WAZIRI
wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla amewaagiza wahifadhi
wote nchini kushirikiana na wadau wengine hasa mamlaka za Mikoa na
Wilaya katika maeneo yenye uvamizi wa mifugo na migogoro ya mipaka ya
hifadhi ili kutatua changamoto hizo kwa namna shirikishi ikiwa ni pamoja
na kuimarisha utoaji wa elimu kwa wananchi wanaozunguka maeneo hayo.
Ametoa
agizo hilo Disemba, 16, 2017 katika Wilaya ya Mlele Mkoani Katavi
wakati akifunga mafunzo ya 15 ya mabadiliko ya kuelekea mfumo wa Jeshi
Usu kwa Maafisa wa Wanyamapori 87 wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori
Tanzania– TAWA, Shirika la Hifadhi za Taifa – TANAPA na Mamlaka ya
Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro.
“Kazi
ya ulinzi wa rasilimali zetu za asili ni yetu na tutaiendeleza, Falsafa
yetu ni kuwashirikisha wadau wote, kama kuna taasisi za kiraia kwenye
eneo lako la kazi, taasisi za kijamii, mamlaka za mikoa na wilaya,
wananchi, halmashauri husika mshirikiane nao ili kupunguza madhara ya
operesheni zetu, na zoezi hili la uhifadhi liwe endelevu,” alisema Dk.
Kigwangalla.
Aidha,
alitoa wito kwa wananchi wote kuendelea kuheshimu Sheria za nchi na
kuacha kufanya shughuli za kibinadamu kwenye maeneo ya hifadhi ikiwemo
kuingiza mifugo, kuanzisha kilimo, makazi na ukataji wa miti kwa ajili
ya kuchoma mkaa na matumizi mengineyo.
Awali
akizungumzia mafunzo hayo alisema, lengo ni kubadilisha utendaji katika
sekta ya uhifadhi kutoka ule wa kiraia kwenda wa jeshi usu ambao
utaongeza nidhamu, uwajibikaji, uadilifu na maadili kwa watumishi wote
wa sekta hiyo ili waweze kusimamia ipasavyo uhifadhi endelevu wa
maliasili za taifa.
Alisema
katika kuelekea mfumo huo, Jeshi hilo litakuwa moja bila kubagua
taasisi yeyote ambayo ipo chini ya Wizara yake. “Sheria ya Wanyamapori
namba 5 ya mwaka 2009 inampa Waziri mamlaka ya kuunda Jeshi Usu,
haikusema jeshi la TAWA, TFS, TANAPA au NGORONGORO na kwa vile hili
jeshi ni langu nataka liwe moja, na tunakimbiza mchakato huu kwa haraka
ukamilike kwa mujibu wa Sheria.
“Tunafarajika
Mhe. Rais ameshaunga mkono na ameshatupa maelekezo, Mwenyekiti wa
Kamati ya Vyombo vya Ulinzi na Usalama ambaye ni Mkuu wa Jeshi la Ulinzi
naye ameshasaini, ni sisi sasa tuendelee kujipanga vizuri ndani ya
wizara, tuanze kuishi kwenye mfumo huo, kuanzia kwenye sare, uratibu wa
mafunzo, uongozi na mfumo wa utawala,” alisema Dk. Kigwangalla.
Alisema
mfumo huo wa Jeshi Usu utakuwa na mnyororo mmoja wa mamlaka (chain of
comand) na kwamba utahusisha taasisi zote za uhifadhi zilizopo chini ya
wizara yake kwenye sekta ya wanyamapori, misitu na mali kale. “Sijawaona
watu wa misitu hapa au mambo ya kale, wote hawa ni ni muhimu,
rasilimali za mali kale nazo ni muhimu sana kulindwa kwani zikiharibika
hazitengenezeki tena” alisema.
Katika
hatua nyingine amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kuhakikisha kuwa
mafunzo yote ya Jeshi Usu ambayo yanaendelea katika kituo cha Mlele,
Mkoani Katavi yanaratibiwa moja kwa moja na Wizara tofauti na ilivyo
hivi sasa ambapo uratibu unafanywa na taasisi zilizopo chini ya Wizara
hiyo.
Akizungumzia
mafanikio ya vita dhidi ya ujangili na matunda ya mafunzo hayo alisema,
“Katika siku za hivi karibuni tumepiga hatua kubwa ya kupambana na
ujangili hasa wa tembo, Kwa dhati napongeza jitihada zinazofanywa na
zinazoendelea kufanywa na wahifadhi, maaskari watumishi wengine na wadau
wetu wote kwa ujumla ambazo zimeimarisha hali ya uhifadhi wa maliasili
zetu”.
Alisema
kwa kiasi kikubwa matukio ya ujangili yamepungua na kwamba nyara nyingi
zinazokamatwa katika kipindi hiki ni za zamani ambazo zilikuwa
zimefichwa na majangili kwa ajili ya kuzitafutia masoko au kukimbia
mikono ya sheria.
Alisema
Wizara yake itaendelea kutumia mbinu za kisasa za kiitelijensia za
kukabiliana na ujangili ikiwemo kutumia ndege zisizo na rubani kwa ajili
ya doria na kuweka mifumo ya kisasa ya mawasiliano ambayo haitaweza
kuingiliwa na majangili au watu wengine wenye nia ovu na uhifadhi.
Kwa
upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori wa Wizara hiyo,
Dk. Nebo Mwina akitoa nasaha zake kwa wahitimu wa mafunzo hayo ya Jeshi
Usu, aliwataka kuishi kwenye viapo vyao kwa kudumu katika ukakamavu,
uhifadhi, maadili mema na nidhamu.
Naye
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania –
TAWA, Dk. James Wakibara aliwataka wahitimu hao kutumia mafunzo
waliyopewa kufanya kazi kwa uaminifu na uadilifu kwa kudhibiti mianya ya
upotevu wa mapato ya Serikali, kujiepusha na rushwa na kudhibiti
vitendo vya ujangili.
Mhifadhi
Gloria Bidebeli kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania –
TAWA akisoma risala ya wahitimu hao alisema mafunzo hayo yatawawezesha
kuboresha ufanisi wa shughuli za uhifadhi kwa kutii amri na kutekeleza
maagizo kwa wakati.
Mafunzo
hayo ya wiki nne ambayo yalianza Novemba, 20 mwaka huu yalihusisha
Mameneja wa Mapori ya Akiba na Tengefu 20, Wakuu wa Kanda wa Kikosi
Dhidi ya Ujangili wanane, Maafisa Wanyamapori 29 kutoka Mamlaka ya
Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania – TAWA, Wahifadhi Wanyamapori watano
kutoka TANAPA na Wahifadhi Wanyamapori 26 kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya
Eneo la Ngorongoro.
Mafunzo
hayo yalihusisha matumizi sahihi ya silaha, mbinu mbalimbali za
kupambana na uhalifu, huduma ya kwanza, ukakamavu, sheria mbalimbali
zinazosimamia maliasili, ukamataji na upekuzi wa wahalifu na jinsi ya
kuwafungulia hati za mashtaka.
Tangu
kuanzishwa kwa mafunzo hayo Septemba 2015 jumla wahifadhi 1468 wakiwemo
Askari wa Wanyamapori na Viongozi mbalimbali kutoka TAWA, TANAPA na
NGORONGORO wameshapatiwa mafunzo hayo katika kituo hicho cha Mlele.
No comments:
Post a Comment