Pages

March 25, 2017

TANZANIA YAHUDHURIA MKUTANO WA 18 WA MWAKA WA BENKI YA DUNIA WA MASUALA YA ARDHI NA UMASIKINI


Na Mboza Lwandiko
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Imeshiriki Mkutano wa mwaka wa 18 wa Benki ya Dunia unaohusu masuala ya Ardhi na Umaskini, Machi 20 – 24, 2017 – Washington DC – Marekani.
Mkutano huo unaobeba ujumbe; “Utawala bora wa Ardhi”, umejumuisha zaidi ya wajumbe 1,200 kutoka nchi wanachama, zilizohusisha Serikali, taaluma, jamii na Sekta binafsi mbalimbali.
Pamoja na mambo mengine; Mkutano huo umejikita zaidi katika Maboresho mbalimbali yanayoendelea kufanyika katika Sekta ya Ardhi Duniani, ikiwa ni pamoja na kuzingatia nafasi ya takwimu na shuhuda zinazoashiria maboresho katika Sera za Ardhi, na kuainisha Mikakati ya Maendeleo katika kuboresha zaidi Sekta ya Ardhi.
Aidha, Mada ambayo imewasilishwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imewasilishwa na Katibu Mkuu wa Wizara; Dkt. Yamungu Kayandabila, ambayo ilibeba ujumbe -  “Ardhi; Ufunguo wa Utawala Bora na Maendeleo ya Uchumi kwa Tanzania”. Alieleza kuwa utawala wa Ardhi Tanzania unazingatia; Sheria, Uwazi, Uwajibikaji na Ushirikishwaji wa Wananchi. Pamoja na mengine Dkt. Kayandabila alieleza jitihada mbalimbali ambazo zimekuwa zikifanyika kuboresha sekta ya ardhi nchini na juhudi ambazo zinaendelea kuboresha utawala bora wa Ardhi nchini.
Baadhi ya maboresho aliyoyataja ni pamoja na; Kuboresha Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995, Upimaji wa viwanja katika maeneo ya vijijini; mfano; Ulanga, Kilombero na Mvomero (Morogoro) kwa mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi (LTSP) na uendeleaji wa kujenga mfumo unganishi wa taarifa za ardhi ujulikanao kama Integrated Land Management Information System (ILMIS).
Wajumbe wengine waliohudhuria Mkutano huo ni pamoja na; Kaimu Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Mipango na Matumizi ya Ardhi (NLUPC), Dkt. Stephen Nindi, Kamishna msaidizi wa Ardhi, kanda ya Dar es Salaam; Mathew Nhone; Mkurugenzi msaidizi wa Idara ya Mipango Miji na Vijiji; Immaculate Senje, Kaimu Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya ; Amina Rashidi, wote wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni; Aaron Kagurumjuli na Afisa Ardhi wa Manispaa ya Kinondoni; Rehema Mwinuka.
Aidha, ujumbe kutoka Tanzania ulipata fursa ya kuonana na ujumbe wa Finland  akiwemo aliyekuwa balozi wa zamani wa Finland nchini Tanzania; Sinikka Antila, Mkurugenzi wa upimaji na ramani wa Finland na wawakilishi wa makampuni mbalimbali ya vifaa vya upimaji na ramani na softwares wa Master plans. Wajumbe hao walifikia makubaliano ya ujumbe wa Finland kufika Tanzania kwa mazungumzo zaidi.
Baadhi ya mada zilizowasilishwa kwenye Mkutano huo ni; Jinsi utawala wa ardhi, unavyoongeza kodi ya Mapato na kuwezesha upatikanaji wa Ajira, Worldbank, Uganda; Matumizi ya takwimu za ardhi kwa utawala wa Serikali za Mitaa. Location International; UK ; Kuboresha Utawala wa Ardhi kwa Utawala Bora; Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Mijji, Uganda; Kuwezeshwa kwa Wananchi na Matumizi ya Ardhi, maendeleo ya ardhi na utawala wa taasisi, Kenya; na Uzoefu wa Sekta Binafsi katika sekta ya Ardhi- USAID, Marekani.  
Na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...