Meneja
wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Dodoma, Mhandisi Leonard
Chimagu, akimuonesha Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, sehemu ya
ujenzi wa barabara ya mchepuo kutoka Chimwaga-Ihumwa yenye urefu wa KM
10 inayojengwa kwa kiwango cha lami kwa ajili ya kupunguza msongamano wa
magari yanayoingia mkoani humo.Mhandisi
Mkazi anayesimamia ujenzi wa barabara ya Chimwaga-Ihumwa KM 10 kwa
kiwango cha lami, Mhandisi Nicholaus Mzeru, akitoa taarifa ya maendeleo
ya mradi kwa waandishi wa habari ambapo mpaka sasa ujenzi wake umefikia
asilimia 92.4 na KM 8 zimeshakamilika kujengwa, mkoani DodomaNaibu
Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, akitoa maelekezo kwa Meneja wa
Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Dodoma, Mhandisi Leonard Chimagu,
wakati akikagua ujenzi wa barabara ya Mbande-Kongwa KM 11.7,
inayojengwa kwa kiwango cha lami, mkoani humo.Meneja
wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Dodoma, Mhandisi Leonard
Chimagu, akimuonesha Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, athari za
mvua eneo la katondo katika barabara za mji huo.Naibu
Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, akiongozana na Meneja wa Wakala wa
Barabara (TANROADS), mkoa wa Dodoma, Mhandisi Leonard Chimagu, wakikagua
athari za mvua eneo la Kibaigwa, katika barabara ya Dodoma-Dar es
Salaam.Naibu
Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, akizungumza na Waziri wa Fedha na
Mipango, Dkt. Philip Mpango, alipokutana nae wakati akikagua athari za
mvua eneo la Kibaigwa, katika barabara ya Dodoma-Dar es Salaam.Muonekano
wa sehemu ya barabara ya mchepuo ya Chimwaga-Ihumwa yenye urefu wa KM
10 inayojengwa kwa kiwango cha lami, mkoani Dodoma.
………………………………………………………………………….
Naibu
Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, amesema kuwa ujenzi wa barabara ya
Mbande – Kongwa (Km 11.7) na Chimwaga – Ihumwa (Km 10) utasaidia
kupunguza msongamano kwa magari yanayoingia Dodoma mjini.
Naibu
Waziri huyo ameyasema hayo wakati akikagua barabara hizo na kuridhishwa
na kasi ya ujenzi wake ambapo amesisitiza kwa makandarasi wanaojenga
barabara hizo kuhakikisha wanamaliza kazi hizo kwa muda uliopangwa na
kwa viwango vilivyo kwenye mkataba.
“Tutaendelea
kujenga na kuboresha barabara hizi za mchepuo lengo ni kupunguza foleni
katikati ya mji kwani Dodoma sasa inakua kutokana na uwepo wa watumishi
wengi wa Serikali na ongezeko la magari, kwa hiyo sisi kama Serikali
hatuna budi kuangalia namna ya kuboresha miundombinu yetu ili ikidhi
haja ya ongezeko hili”, amesema Naibu Waziri Kwandikwa.
Aidha,
amefafanua kuwa barabara hizo zikikamilika zitakuwa ni njia mbadala kwa
watumiaji kwani sio lazima kwa magari yote kupita mjini na badala yake
yatatumia njia nyingine za mchepuo kuendelea na safari zake.
Katika
hatua nyingine, Naibu Waziri Kwandikwa amekagua athari za mvua katika
barabara za mji wa Dodoma na kuwataka wananchi na madereva kuchukua
tahadhari ili kuepusha hatari zinazoweza kuwakabili wakati wakivuka ama
kupitisha magari yao katika kipindi hiki ambacho baadhi ya sehemu za
barabara zinajaa maji kutokana na mvua nyingi zinazoendelea kunyesha.
Amewaomba
viongozi mbalimbali wa Serikali kushirikiana katika kutoa ushauri kwa
wananchi kuhusu utafutaji wa maeneo yanayowafaa kuishi ili kunusuru
maisha yao na mafuriko ambayo yanaweza kuwakabili kutokana na kuchagua
maeneo yasiyo sahihi kwa makazi ya binadamu.
Kwa
upande wake, Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Dodoma,
Mhandisi Leonard Chimagu, amefafanua kuwa barabara ya Mbande- Kongwa
yenye urefu wa KM 11.7, kwa sasa imejengwa kilometa Tano ikiwa ni awamu
ya kwanza na kufikia mwezi ujao watajenga tena kilometa nyingine Tano.
Naye,
Msimamizi wa ujenzi wa barabara ya Chimwaga – Ihumwa yenye urefu wa KM
10 kwa kiwango cha lami, Mhandisi Nicholaus Mzeru, amesema mradi ulianza
mwaka 2013, ambapo kwa sasa umefika asilimia 92.4 na kilometa 8 tayari
zimeshajengwa.
Ujenzi
wa Barabara ya Chimwaga- Ihumwa (Km 10), inajengwa na mkandarasi Nyanza
Road Works kwa gharama ya takriban shilingi bilioni 15 ambapo ujenzi
wake unaendelea na unategemewa kukamilika mwezi Aprili mwaka huu.
No comments:
Post a Comment