Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Taasisi ya Okoa Moyo
wa Mtoto (Save a Child Heart – SACH) ya nchini Israel wamefanya upasuaji
wa bila kufungua kifua (Catheterization) kwa watoto 20 wenye matatizo
ya Moyo.
Upasuaji
huo ambao unatumia mtambo wa Cathlab umefanyika katika kambi maalum ya
matibabu iliyoanza tarehe 23/11/2017 na kumalizika kesho tarehe
27/11/2017. Matibabu yaliyofanyika ni ya kuziba matundu kwenye moyo na
kutanua mishipa ya moyo.
Katika
kambi hii tunatarajia kufanya uchunguzi wa moyo kwa watoto 100 kati ya
hao watoto 60 ambao watakuwa na matatizo makubwa watapelekwa nchini
Israel kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji wa kufungua kifua mwakani na
watoto 40 watatibiwa hapa nchini.
Tumepanga
kufanya matibabu kwa watoto 25 tunaamini hadi kambi itakapomalizika
watoto wote hawa watakuwa wamepata matibabu. Watoto 20 waliopata
matibabu wengine wameruhusiwa na waliobaki hali zao zinaendelea vizuri
na wataruhusiwa pindi afya zao zitakapoimarika.
Tangu
mwaka 2015 Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete ilianza kushirikiana na
Taasisi ya Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child Heart- SACH) ya nchini
Israel ambapo hadi sasa jumla ya watoto 40 wamefanyiwa upasuaji wa moyo
nchini Israel. Gharama za matibabu ya watoto hawa zinagharamiwa na
Taasisi hii.
Tunawashukuru
sana wenzetu hawa wa SACH kwa kuona umuhimu wa kutoa huduma ya matibabu
bure kwa watoto wenye matatizo ya moyo. Watoto waliotibiwa wamepona na
wale ambao walikuwa wanafunzi wanaendelea na masomo yao.
Wakati
kambi hii inaendelea baadhi ya wafanyakazi wa SACH na JKCI walienda
mkoani Kagera kufuatilia maendeleo ya mtoto Julius Kaijage (12)
mwanafunzi wa darasa la nne katika shule ya msingi Green Acres iliyoko
Bunazi ambaye alifanyiwa upasuaji wa moyo nchini Israel mwaka 2013.
Tumekuwa na tabia ya kufuatilia maendeleo ya watoto tunaowafanyia
upasuaji hii inatusaidia sana kufahamu maendeleo yao.
Aidha
tunatarajia kuwa na kambi nyingine ya matibabu ya moyo kwa watoto na
watu wazima itakayoanza kesho tarehe 27/11/2017 hadi tarehe 01/12/2017.
Katika kambi hii ambayo tutashirikiana na wenzetu kutoka Taasisi ya Open
Heart International ya nchini Australia tunatarajia kufanya upasuaji wa
kufungua kifua kwa watoto 13 na watu wazima 10.
Tunawaomba
wananchi waendeleee kuchangia damu kwani wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji
wa moyo wanahitaji kuongezewa damu wakati wanapatiwa matibabu. Kwa mtu
mmoja mmoja au kikundi cha watu wanaopenda kuchangia damu tunawaomba
wafike Taasisi ya Moyo iliyopo Muhimbili mkabala na Maabara kuu. Kwa
maelezo zaidi wawasiliane kwa simu namba 022-2151379au 0713304149.
Kama
mnavyofahamu matibabu ya moyo ni ya gharama hivyo basi tunaendelea
kuwahimiza wananchi kujiunga na mfuko wa taifa wa bima ya afya ambao
utawasaidia kulipa gharama za matibabu pindi watakapougua na kuhitaji
kupata matibabu.
Kwa
namna ya kipekee Bodi ya Udhamini, Uongozi na Wafanyakazi wote wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete tunamshukuru sana Mhe. Rais John Pombe
Magufuli katika hotuba yake aliyoitoa tarehe 25/11/2017 wakati wa
ufunguzi wa Hospitali ya Taaluma na Tiba ya chuo kikuu cha Afya na
Sayansi shirikishi Muhimbili kampasi ya Mloganzila kwa kutupatia jengo
ambalo tutalifanya kuwa jengo la watoto.
Kama
mnavyofahamu asilimia 70 ya wagonjwa tunaowafanyia upasuaji wa kufungua
kifua ni watoto, tuna jumla ya vitanda 123 kati ya hivi vitanda vya
watoto ni 24 tu.
Kuwa
na jengo la watoto kutasaidia watoto kupata sehemu nzuri ya matibabu
pamoja na sehemu ya kujifunza mambo mbalimbali kwani watoto wanahitaji
kucheza na kujifunza. Watoto wengine wanakaa wodini muda mrefu
wakisubiri matibabu, watoto hawa wakiwa na mahali pa kujifunzia wataweza
hata kujifunza kusoma na kuandika.
No comments:
Post a Comment