 2018

Ndugu Waandishi wa Habari, nimewaita hapa kuzungumza nanyi na kupitia kwenu kuzungumza na wananchi wenzangu kuhusu taaarifa ya kukamatwa kwa meli zilizokuwa zimepakia shehena za dawa za kulevya na silaha zikiwa zinapeperusha bendera ya nchi yetu.

Meli hizo ni: 

Kaluba yenye usajili namba IMO 6828753 iliyokamatwa tarehe 27 Desemba 2017 ikiwa na wastani wa kilo 1,600 za dawa za kulevya huko katika maeneo ya Jamhuri ya Dominican Republic; na 

Andromeda yenye namba za usajili IMO 7614666 iliyokamatwa kwa kusafirisha silaha kinyume na Sheria za kimataifa. 
Meli zote mbili zimesajiliwa Tanzania kupitia taasisi yetu ya Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar ambayo ndiyo imepewa mamlaka ya kusajili meli za nje.
Hapa kwetu Tanzania tuna aina mbili za kusajili Meli; usajili wa Meli zenye asili ya Tanzania na zile zenye asili ya Nje. kwa kuzingatia kuwa Tanzania ni nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa na mashirika yake mbalimbali, siku zote tumekuwa tunaheshimu na kutekeleza kikamilifu majukumu yetu ya kimataifa yaliyowekwa kupitia mikataba na maazimio mbalimbali ya vyombo hivyo

Ndugu Waandishi wa Habari, kwa mujibu wa mkataba wa UNCLOS 1982 kila nchi imepewa haki ya kufanya usajili wa meli kwa kuzingatia mikataba ya kimataifa na sheria za nchi husika.Kwa upande wa Tanzania, usajili wa meli za kimataifa unasimamiwa na Sheria Na 5 ya mwaka 2006,

(Kwa upande wa SUMATRA ina Merchant Shipping Act ya mwaka 2003. Sheria hi inaruhusu usajili wa meli inayomilikiwa na Mtanzania, au meli inayomilikiwa kwa ubia kati ya Mtanzania na raia wa nchi nyingine. Kwa sheria hii ili meli ipate usajili wa SUMATRA na kuruhusiwa kupeperusha bendera ya Tanzania ni lazima umiliki wa meli uhusishwe na raia wa Tanzania kwa umiliki wote au kwa ubia lakini ni lazima Mtanzania awe na hisa nyingi. Vilevile kampuni hiyo ya umiliki lazima iwe ya Kitanzania kwa maana ya kusajiliwa na kujiendesha kutokea Tanzania hata kama kampuni hiyo inamilikiwa na watu wasio Watanzania. Na kwa upande wa Zanzibar kupitia ZMA wana Maritime Transport Act ya mwaka 2006).

Sheria hii inaruhusu usajili wa meli yoyote hata kama mmiliki wake sio Mtanzania wala kampuni kuwa ya Kitanzania hivyo basi kutoa fursa kwa meli ambayo haina umiliki wa aina yeyote wa Tanzania kwa maana umiliki na ukazi kupewa usajili wa kupeperusha bendera yetu nje ya Tanzania. Aidha, Sheria hizi huendeshwa sambamba pamoja na Sheria na Kanuni za Kimataifa.
Ni vyema tukafahamu kuwa Sheria na Kanuni hizo humlazimu mwenye Meli, kujaza fomu maalumu ya maombi pamoja na Fomu za “DECLARATION OF VESSELS NON INVOLVEMENT WITH CRIMINAL ACTS OR OMISSIONS”; na ndipo hatua nyingine za kufanya uchunguzi wa historia ya meli kupitia International Maritime websites na vyanzo vingine, tangu Meli ilipotengenezwa hadi muda inapoomba usajili.
Uhakiki hufanywa pia kupitia mitandao mingine mikubwa mitatu inayotumika duniani kote kupata historia ya meli, Mitandao hiyo ni:

Fleet Moon; 
Maritime Traffic; na 
iii. Maritime-connector.

Baada ya ZMA ambayo ndio kisheria imeruhusiwa kusajili meli nje ya Tanzania, kujiridhisha na maelezo na taarifa zilizopatikana, maamuzi ya kusajili au kutosajili yanatolewa kupitia Idara ya Usajili.

