Kaimu
Mkurugenzi Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Bw. Lazaro
Kitandu akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam
kuhusu mfumo mpya wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja (Bulk Procurement
System). Kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka
Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Bw. Richard Kasuga. Picha na Fatma
Salum- MAELEZO
Na Fatma Salum (MAELEZO)
Serikali
kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea nchini (TFRA) imeanzisha mfumo
mpya wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja (Bulk Procurement System) kutoka
nje ya nchi utakaosaidia kupunguza bei na kuhamasisha matumizi ya mbolea
kwa wakulima.
Akizungumza
na Waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu
wa Mamlaka hiyo Bw. Lazaro Kitandu alisema uamuzi huo wa kuanzisha mfumo
mpya umekuja baada ya Serikali kugundua kuwa kwa muda mrefu matumizi ya
mbolea hapa nchini si ya kuridhisha kutokana na bei ya mbolea kuwa juu.
“Serikali
kupitia Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na wadau wa
masuala ya mbolea imeanzisha mfumo huu baada kupitia tafiti mbalimbali
zilizofanywa na wataalam waelekezi wa ndani na nje ya nchi na kutumia
uzoefu wa taasisi nyingine zinazofanya ununuzi wa bidhaa kwa pamoja”
Alisema Kitandu.
Kitandu
alieleza kuwa katika nchi zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara (SSA),
Tanzania ni mojawapo ya nchi zenye matumizi ya chini ya mbolea kwa
kutumia kilo 19 za virutubisho hivyo kwa hekta katika ngazi ya wakulima
wadogo ambapo kiasi hicho hakiendani na malengo ya azimio la Maputo la
nchi za SADC linalotaka kufikia angalau kilo 50 kwa hekta moja.
Alisema
kuwa kwa msimu wa mwaka 2017/2018 mfumo huo utaanza na aina mbili tu za
mbolea ambazo ni mbolea ya kupandia (DAP) na mbolea ya kukuzia (UREA)
na mbolea nyingine zitafuata baadaye kadri itakavyoonekana mfumo huo
kuleta manufaa kwa wakulima.
Akifafanua
kuhusu faida za mfumo wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja, Kitandu alisema
utasaidia kuimarisha utaratibu wa usambazaji wa mbolea ambapo wadau wote
watakuwa na uhakika wa upatikanaji wa mbolea kwa bei ya ushindani.
Kwa
mujibu wa Kitandu pia mfumo huo utawezesha wafanyabiashara wadogo kukua
na kushiriki katika biashara ya mbolea na kuimarisha mtandao wa
usambazaji hadi ngazi ya mkulima.
“Ununuzi
wa mbolea kwa pamoja pia utasaidia kudhibiti bei ya mbolea iwapo
kutajitokeza ongezeka lisilokuwa na sababu (soko holela) kwa kuwa bei
itatangazwa kwa kuzingatia bei halisi ya mbolea, gharama halisi za
usafirishaji wa mbolea, tozo mbalimbali na kiwango stahiki cha faida ya
mfanya biashara” alibainisha Kitandu.
Serikali
kupitia mfumo huu inatarajia matokeo chanya katika kupunguza bei ya
mbolea kwa wakulima hivyo kuongezeka kwa matumizi ya mbolea na
uzalishaji wenye tija ili kuchochea maendeleo ya uchumi wa viwanda.
No comments:
Post a Comment