Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainabu Telack amefanya ziara ya kukagua
kilimo cha zao la Pamba na Mtama wilayani Kishapu kwa ajili ya kuendelea
kuhamasisha wakulima kulima mazao hayo kwa wingi kwa njia za kitaalamu
ambayo yatawafanya wakue kiuchumi na mkoa kwa ujumla.
Telack amefanya ziara hiyo leo Jumatatu Januari 8,2018 wilayani
Kishapu kwa kukagua baadhi ya mashamba ya pamba na mtama ambayo
yamelimwa na wakulima kwa njia ya kitaalamu na kuwataka wakulima
kuendelea kutii magizo ya serikali kwa kulima mazao hayo ya biashara na
chakula ambayo yatabadili mfumo wa maisha yao pamoja na kuacha kuishi
kwenye nyumba za tembe.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara baada ya kutembelea mashamba ya
wakulima katika kijiji na kata ya Shangihilu Telack amewataka wakulima
kijijini kuendelea kujikita kulima mazao hayo ya pamba na mtama kwa njia
ya kitaalamu ambayo itawafanya kupata mavuno mengi na kuinuka
kiuchumi.
“Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na rais wetu mpendwa Dkt.
John Pombe Magufuli imejipanga kumuinua mkulima kiuchumi kupitia kilimo
na ndiyo maana changamoto zote zilizokuwa zikimkabili mkulima
zinatatuliwa ili muweze kunufaika na kilimo chenu , hivyo nawasihi mlime
mazao ya pamba na mtama kwa wingi kwani soko lake lipo”,alisema
Telack.
Aidha aliwataka wakulima hao pindi watakapouza mazao yao baadhi ya
fedha wazielekeze kwenye ujenzi wa nyumba za kisasa na kuondoa matembe
yaliyopo ili kuishi katika nyumba zenye usalama na zisizo na mashaka
hasa pale mvua zinapoanza kunyesha kwa hofu ya nyumba kuanguka.
Pia alitoa agizo kwa wakulima ambao wanalima mazao kwa kuchanganya
kwenye shamba moja wakamatwe na kushughulikiwa kisheria kwa sababu
wanaonekana kukaidi maagizo ya serikali ya kuhamasisha wakulima kulima
kilimo cha kisasa ambacho kitakuwa na tija kwa wananchi katika kuwainua
kiuchumi.
Naye mkuu wa wilaya ya Kishapu Nyabaganga Taraba akisoma taarifa ya
utekelezaji wa kilimo wilayani humo katika msimu wa kilimo (2017-18)
alisema asilimia 80 ya wakazi wilayani humo ambao wapo 298,554
wanategemea kilimo na katika msimu huu zaidi ya wakulima 24,216
wamejisajili kulima zao la pamba.
Alisema katika msimu huu (2017-18) wamelenga kulima zao la pamba
hekali 177,026 sawa na hekta 70,811 ambapo eneo hilo linahitaji tani
1,770 za mbegu za manyoya au Tani 1,062 za mbegu zisizo na manyoya, na
mpaka sasa wakulima wamelima hekta 52,095 na matarajio ya mavuno ni tani
169,454, au kilo milioni 100 za zao hilo.
Aliongeza kuwa bado wanaendelea kuandikisha wakulima watakao lima zao
hilo kwa vile kilimo bado kinaendelea pamoja na kuunda vyama vya
ushirika kwa kila kijiji ambavyo vitasaidia wakulima kuwa wamoja pamoja
na kuuza mazao yao kwa uhakika bia ya kupunjwa na kupata faida.
Nao baadhi ya wakulima wilayani humo ambao walibahatika kutembelewa
mashamba yao na mkuu wa mkoa,akiwemo Kazimiri Masunga walipaza kilio
chao kikuu ambacho kilikuwa ni wadudu waharibufu ambao wameonekana
kuishambulia pamba huku dawa ambayo wanaipulizia ya maji ya kuulia
wadudu kutokuwa na nguvu tofauti na ya zamani ya mafuta ambayo ilikuwa
bora zaidi.
Naye ofisa kilimo wa kata hiyo ya Shaghihilu Yona William alikiri
wadudu hao kushambulia pamba za wakulima na kutolea ufafanuzi kuwa dawa
ambayo wanaipulizia (Dudu all) ya kuulia wadudu hao baadhi yao
wanaikosea kwa kuzidisha vipimo na kujikuta inakosa nguvu na kutoua
wadudu hao.
Alisema baadhi ya wakulima wamekuwa wakikaidi kutohudhuria kwenye
mikutano ya hadhara ambayo hutoa elimu ya dawa hizo za kuulia wadudu
pamoja na kuifanya kwa vitendo kwenda kwenye moja ya shamba na matokeo
yake wanapoamua kutumia dawa hizo hujikuta wakiikosea na kutoua wadudu.