Ndugu Waandishi wa Habari, kwa mujibu wa taratibu za Mkataba wa Kimataifa wa Kupambana na Usafirishaji wa Dawa za Kulevya, 1988 na Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa 1970 (2011).

nchi zilizosajili Meli zinazokamatwa hutakiwa kutoa kibali kwa Walinzi wa Mwambao wa Bahari wa nchi husika, na kwa Meli hizi, tulitoa kibali kwa Jeshi la Mwambao wa Marekani na Jeshi la Mwambao wa Ugiriki kuzikamata na kuzipekua meli hizo.
Baada ya kupata taarifa za upekuzi hatua za haraka zilizochukuliwa upande wetu ni kufuta Usajili wa Meli hizo.
Ndugu Waandishi wa Habari, Tanzania vilevile ni mwanachama wa Mkataba wa Kimataifa wa Kupiga Vita Usafirishaji Haramu wa Dawa za Kulevya (United Nations Convention Against Illicit Traffic of Narcotic Drugs and Psychotropic Substance, 1988) na pia ni Mwanachama wa Mkataba wa Kimataifa wa Kupiga Vita
Usafirishaji Haramu wa Silaha (United Nations Protocol Against Illicit Manufacturing of and Trafficking in Arms, their Parts and Components and Ammunition, Supplementing the United Nations Convention Against Transnational Organized Crime, 2001).
Kwa mnasaba huu, tunapenda kutoa taarifa kuwa Tanzania imejidhatiti na imedhamiria kutekeleza majukumu yake yaliyoelezwa katika mikataba hiyo ya kimataifa, ikiwemo kushirikiana na mataifa mengine pamoja na mashirika ya kimataifa katika kupiga vita usafirishaji wa dawa za kulevya na silaha. Nyote ni mashahidi kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Awamu ya Tano imetangaza vita dhidi ya watu wote wanaojihusisha na dawa za kulevya na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vimekuwa vikifanya kazi usiku na mchana kuhakikisha vinatokomeza kabisa uhalifu huo.

Hivyo basi, taarifa ya kukamatwa kwa meli zenye bendera ya Tanzania zikisafirisha dawa za kulevya na silaha ni kinyume na Sheria za nchi yetu na zile za kimataifa. Taarifa hizi zimeleta mshtuko mkubwa ndani ya nchi yetu. hasa kwa kuwa Tanzania imejipambanua kupambana na maovu hayo kwa kutumia nguvu zote.
Ndugu Waandishi wa Habari, kufuatia taarifa hizo, Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliniagiza kuitisha kikao cha dharura baina ya viongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wale wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuzungumzia kadhia hiyo.
Jana Jumatano, tarehe 17 Januari 2018, Viongozi na Wataalamu wa pande zote mbili wakiongozwa na mimi mwenyewe na Mhe. Balozi Seif Ali Idi, Makamo wa Pili wa Rais, Zanzibar tulifanya kikao kilichojadili masuala haya kwa kina huko Zanzibar.
Ndugu Waandishi wa Habari, baada ya majadiliano ya kina kuhusu masuala haya, kikao kilibaini yafuatayo: 
Suala la Usajili wa Meli za Nje linafanywa na Nchi nyingiduniani; Kwa mfano katika Bara la Afrika 
nchi zinazofanya usajili wa kimataifa ni pamoja na Liberia, Komoro na Sierra Leone. Aidha, kwa Bara la Asia, kuna nchi za China na Singapore na kwa Amerika ya Kusini ni pamoja na Panama.

Ilibainika kwamba Wenye Meli hupendelea kusajili meli zao nje ya nchi zao kwa kukimbia uzito wa kodi na sheria zinazobana shughuli zao. 

Wakala aliyekuwa akifanya kazi hii kwa niaba ya ZMA na ambaye ameshavunjiwa Mkataba bado anaendelea kufanya usajili kwa kuiba Bendera ya Tanzania. 
Kutokana na hayo kikao kiliazimia yafuatayo: 
Kutoa taarifa na ufafanuzi wa kina kuhusu kadhia ya meli hizo kukamatwa na dawa za kulevya na silaha kwa umma wa Watanzania na dunia kwa ujumla ili kuondoa upotoshaji wa aina yoyote kwa kupitia vyanzo visivyo rasmi. Kwa sasa ndio natekeleza azimio hili; 

Kwa kuwa uendeshaji wa biashara hii unaonekana kuleta utata na kutia dosari kubwa kwa Taifa letu na kuharibu sifa njema za Nchi yetu, imeonekana haja ya kuunda kamati ya pamoja ya wataalam wa SMZ na SMT itakayoshirikisha vyombo vya ulinzi na usalama kwa ajili ya kupitiwa upya usajili uliokwishafanyika na kuzihakiki taarifa za meli zote zilizosajiliwa nchini mwetu, kuangalia mwenendo mzima wa usajili, na hatimaye kutoa mapendekezo na ushauri kwa Serikali; 

Kuanzisha utaratibu wa kuzifanyia uchunguzi wa kina (due diligence) meli zote mpya zitakazoomba usajili pamoja na wamiliki wake kwa kushirikisha vyombo mbalimbali vya Serikali vikiwemo vile vya ulinzi na usalama; 
iii. Kufanya mapitio ya sheria zetu, ili kuzipa nguvu zaidi taasisi zinazosimamia usajili wa meli. Wakati wa mapitio ya sheria, timu ya wataalam itaangalia kwa makini kodi zinazotozwa na mchango wake nchini ili zisiwe kivutio kwa meli zisizokidhi viwango kuomba usajili Tanzania;

Kuendelea kushirikiana na nchi nyengine kwa kuzipa ruhusa kukamata na kuzipekua meli zinazopeperusha bendera yetu wakati wote zinapohisiwa kuwa zinafanya uhalifu, au masuala ambayo haziruhusiwi kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni zinazokubalika kimataifa na wakati wa usajili. 

Asanteni kwa kunisikiliza.

January 18, 2018

NAIBU WAZIRI WA MADINI MHE BITEKO AWATAKA WACHIMBAJI WADOGO WA GYPSUM KUWA NA UMOJA

Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Dotto Mashaka Biteko akiwasili kijiji cha Hoteli Tatu, Kata ya Mandawa Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi kwa ajili ya kuembelea kampuni ya Universal Mining Ltd kujionea hali ya uzalishaji wa jasi (Gypsum) unavyoendelea wakati wa ziara ya Siku tatu katika Mkoa wa Lindi na Mtwara, Leo 17 Januari 2018. Picha Zote Na Mathias Canal
Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Dotto Mashaka Biteko  akikagua uzalishaji wa madini aina ya Jasi (Gypusm) katika kijiji cha Hoteli Tatu, Kata ya Mandawa Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi, Leo 17 Januari 2018.
Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Dotto Mashaka Biteko  akizungumzia umuhimu wa wachimbaji wadogo kuwa na umoja ili kukuza ufanisi na tija katika kupanga bei ya rasilimali wanazozalisha wakati alipozuru kijiji cha Hoteli Tatu, Kata ya Mandawa Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi, Leo 17 Januari 2018.

Na Mathias Canal, Lindi

Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Dotto Mashaka Biteko Leo 17 Januari 2018 amewataka wachimbaji wadogo wa madini Jasi(Gypsum) kuwa na umoja na mshikamano katika uuzaji madini hayo na kuwa na kauli moja katika ushiriki wa soko la bidhaa hiyo.

Mhe Biteko ameyasema hayo alipotembelea katika kijiji cha Hoteli Tatu, Kata ya Mandawa Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi wakati wa ziara ya Siku tatu katika Mkoa wa Lindi na Mtwara ambapo pamoja na mambo mengine atakutana na makundi ya wachimbaji wadogo ili kubaini changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi.

Alisema kuwa kila mchimbaji anajipangia gharama aitakayo yeye pasina kushirikiana na wachimbaji wengine ili kuwa na bei moja ambayo itakuwa na tija na manufaa kwa kila mmoja hivyo kupitia umoja wao watakuwa na kauli na maamuzi ya pamoja yenye tija na faida kwao.

Mhe Biteko aliwashauri wachimbaji hao kuwa na umoja utakaokuwa na uwezo wa kudai bei itakayofanana kwa wote pia kuwa na uwezo wa kutengeneza sheria ndogondogo ambazo zitatumika kujisimamia wao wenyewe.

Aidha, amezitaja Changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi sambamba na wachimbaji wadogo hususani ubovu wa barabara ambapo ameishauri Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa kusaidia utengenezaji wa Barabara itakayorahisisha usafirishaji wa jasi (Gypusm) na kurahisisha huduma za wananchi ili kufika kwa urahisi katika Barabara kuu.

Mhe Biteko alisema kuwa serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais Dkt John Pombe Magufuli itaendelea na juhudi zake za kuweka miundombinu rafiki kwa ajili ya wananchi, wawekezaji, na wachimbaji (wakubwa na wadogo) hivyo ili kufikia adhma ya mafanikio hayo ni lazima kusema na kutekeleza maelekezo yote ili kupiga hatua za maendeleo.

Alibainisha kuwa nia ya sekta ya madini ni kufanya mchakato wa kuongeza pato la Taifa kufikia asilimia 10% tofauti na ilivyo hivi sasa ambapo sekta ya madini inachangia kiasi kidogo kwenye pato la Taifa.


WCF YAWANOA WAAMUZI, WASULUHISHI NA MAKATIBU MUHTASI KUTOKA TUME YA USULUHISHI NA UAMUZI(CMA) Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala, Wizara ya Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Bw.Peter Kalonga, (kushboto), akijadiliana jambo na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, (WCF), Bw. Masha Mshomba, (wkawanza kulia) na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Bw.Shanes Nungu, wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku tatu kwa Waamuzi, Wasuluhishi na Makatibu Muhtasi kutoka Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) mjini Morogoro leo Januari 17, 2018. Bw. Kalonga alimwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Bw. Eric Shitindi.
Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala, Wizara ya Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Bw.Peter Kalonga,kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Eric Shitindi, akifungua mafunzo hayo.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, (WCF), Bw. Masha Mshomba, akitoa hotuba yake.

NA K-VIS BLOG/Khalfan Said, Morogoro

MFUKO wa Fidia kwa Wafanyakazi, (WCF), umejipanga vema kuendelea kutoa huduma bora kwa wadau, hususan katika kipindi hiki ambacho Mfuko unategemea ongezeko kubwa la waajiri na wafanyakazi, kutokana na mkakati wa Serikali ya awamu ya tano wa kujenga uchumi wa viwanda, ambao utaongeza ajira.

Hayo yamesemwa leo Januari 17, 2018 mjini Morogoro na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, (WCF), Bw. Masha Mshomba wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku tatu kwa Waamuzi, Wasuluhishi na Makatibu Muhtasi kutoka Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), ili kuongeza ujuzi kwenye utekelezaji wa majukumu ya Tume.

“Katika jambo hili la kujenga uchumi wa viwanda,  makampuni mengi yataanzishwa, kutakuwa na waajiri wengi, ongezeko la wafanyakazi, kwa hivyo unategemea kwamba hitajio la utoaji huduma za Mfuko kwa wadau  litaongezeka na Mfuko umekuja wakati muafaka na tupo kwa ajili ya kuwahudumia wale wote watakaopatwa na majanga mahala pa kazi lakini pia kuelimisha.” Alisema Bw. Mshomba.

Bw. Mshomba  alisema, kuanzia Julai, 2016 Mfuko ulianza kupokea madai ya Fidia yanayotokana na kuumia au kuugua mahali pa kazi.

“Jambo hili si rahisi kwa sababu ndio linaanza kwa hivyo tunahitaji ushirikiano wa karibu sana kutoka kwa wadau mbalimbali mkiwemo ninyi CMA, na katika hilo ushirikiano tu hautoshi Mfuko umekuwa ukitoa elimu ili kuwawezesha watu  wajue Mfuko umeanzishwa kwa sababu gani, kazi zake, lakini pia kujua taratibu za kudai fidia pale mfanyakazi anapopatwa na majanga ya kuumia au kuugua wakati akitekeleza wajibu wake wa kikazi.” Aliongeza Bw. Mshomba.

“Ndio maana leo hii tunao wataalamu wetu watakaotoa mada mbalimbali zikiwemo, Sheria za Fidia, Namna Fidia inavyolipwa lakini shughuli za Mfuko.” Alibainisha Mkurugenzi Mkuu Bw. Mshomba.

Aidha aliishukuru Tume kwa kuwashirikisha WCF ili kuwaelimisha wafanyakazi wake kutoka mikoa yote ya Tanzania bara.

“Ni muhimu kwetu sisi kuwaelimisha wadau kuhusu shughulim zetu na ndio maana huwa tuko tayari wadau wetu wanapotualika ili kutoa elimu hiyo.” Alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa ……..kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira, na Wenye Ulemavu, Bw. Eric F. Shitindi amewahimiza washiriki wa kuzingatia elimu watakayoipata kwenye mafunzo hayo ili hatimaye watekeleze ipasavyo malengo ya serikali ya awamu ya nne ya kujenga uchumi wa kati ifikapo mwak 2025.

“Ni matarajio yetu kwamba Tume na Mfuko wa Fidia Kwa Wafanyakazi, mnao wajibu mkubwa sana katika kufanikisha azma hiyo ya serikali kama nyinyi mtatekeleza wajibu wenu.” Alisema.
Baadhi ya washiriki.
Baadhi ya washiriki.
Mwenyekiti wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Bw.Edrisa Mavura, akitoa hotuba yake.
Maafisa wa CMA wakiteta jambo.
Bw. Mshomba, (kulia), na Bw.Nungu, wakijadili jambo.
Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala, Wizara ya Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Bw.Peter Kalonga, akikaribishwa na Wakurugenzi wa WCF, Bw. Masha Mshomba, (kulia) na wa CMA, Bw.Shanes Nungu, alipofika kufungua mafunzo hayo
 Bw. Mshomba akijibu baadhi ya maswali ya washiriki kuhusu shughuli za Mfuko.
Baadhi ya washirtiki wakifuatilia mafunzo.
Kamishna wa Tume, Bi.Suzanne Ndomba, (kulia), akizungumza kwenye mafunzo hayo. Wengine ni Makamishna wenzake, kutoka kushoto, Bw.Kibwana Njaa, Bw.Jones Majura na Bw.Jaffary Ally Omar.
Picha ya pamoja.
Bw. Mashomba akibadilishana mawazo na Mkurugenzi wa Sheria wa WCF, Bw. Abraham Siyovelwa, (katikati) na Mkurugenzi wa Huduma za Tiba na Tathmini, Dkt. Abdulsalam Omar.
Washiriki wakipitia vipeperushi vya WCF.
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...