Waandishi wa habari wakimsikiliza Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi CCM, Itikadi na Uenezi Ndg Humprey Polepole wakati wa Mkutano wake na Waandishi wa Habari katika ukumbi wa Mikutano Ofisi ndogo ya CCM Lumumba Jijini Dar es salaam.
Katibu
wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi CCM, Itikadi na Uenezi Ndg
Humprey Polepole akizungumza na Waandishi wa Habari katika ukumbi wa
Mikutano Ofisi ndogo ya CCM Lumumba Jijini Dar es salaam.
Na Mathias Canal, Dar es salaam
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimempongeza
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli
ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa kwa kutekeleza sera na kuisimamia
ilani ya ushindi ya CCM ya mwaka 2015/2020 na kuwaomba watanzania wote
kwa kauli moja pasina itikadi za vyama kumuunga mkono kwani atakuwa
imara na madhubuti zaidi katika utendaji wake iwapo ataungwa mkono na
watanzania wote.
Chama cha Mapinduzi (CCM) Kimetoa pongezi hizo kutokana na maamuzi
yaliyofanywa na Rais Magufuli mara baada ya kupokea Ripoti ya kamati
iliyokuwa inachunguza Hatma ya mchanga wa madini iliyoundwa na Rais
Magufuli Machi 29 mwaka huu ikiwajumuisha Profesa Abdulkarim Hamisi
Mruma (Mwenyekiti), Profesa Justiania Rwezaura Ikingula, Profesa Joseph
Bushweshaiga, Dokta Yusuph Ngenya, Dokta Joseph Yoweza Phili, Dokta
Ambrose Itika, Mohamed Zengo Makongoro na Hery Issa Gombela.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi
CCM, Itikadi na Uenezi Ndg Humprey Polepole wakati akizungumza na
Waandishi wa Habari katika ukumbi wa Mikutano Ofisi ndogo ya CCM Lumumba
Jijini Dar es salaam.
Polepole alisema kuwa uamuzi wa kuundwa kwa kamati hiyo ulitokana na
kukamatwa kwa makontena 277 ya mchanga huo katika bandari ya Dar es
salaam Machi 23 Mwaka huu baada ya Rais kufanya ziara ya kushitukiza
katika bandari hiyo na kukuta makontena 20 yakiwa mbioni kusafirishwa
kinyume cha maelekezo yake ya Machi 2 ya kuzuia kusafirisha mchanga huo
nje ya nchi.
Alisema kuwa huu sio wakati wa kulumbana
na kutofautiana kisa itikadi za vyama bali ni wakati wa kusimama pamoja
na kuikabili vita ya kiuchumi kwani kwa kuzingatia taarifa iliyosomwa
na Profesa Mruma mbele ya Rais Magufuli imebainisha jinsi Taifa
lilivyopata hasara ya mabilioni ya fedha kwa kuwa makontena
yaliyozuiliwa bandarini yana thamani ya madini yaliyomo kwa kiwango cha
wastani wa shilingi Bilioni 829.4 na kiwango cha juu ni Shilingi Trioni
1.4
"Tumeibiwa na kudhulumiwa sana mali zetu
ambazo tumezirithi kutoka kwa babu zetu lakini awamu ya Tano ikiongozwa
na Rais Magufuli imeamua kwa dhati kabisa kutilia mkazo Vita dhidi ya
Rushwa, Uhujumu uchumi, Udhalimu wa kila namna, sambamba na wizi na
ufisadi kwa maslahi mapana ya Taifa la Tanzania na Watanzania wote"
Alisema Polepole
Akizungumzia Mauaji yanayotokea katika
maeneo mbalimbali nchini hususani Mkoani Pwani katika Wilaya ya Kibiti,
Rufiji na Mkuranga alisema kuwa kipindi hiki kigumu kwa kuwapoteza ndugu
zetu vyama vya siasa vilipaswa kushikamana kwa pamoja pasina kujali
itikadi zao badala yake vimeanza kutumia misiba hiyo kwa maslahi ya
kiuongozi kuliko maslahi ya Taifa.
Polepole
alisema kuwa vyombo vyote vya serikali vinavyoshughulikia ulinzi
vinapaswa kutumia Rasilimali zao, Weledi na Utendaji wao, na kuweka
umaalumu katika kuyakabili matukio ya mauaji na kuyakomesha kabisa.
"Hakuna
dini yoyote Duniani inayoamini katika kutoa uhai wa mtu ambapo pia kuua
mtu ni kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivyo
Tunataka amani ya wananchi wetu inarudi"
"Tunatambua
kuwa wananchi wetu wanapita katika wakati mgumu kutokana na kukatishwa
kinyama maisha ya Wananchi wenzao, Viongozi, Askari, Watendaji wa
serikali, Wanachama wa CCM si kwa sababu ya mapenzi ya Mungu Bali kwa
sababu yamekatishwa katika namna inayokiuka ubinadamu kwa kuuawa
kikatili na watu wasio na Utu, Hisia na Imani ya Dini" Alisema Polepole
Polepole
ametilia msisitizo wananchi kutoa taarifa kwa jeshi la Polisi kuhusu
watu wanaofanya mauaji hayo kwani ushirikiano huo utasaidia kufichua
uovu wa wadhalimu wanaokatisha maisha ya watanzania.
No comments:
Post a Comment