Magenge hayo ya wahalifu hutenda uhalifu wakiwa katika makundi ya watu watano hadi 20 wakiwa na silaha mbalimbali zikiwamo za moto.
Juzi kundi la watu 20 wanaodhaniwa kuwa majambazi lilivamia nyumba ya mapadri wa Kanisa Katoliki na kupora fedha na mali nyingine.
Majambazi hao walivamia Parokia ya Kilungule, wilayani Temeke na kupora fedha taslimu na mali zenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni nne. PAROKO MSAIDIZI ASIMULIA
Akizungumza na NIPASHE eneo la tukio, Paroko Msaidizi wa parokia hiyo, Padri Pascal Libongi, alisema majira ya saa 8:00 usiku wa kuamkia jana, waliamshwa na walinzi wa nyumba hiyo kuwa kuna kundi la vijana wenye silaha wanavamia ndipo walipotoka na kujificha.
“Tuliamshwa na mlinzi wa ndani kuwa tunavamiwa ndipo tukajificha, nilijificha bafuni na Paroko alijificha kwingine, walifika wakapanda kwenye geti na kufungua mlango kwa ndani na kuingia kisha wakavunja mlango mkuu kwa baruti,” alisema.
Alisema watu hao waliingia ndani ya geti huku wakipiga kelele wakisema wanataka kuua na kwamba walitumia muda wa dakika 10 hadi 15 kuvunja mlango kwa kutumia silaha walizokuwa nazo na walifyatua baruti.
“Baada ya kuingia ndani walizima umeme kwenye main switch, wakabishana kwa muda, waliambizana twende kwenye chumba cha bosi, waliingia wakachukua walichoweza na walitoka sebuleni na kuchukua seti ya TV nchi 24 na kuondoka,” alisema Padri Libongi.
Padri Libongi alisema ndani ya chumba cha Paroko walichukua simu tatu na fedha taslimu Sh. milioni 3.2 na TV na baadaye waliondoka huku wakipiga kelele.
Alisema baada ya kuridhika kuwa wameondoka, yeye (Libongi) alitoka mafichoni na kuangalia uharibifu uliofanyika na kukuta walivunja mlango na kuuharibu kabisa, huku wakitaka kutoa geti la chuma lililokuwapo.
Alieleza kuwa tukio hilo lilichukua dakika 22 na kwamba polisi walifika eneo hilo baada ya nusu saa na kwamba mmoja wa walinzi alijeruhiwa na waya wakati akiruka ukuta kujiokoa.
Aidha, alisema ongezeko la matukio ya ujambazi linatokana na ukosefu wa ajira na vijana kutopenda kujishughulisha, wazazi kutelekeza familia, watoto kulelewa na mzazi mmoja na matumizi ya dawa za kulevya.
MLINZI AZUNGUMZA
Mmoja wa walinzi wa nyumba hiyo, Ismail Karama, alisema baada ya kusikia vishindo aliangalia nje kupitia matundu ya ukuta na kuona kundi la watu wapatao 20 wakiwa wameziba sura zao, wameshika mapanga, marungu na bunduki, ndipo alipomtaarifu mlinzi mwenzake na kuwaamsha mapadri.
Alisema walipofika getini walimtaka afungue geti, lakini alikataa ndipo walioopanda na kuanza kurukia ndani mmoja baada ya mwingine.
“Huku nikipiga filimbi kuomba msaada nilitumia ngazi iliyopo kupanda ukutani na kuruka nje, nilisikia milio mitatu ya risasi na kelele nyingi za kuvunja mlango na baada ya muda palikuwa kimya...nilitoka mafichoni na kwenda ndani tulikuta wameiba,” alisema.
KAULI YA RPC
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Andrew Satta, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa lilitokea juzi saa 8:00 usiku na kwamba kundi la vijana hao ambao ni vibaka walikuwa na silaha za jadi na baruti.
Alisema hakuna risasi iliyopigwa eneo la tukio bali baruti na kwamba baada ya kuingia ndani walikwenda moja kwa moja kwenye droo yenye fedha hizo na kwamba licha ya chumba hicho kuwa na vitu vingine vya thamani, walikwenda kuchukua fedha moja kwa moja kiasi cha Sh. milioni tatu na TV yenye thamani ya Sh. milioni moja.
Kamanda huyo alisema wanaendelea na upelelezi wa tukio hilo na kwamba baada ya tukio walikimbilia kwenye korongo la Buza.
Alisema kwa sasa mkoani humo yamezuka makundi ya vijana yanayojihusisha na uhalifu na kwamba kwa kushirikiana na polisi jamii wanakabiliana nayo.
Kwa mujibu wa kamanda huyo, baada ya kuwadhibiti eneo la Buza wamehamia maeneo ya Zansa, Kilungule, Chanika, Mbande na kwingine.
Kamanda Satta alisema ongezeko hilo linatokana na vijana waliokuwa wamekimbilia Afrika Kusini kurejea nchini, baada ya vurugu za raia wa nchi hiyo dhidi ya raia wa kigeni na kwamba ushiriki wa jamii ndiyo utawapunguza na kumaliza uhalifu.
Aliiomba jamii katika eneo la Mbagala na maeneo mengine kutoa ushirikiano kwa polisi ili kuwakamata wahalifu hao ambao wamekuwa wakishika mabegi kama wasafiri wakati lengo lao ni kupora watu na nyumba na kuwa kwa siku za hivi karibuni walipora katika baa na maduka Dar es Salaam.
MATUKIO YA HIVI KARIBUNI
Matukio ya ujambazi wa kupora kwenye makazi ya watu, maduka na sehemu nyingine za biashara yameshika kasi katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam siku za hivi karibuni.
Magenge ya wahalifu hao hutenda uhalifu wakiwa katika makundi ya watu watano hadi 20 wakiwa na silaha mbalimbali zikiwamo za moto.
Kwa takribani wiki moja, wakazi kadhaa wa jiji hilo wamekumbwa na matukio ya kuporwa.
Mwandishi wa NIPASHE, Mashaka Mgeta, alivamiwa na majambazi usiku wa kuamkia Mei 3, mwaka huu, nyumbani kwake Kimara-Golani na kupora vifaa vya kazi ikiwamo kompyuta mpakato, tape recorder, flash na kamera.
Msanii wa Bongo Flava, Ally Kiba, alivamiwa nyumbani kwake eneo la Mbezi na kundi la majambazi wapatao 20 wakiwa wameziba sura (kininja) na kuiba vitu mbalimbali kama fedha na mali nyingine ambazo thamani yake haijajulikana
Mei 3, mwaka huu, majira ya saa 2 usiku, kundi la watu wanaosadikiwa ni majambazi walivamia duka la kutoa huduma ya fedha kwa mtandao wa simu, kuuza umeme na bidhaa mbalimbali eneo la Ikweta, Nzasa Mbagala.
Aidha, hivi karibuni baa ya Manchester, Temeke ilivamiwa na kundi la watu wanaosadikiwa ni majambazi na kupora fedha za mauzo ya siku hiyo. CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment