Jeshi la Israel leo limetangaza kifo cha Hadar Goldin, mwanajeshi ambaye alipotea katika ukanda wa Gaza siku mbili zilizopita, huku hali ya umwagaji damu ikiendelea bila kuwa na matumaini ya kufikia mwisho.
Tume maalum inayoongozwa na mkuu wa masuala ya kidini wa jeshi hilo, rabbi , amesema luteni Goldin ameuwawa katika mapambano katika ukanda wa Gaza siku ya Ijumaa, jeshi la Israel limesema katika taarifa. Msemaji wa jeshi amekataa kusema iwapo mwili wa mwanajeshi huyo umepatikana ama la.
Upande wa Israel hapo kabla ulionesha hisia kuwa mwanajeshi huyo mwenye umri wa miaka 23 Goldin amekamatwa mateka na wapiganaji wa Hamas katika ukanda wa Gaza, na kutoa nafasi finyu ya kuwapo makubaliano ya muda mrefu ya kusitisha mapigano katika mzozo huo uliosababisha umwagikaji mkubwa wa damu.
Wanajeshi wa Israel ndani ya Gaza
Uchukuaji mateka unaonekana na Israel kuwa ni kama kuiweka nchi hiyo rehani.
Tawi la kijeshi la Hamas , la Ezzedine al-Qassam, limekiri kuwa wapiganaji wake wamefanya shambulio la kushitukiza mapema siku ya Ijumaa ambapo wanajeshi wawili wa Israel wameuwawa, lakini imekana kumshikilia Goldin.
Mazungumzo mjini Cairo
Kukiwa hakuna suluhisho linalowezekana kufikiwa hivi karibuni , ujumbe wa ngazi ya juu wa Wapalestina umewasili mjini Cairo kwa mazungumzo leo kuhusiana na juhudi za kusitisha mapigano zilizoanzishwa na Misri, lakini Israel imesema haitatuma ujumbe wa majadiliano.
"Hamas imethibitika kukiuka makubaliano yoyote yaliyokwisha fikiwa mara moja, kama ilivyotokea mara tano katika makubaliano yaliyopita," naibu waziri wa mambo ya kigeni Tzahi HaNegbi ameliambia shirika la habari la AFP.
Majumba yaliyoharibiwa Gaza
"Kwa hiyo haifahamiki katika wakati huu Israel itafaidika vipi kwa kushiriki katika juhudi hizo za kufikia makubaliano, chini ya msingi wa juhudi za Misri," ameongeza.
Mjumbe wa Marekani katika mashariki ya kati Frank Lowenstein anatarajiwa kuwasili kwa mazungumzo, pamoja na wawakilishi wa Hamas na Islamic Jihad.
Ghasia za Gaza zimesababisha vifo 1,712 kwa upande wa Wapalestina na wengine zaidi ya robo ya wakaazi wa eneo hilo wamekimbia makaazi yao. Kifo cha Goldin kinafikisha idadi ya wanajeshi 64 wa Israel waliouwawa tangu kuanza kwa mzozo huo Julai 8, ikiwa ni idadi kubwa kabisa kwa jeshi la Israel tangu vita vya mwaka 2006 dhidi ya kundi la Hezboullah nchini Lebanon.
Maandamano ya kupinga vita katika ukanda wa Gaza mjini Paris
Israel yaanza kuondoa vikosi vyake
Mapema jana Jumamosi Israel imeondoa vikosi vyake kutoka maeneo mawili ya Gaza katika kile kinachotafsiriwa kuwa ishara ya kufikisha mwisho operesheni yake kubwa katika miongo kadha dhidi ya ukanda wa Gaza.
Jeshi hilo limewaarifu wakaazi wa Beit Lahiya na Al-Atatra upande wa kaskazini kuwa ni salama sasa kurejea katika maeneo yao. Majeshi pia yalionekana kuondoka kutoka katika vijiji mashariki mwa Khan Yunis upande wa kusini, katika hatua ya kwanza tangu operesheni ya Israel kuanza mwezi uliopita.
Lakini hakuna ishara zaidi kuwa Israel inapanga kukamilisha operesheni yake, wakati waziri mkuu Benjamin Netanyahu akiahidi kuwa Hamas watagharamika pakubwa kwa kuendelea kufyatua maroketi katika ardhi ya Israel.
Maafisa wa hospitali wamesema kuwa kiasi Wapalestina saba wameuwawa leo katika mashambulizi mengine ya anga ya Israel dhidi ya ukanda wa Gaza. Wakati huo huo maelfu ya waandamanaji , wengi wao wakiwa wamejifunga bendera za Palestina waliandamana nje ya ikulu ya Marekani White House jana Jumamosi wakitoa wito wa amani na kumalizika kwa mapigano katika ukanda wa Gaza.
Maandamano kuwaunga mkono Wapalestina mjini Washington
Kundi hilo la watu , vijana na wazee kutoka sehemu mbali mbali nchini Marekani , ikiwa ni pamoja na watoto kadhaa wakiwa katika mabega ya baba zao, waliimba , "usitishwe msaada wa Marekani kwa Israel" na Israel iondoke Palestina."
No comments:
Post a Comment