Habari zilizopatikana jana kutoka
Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini kupitia kwa Msemaji wake, Habib Awesi
zilisema Waziri Mgimwa amefariki dunia mchana... “Ni kweli amefariki leo mchana
tumepeleka taarifa Ikulu, Dar es Salaam.”
Baadaye jana, Katibu Mkuu Kiongozi,
Balozi Ombeni Sefue alithibitisha kupokea taarifa za kifo hicho na kusema
Waziri Mgimwa alifariki dunia saa 5:20 kwa saa za Afrika Kusini (saa 6:20).
“Kinachofanyika kwa sasa ni maandalizi
ya kuurudisha nyumbani mwili wa marehemu na hilo linafanywa na Serikali kwa
kushirikiana na familia yake. Taarifa zaidi zitatolewa baadaye kadiri
zitakavyopatikana,” alisema Balozi Sefue.
Akizungumzia msiba huo, Naibu Spika wa
Bunge, Job Ndugai alisema: “Bunge limepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha
Dk Mgimwa, alikuwa ni mtu mwaminifu katika kazi zake na alishirikiana
kikamilifu na wabunge katika kutekeleza kazi za Serikali. Taifa limepoteza mtu
makini aliyefanya kazi katika sekta ambayo aliisomea, jambo ambalo lilimfanya
awe na ufahamu mzuri wa mambo katika wizara (Fedha),” alisema Ndugai.
Kikwete
atuma rambirambi
Jana jioni Rais Jakaya Kikwete alitoa
taarifa akielezea kushtushwa na kifo cha Waziri Mgimwa.
“Nimepokea kwa mshtuko na huzuni kubwa
taarifa za kifo cha Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa,” ilisema taarifa yake
kupitia Kurugenzi ya Mawasiliano, Ikulu.
Alisema taifa limempoteza Waziri Mgimwa
katika kipindi lilipokuwa linamhitaji zaidi kutokana na mchango wake mkubwa
ambao amekuwa akiutoa kupitia nafasi zake za Waziri wa Serikali na mwakilishi
wa wananchi wa Jimbo la Kalenga.
Katika salamu zake kupitia kwa Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda na kwa familia ya marehemu Mgimwa, Rais Kikwete alisema:
“Sina maneno ya kutosha kuelezea mshtuko na huzuni yangu kubwa kufuatia taarifa
za kifo cha Mgimwa.
“Binafsi nilimtembelea mara mbili
hospitali alikokuwa amelazwa na mara ya mwisho hali yake ilikuwa imeimarika.
Tulizungumza kwa kiasi cha dakika 10 hivi akanielezea nia yake na tamaa yake ya
kurejea nyumbani kwa sababu hali yake ilikuwa nzuri.
“Sote tunajua mchango wake katika
Serikali. Sote tulitamani kuendelea kuwa naye, lakini haya ni mapenzi ya
Mungu... Natoa pole nyingi na rambirambi zangu za dhati kwa wana familia wote
kwa kuondokewa na mhimili wao. Naungana nanyi katika kuomboleza msiba huo
mkubwa. Napenda mjue kuwa msiba huu ni msiba wangu pia. Machungu yenu ni
majonzi yangu,” alisema Rais Kikwete.
No comments:
Post a Comment