Mama mzazi wa Mkuu wa Polisi nchini (IGP),
Ernest Mangu, Mwanaidi Msengi, anayeishi Kijiji cha Kihanuda, Ilongero,
Wilaya ya Singida akipasua kuni kwa ajili ya kupikia nyumbani kwake, jana
mchana. Picha na Gasper Andrew
·
Asimulia jinsi alivyobeba vyungu kutafuta fedha za kusoma hadi
akapata upara.
Singida. Mama Mzazi wa Mkuu
wa Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu, Mwanaidi Msengi, amemsihi mwanawe
kufanya kazi kwa bidii asimwangushe Rais Jakaya Kikwete ili asije kujutia kumpa
nafasi hiyo.
Mwanaidi alisema licha
ya furaha kubwa aliyonayo, anamuasa mtoto wake kuchapa kazi kwa bidii
kama njia mojawapo ya shukurani kwa Rais Kikwete kwa kumteua akiwa
mwenyeji wa kwanza kutoka Mkoa wa Singida kushika wadhifa huo nyeti.
“Hii ni heshima kubwa
sana kwangu binafsi, ndugu zake, wakazi wa Kijiji cha Kihunadi na Mkoa wa
Singida, kwa hiyo lengo langu ni kumwombea mtoto wangu Mangu asimwangushe
Rais... Eee Baba (Mungu) msaidie mwanangu atimize wajibu wake ipasavyo ili Rais
Kikwete siku moja aseme hakukosea kumpa Mangu ukuu wa polisi,” alisema
Mwanaidi.
Juzi ndugu, jamaa na
marafiki walifanya hafla ndogo iliyoambatana na vifijo, nderemo na bashasha na
wakazi wa Kijiji cha Kihunadi, Tarafa ya Ilongero, mkoani Singida, alikozaliwa
IGP huyo huku wakidai sasa kijiji chao kitajulikana haraka ndani na nje ya
Tanzania.
Walisema licha ya
kujulikana, changamoto mbalimbali zinazokikabili kijiji hicho zitapatiwa
ufumbuzi wa kudumu mapema iwezekanavyo.
Mwanaidi alisema Mangu
alianza kumwonyesha mafanikio tangu Shule ya Msingi Kinyagigi, kwani alikuwa na
bidii ya kujisomea mara kwa mara alishika nafasi ya kwanza au ya pili.
Kwa mujibu wa
Mwanaidi, IGP Mangu ni mtoto wa pili kati ya saba aliowazaa.
“Mangu ni wa
pili kati ya watoto wangu saba baada ya kuolewa na baba yao, Jumbe Omari Mangu
aliyefariki Aprili 27, 1988. Jina la Jumbe linatokana na kupewa kazi ya
ujumbe wa wakoloni wakati wa ujana wake,” alisema.
Wenyeji wa kijiji
hicho, walisema wamekuwa wakiamini Mangu atafika mbali kwa kushika nafasi
za juu za uongozi, kutokana na uadilifu, uchapaji kazi, ukaribu wake na
wananchi, uaminifu na uwazi.
Mwanaidi alisema Mangu
alipofaulu kwenda sekondari alilazimika kuomba ng’ombe kwa mke mweza, ili
akamuuze apate fedha za kugharimia masomo ya mtoto wake.
“Mke mwenzangu alimtoa
ng’ombe wake, lakini Mangu alipomuuza kwenye mnada pale Singida mjini,
aliibiwa fedha zote na alirudi nyumbani akilia sana,” alisema.
Alisema baada ya hapo alimwambia mtoto wake
kwamba, ataanza kutengeneza vyungu kwa kutumia udongo wa mfinyanzi ili kupata
fedha za kugharimia masomo yake.
“Nashukuru Mangu alinielewa vizuri kwa sababu
alishiriki kubeba kichwani vyungu hivyo wakati wa kuviuza hadi kichwa chake
kilikaribia kuwa kipara. Nilibuni chanzo kingine cha mapato ambacho
kilikuwa ni kukoroga na kuuza pombe za kienyeji,”
Inadaiwa baba yake,
IGP Mangu alioa wanawake sita kwa nyakati tofauti, lengo likiwa ni kupata
mtoto wa kiume. Wengi wa wake zake walikuwa wakizaa watoto wa kike
Chanzo.Mwananchi
No comments:
Post a Comment