Kwa upande wake mkaguzi wa pamba kutoka wilaya ya Kishapu na
Shinyanga Thomas Tiluhongelwa alisema dawa zote za kuuliwa wadudu za
maji na mafuta zote ni bora isipokuwa dawa ya mafuta ina gharama na
ndiyo maana ilisitishwa kuingizwa nchini na kuruhusiwa hiyo ya maji
ambayo ina gaharama nafuu ambayo kila mkulima atakuwa na uwezo wa
kuinunua, isipokuwa wanatakiwa kufuata masharti yake ambayo hupewa na
wataalamu.
Habari imeandikwa na Marco Maduhu -Malunde1 blog
Mkuu
wa mkoa wa Shinyanga Zainabu Telack mwenye ushungi akiwa na mkuu wa
wilaya ya Kishapu Nyabaganga Taraba (katikati mwenye nguo ya njano) na
aliyepo mkono wa kushoto ni Diwani wa Kata ya Shangihilu Mohamed Hamadi
pamoja na wataalamu wa kilimo na mkurugenzi wa halmashauri hiyo Steven
Magoiga wakikagua shamba la pamba hekali 22 la mkulima Kazimiri Masunga
-Picha na Marco Maduhu- Malunde1 blog
Mkulima
wa zao la Pamba Kazimiri Masunga akimuonyesha mkuu wa mkoa wa Shinyanga
Zainabu Telack ukubwa wa eneo alilolima shamba hilo hekali 22, na
kutarajia kwenye mavuno kumuinua kiuchumi huku akiomba serikali
kuwapatia dawa ya kuua wadudu waharibifu ili wasipate hasara.
Mkuu
wa mkoa wa Shinyanga Zainabu Telack akiangalia wadudu
wanavyolishambulia zao hilo la pamba na kutoa maagizo kuhusu ufumbuzi
upatikane wa kuwateketeza kwa kupulizia dawa yenye nguvu ya kuua wadudu
ili kutowapatia hasara wakulima.
Viongozi wakiwemo wataalamu wa kilimo wakiangalia jinsi pamba ilivyoshambuliwa na wadudu
Mkaguzi
wa pamba wilaya ya Kishapu na Shinyanga kutoka bodi ya Pamba Thomas
Tiluhongelwa akiangalia wadudu wanavyo shambulia zao hilo la pamba na
kumuahidi mkuu wa mkoa kulifanyia kazi ndani ya Siku mbili ilikufahamu
ni wadudu wa aina gani wanaoshambulia zao hilo na kuwateketeza kabisa
Mkuu
wa mkoa wa Shinyanga Zainabu Telack akimpongeza mkulima wa zao la pamba
hekali 22 Kazimiri Masunga kwa kutii maagizo ya serikali kulima zao
hilo tena kwa kilimo cha kisasa.
Mke wa Kazimiri Felista Kija akipunguza mashina kwenye zao la pamba ili lipate kustawi vizuri
Mkuu
wa mkoa wa Shinyanga Zainabu Telack akiwataka wataalamu wa Kilimo kuwa
karibu na wakulima muda wote mashambani na kutoa elimu kwa wakulima
namna ya kupulizia dawa na kuwaua wadudu waharibifu pamoja na kuendelea
kulima kilimo cha kisasa
Mkuu
wa mkoa wa Shinyanga Zainabu Telack akisikiliza maelezo kutoka kwa
mkulima wa zao la Mtama Nkalango Ngiti Bundala mkazi wa kijiji cha
Mwataga ambaye amelima hekali 270 za Mtama baada ya kuhamasishwa na
serikali kupitia mkuu wa wilaya hiyo Nyabaganga Taraba
Mkulima
wa zao la Mtama Nkalango Ngiti Bundala mkazi wa kijiji cha Mwataga
akimwelezea mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Taraba namna alivyohamasika
kulima zao hilo
Eneo lililolimwa hekali 270 za zao la mtama na bwana Nkalango Ngiti Bundala
Mkuu
wa mkoa wa Shinyanga Zainabu Telack akiwataka wataalamu wa kilimo kuwa
karibu na wakulima muda wote mashambani na kutoa elimu kwa wakulima
namna ya kulima kwa njia za kitaalamu
Mkuu
wa mkoa wa Shinyanga Zainabu Telack akiwa kwenye mkutano wa hadhara na
wananchi wa kijiji cha Shangihilu na kuwataka walime kwa wingi mazao ya
pamba na mtama angalau kwa kila kaya kekali tatu ,tatu tena kilimo cha
kitaalamu ambacho kitawapatia mavuno mengi na kuinuka kiuchumi na
kubadirisha mfumo wa maisha yao pamoja na kuondokana na nyumba za
tembe.
Wananchi
wa kijiji cha Shangihilu wakiwa kwenye mkutano wa hadhara wakisikiliza
maagizo ya serikali ya kulima mazao ya pamba na mtama ,pamoja na
kusomesha watoto wao
Wananchi wakiwa katika mkutano
Wananchi wakimsikiliza mkuu wa mkoa wa Shinyanga
Viongozi wa CCM wakiwa kwenye mkutano huo wa hadhara wakisikiliza maagizo ya serikali ya kulima mazao ya biashara na chakula
Wananchi wakiwa katika mkutano.
No comments:
Post a Comment