Pages

March 15, 2015

CHAHITA YAPANIA KUINUA UFAULU WA HESABU

Mwandishi Wetu ,Arusha.
Mwenyekiti wa Chama Cha Hisabati Tanzania (CHANITA) Emanuel  Kisongo amesema kuwa wamejipanga kuhakikisha kuwa wanawahimiza Wanafunzi kupenda somo la hisabati na kutoa mafunzo  sahihi kwa wanafunzi ili kuinua kiwango cha ufaulu na kukuza maendeleo ya jamii na nchi kwa ujumla kupitia hisabati.

Kisongo ameeleza  kuwa hakuna maendeleo bila hisabati  ambayo hutumika katika maisha ya kila siku hivyo amewataka wanafunzi kutilia mkazo somo hilo ili waweze kubobea katika fani mbali mbali za ujenzi,uhandisi  na nyingine nyingi ambazo huhitaji mahesabu.

“Hesabu inatumika katika maisha yetu ya kila siku unapokula,unapovaa ,unapotaka kujenga nyumba kila nyanja ya maisha inahitaji hesabu hivyo ukikosea hesabu umekosea maisha ndio maana tunawahamasisha wanafunzi kupenda hesabu”  Alieleza  Mwenyekiti huyo katika maadhimisho ya siku ya Pai duniani ambayo ni kanuni ya hesabu ya kimataifa inayotumika duniani kote yaliyofanyika katika shule ya msingi Arusha  jana.

Mlezi wa chama hicho ambaye pia ni Mkuu wa Shule ya Sekondari Arusha  Christopher Malamsha amewaasa walimu kuwahamasisha watoto kupenda hesabu na kutowaogopesha kuwa somo hilo ni gumu jambo ambalo linawarudisha nyuma  katika ufaulu wa somo hilo.

Malamsha  anaeleza kuwa juhudi zinapaswa kufanywa kuanzia ngazi za chini kuhakikisha kuwa wanafunzi wanafanya vizuri na kufaulu huku akitolea mfano kwa mwaka jana kiwango cha ufaulu kilikua asilimia 19% kwa mwaka huu wanatarajia kuvuka kiwango hicho na kwenda mbele zaidi.

Mwanafunzi wa shule ya Sekondari St.Jude Sifuni Ernest alisema kuwa chanzo cha wanafunzi kufeli ni kukosekana kwa walimu wa kutosha wa somo la hesabati,vifaa vya kufundishia na vitabu hasa katika shule za kata hivyo hali ikiboreshwa huenda ufaulu ukaongezeka na kwenda juu.

Glory Kimario Mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya sekondari Arusha  Day anaeleza kuwa tatizo ni mtazamo wa wanafunzi juu ya somo hilo kuwa ni gumu na hata kulibatiza jina kuwa ni ugonjwa wa taifa jambo ambalo si kweli ,kwake yeye hesabu ni rahisi kwasababu huwa anafanya mazoezi ya kukokotoa mara kwa mara.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...