Mkuu
wa Mkoa wa Singida amewataka watumishi wa umma wote mkoani hapa kulima
ekari moja ya korosho ili kutunza mazingira, kujiongezea kipato pamoja
na kuonyesha mfano kwa wananchi wengine ili waweze kulima zao hilo kwa
ufanisi.
Dkt
Rehema Nchimbi ametoa agizo hilo mapema wiki hii mara baada ya
kutembelea na kukagua shamba la mkulima wa zao hilo Juma Patrick katika
kijiji cha Sanjaranda halmashauri ya wilaya ya Itigi.
Dkt
Nchimbi amesema kuongoza ni kuonyesha njia hivyo watumishi wa umma
wanatakiwa kuonyesha njia kwa kulima vizuri hasa katika mazao ya
biashara yanayopewa kipaumbele kitaifa ambapo kwa mkoa wa Singida ni
korosho, pamba na tumbaku.
“Watumishi
hamuwezi kuwaambia wakulima walime korosho au pamba wakati wewe
haujalima wala haufahamu changamoto na faida za kilimo hicho, naagiza
kila mtumishi alime ekari moja ya korosho ili muwe mabalozi wazuri wa
zao hilo mkoani hapa”, amesisitiza Dkt Nchimbi.
Aidha
Dkt Nchimbi ametoa wito kwa wananchi wote kuchangamkia fursa ya kilimo
cha korosho kwakuwa ndio mkombozi wa kutunza mazingira kwa mkoa huu
pamoja na kuinua pato lao.
Amesema
pembejeo na miche ya zao hilo inatolewa bure hivyo mwananchi hataingia
gharama nyingine zaidi ya kuandaa shamba lake ambalo atavuna mara baada
ya miaka mitatu tangu kupanda na kuendelea kuvuna kwa zaidi ya miaka 50.
“Wananchi
korosho ni zao zuri sana, serikali ya awamu ya tano inatoa mbegu na
pembejeo bure, nyie andaeni mashamba yenu tu lakini pia ukianza kuvuna
korosho yako hiyo baada ya miaka mitatu utaendelea kuvuna kwa zaidi ya
miaka hamsini, hii ni faida kubwa sana.
Dkt
Nchimbi amefafanua kuwa Mkoa wa Singida umejipanga kuifanya korosho kuwa
zao la kudumu la biashara mkoani hapa na kuwa mzalishaji mkubwa nchini
wa korosho.
Kwa
upande wake mkulima Juma Patrick wa kijiji cha Sanjaranda halmashauri ya
wilaya ya Itigi amesema anamiliki ekari 11 za korosho ambapo kwa msimu
wa mwaka 2015/2016 alivuna kilo 410 na msimu wa mwaka 2016/2017 alivuna
kilo 826.
Patrick
amesema mavuno yamekuwa ni kidogo kutokana na kutopata elimu ya kilimo
hicho huku akiwa hafahamu namna ya kupata soko la korosho yake licha ya
kuwa ardhi na mazingira ya Singida yanastawisha korosho vizuri.
Aidha
amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kukagua shamba lake na kwa agizo lake la
kuwataka watendaji wa halmashauri kuwatembelea wakulima ili wawape
pembejeo na elimu ya kilimo bora cha korosho.
Patrick
ametoa wito kwa wananchi wote hasa vijana kuchangamkia kilimo cha
korosho kwa kuwa ni zao ambalo linastawi vizuri, linatunza mazingira na
kukuza uchumi pamoja na kutohitaji uangalizi mkubwa hivyo kutoa nafasi
ya kuendelea na shughuli nyingine huku ukiwa umepanda korosho.
Mkuu
wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi akisisitiza jambo wakati akikagua
shamba la korosho la mkulima Juma Patrick wa Kijiji cha Sanjaranda
halmashauri ya Wilaya ya Itigi.
Mkulima
Juma Patrick wa Kijiji cha Sanjaranda halmashauri ya Wilaya ya Itigi
akimuonyesha Mkuu wa Mkoa wa Singida mikorosho iliyostawi katika shamba
lake.
Mkuu
wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya
Manyoni Miraji Jumanne Mtaturu wakiwa katika shamba la korosho la
mkulima Juma Patrick wa Kijiji cha Sanjaranda halmashauri ya Wilaya ya
Itigi.
Shamba la mikorosho lenye ukubwa wa ekari 11 la mkulima Juma Patrick lililoko halmashauri ya Wilaya ya Itigi likiwa limestawi.
No comments:
Post a Comment