Kaimu
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali katika Wizara ya Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Mkumbwa Ally akizungumza na
Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu hatua zilizochukuliwa na
Ubalozi wa Tanzania nchini Urusi katika kuhakikisha Wanafunzi kutoka
Tanzania wanaondoka katika Jimbo lenye machafuko la Lugansk huko
Ukraine. Mwingine katika picha ni Bw. Ally Kondo, Afisa Habari.
Mkutano ukiendelea (Picha na Reginald Philip)
Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa inapenda kukanusha vikali
taarifa iliyotangazwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC),
tarehe 30 Julai, 2014, iliyodaikuwa Serikali ya Tanzania imetelekeza wananchi wake wanaosoma Ukraine Mashariki, ambako kunarindima vita ya wenyewe kwa wenyewe.
Taarifa
hiyo ya upande mmoja, iliyomnukuu mtu anayeitwa Shamila, aliyedai ni
mmoja wa wanafunzi Watanzania nchini Ukraine, ilisema eti wananchi hao
wameachwa bila msaada wowote.
Wizara
imesikitishwa na taarifa hiyo iliyotolewa bila kufanyiwa uchunguzi wa
kutosha. Ukweli ni kwamba Ubalozi wa Tanzania nchini Urusi, ambao
unatuwakilisha pia Ukraine, umechukua hatua za haraka tangu mwezi Juni,
2014, kuhakikisha wanafunzi Watanzania wote wanaondoka katika jimbo la
Lugansk lililoko vitani.
Ubalozi
ulishirikiana na Rais wa wanafunzi wa Tanzania katika mji wa Lugansk,
Bwana Ahmad Juma, kufanikisha kuondoka kwa Watanzania wote 32
waliokuwepo huko kurudi nyumbani au kuhamia mji wa Kharkov, ambao ni
salama zaidi.
Serikali
kupitia Ubalozi wake Moscow iliwaombea wanafunzi hao malazi kwenye Chuo
cha Kharkov Technical University ambacho kilikubali kutoa hosteli kwa
wanafunzi hao. Hata hivyo, wengi wa wanafunzi hao waliondokea Lugansk
kurudi nyumbani isipokuwa wanafunzi saba ambao walihamia Kharkov. Mpaka
tarehe 31 Julai, 2014, ni wanafunzi watatu tu waliokuwa wamebaki mjini
Kharkov. Wanafunzi 20 wamedhaminiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
kupitia Bodi ya Mikopo.
Orodha ya
wanafunzi iliyopo Ubalozini haijumuishi jina la Shamila anayedaiwa
kuhojiwa na BBC. Inasemekana mtu huyo alikwishamaliza masomo yake ya
shahada ya kwanza na ya pili lakini akaamua kubakia Ukraine akifanya
udalali wa kuleta wanafunzi kutoka Tanzania kwa kushirikiana na vijana
wa Nigeria.
Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa inapenda kuuhakikishia Umma
kuwa inasimamia kikamilifu usalama na ustawi wa Watanzania walioko
Ukraine na popote ulimwenguni na inasikitishwa na taarifa ya uzushi,
upotoshaji na uzandiki iliyomnukuu mtu anayeitwa Shamila.
IMETOLEWA NA WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA DAR ES SALAAM
02 AGOSTI, 2014
No comments:
Post a Comment