Mbunge
wa Monduli (CCM), Edward Lowassa akiwasalimia wananchi waliohudhuria sherehe za
Mwaka Mpya nyumbani kwake jana. Kushoto ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Godluck ole Medeye na kulia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa
Arusha, Onesmo ole Nangole. Picha na Mussa Juma.
KWA UFUPI
·
Akizungumza katika ibada ya shukrani na
kuupokea mwaka mpya, katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania
(KKKT),Usharika ya Monduli Mjini, Lowassa bila ya kutaja safari hiyo ni ipi,
aliwashukuru watu wote kutoka maeneo mbalimbali nchini, ambao walimsindikiza
katika ibada hiyo.
Monduli. Waziri Mkuu wa
zamani, Edward Lowassa ametangaza kuanza rasmi kwa safari aliyoiita ya
matumaini ya ndoto zake, ambayo amesema itatimiza ndoto za Watanzania za kupata
elimu bure, maji safi na maendeleo ya uhakika.
Akizungumza katika ibada ya shukrani na kuupokea mwaka mpya,
katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT),Usharika ya Monduli
Mjini, Lowassa bila ya kutaja safari hiyo ni ipi, aliwashukuru watu wote kutoka
maeneo mbalimbali nchini, ambao walimsindikiza katika ibada hiyo.
Lowassa alisema anaamini watu hao waliofika, wana uhakika wa
ushindi katika safari hiyo kwa kumtegemea Mungu.
“Nimefarijika sana leo kuwaona hapa marafiki zangu wengi.
Ninapowatazama hadi machozi yananitoka na kwa uwezo wa Mungu tutashinda kwani
nyote mnajua nia na ndoto yangu,’’ alisema Lowassa na kupokelewa na sauti za
shangwe kanisani.
Licha ya kutoweka bayana, Lowassa amekuwa akitajwa kuwa ni mmoja
wa wanasiasa wanaowania kumrithi Rais Jakaya Kikwete baada ya kumaliza kipindi
chake cha uongozi mwakani.
Azungumzia Katiba Mpya.
Akizungumzia Katiba Mpya, ambayo mchakato wake sasa unaelekea
katika Bunge Maalumu, licha ya kuipongeza Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya
Mwenyekiti wake, Jaji Joseph Warioba alisema ana wasiwasi juu ya muundo wa
Serikali Tatu.
“Nina wasiwasi na huu muundo, ni vyema viongozi wa dini,
kuliombea taifa tupate Katiba bora kwani maoni ya watu asilimia 40 ambao
hawakutaka muundo wa Serikali Tatu lazima yatazamwe,” alisema Lowassa.
Ibada katika Kanisa hilo, ambayo iliendana na harambee ya
kuchangia hosteli na zaidi ya Sh89 milioni kupatikana, iliongozwa na Kaimu
Askofu wa KKKT, Usharika wa Kaskazini Kati, Solomon Masango.
Katika mahubiri yake, Kaimu Askofu Masango alimtakia kila la
heri Lowassa katika safari yake hiyo akisema anamtambua kuwa ni kiongozi bora.
Hafla ya nyumbani
Akizungumza
katika hafla aliyoandaa baadaye nyumbani kwake, Lowassa alirudia kauli yake ya
kuanza safari.
Waliohudhuria halfa hiyo ni pamoja na
wabunge wengi wakiwa wa CCM, wenyeviti wa CCM, wakiongozwa na Mwenyekiti wa
Wenyeviti wa CCM, Mgana Msindai kutoka Mkoa wa Singida, Mwenyekiti wa Wenyeviti
wa UVCCM, Manka Dilu kutoka Mkoa wa Mara na Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Wanawake
wa CCM, Diana Chilolo pia kutoka Mkoa wa Singida, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa
Manyara, Lucas ole Mukusi ambaye ndiye katibu wa wenyeviti wote wa CCM.
Wengine waliohudhuria ni wajumbe wa
Halmashauri Kuu ya CCM (Nec), mikoa mbalimbali ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa
CCM na viongozi wa dini mbalimbali. Pia alikuwapo aliyekuwa mgombea urais wa
Kenya katika uchaguzi uliopita, Profesa James ole Kiapi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Lowassa
alisema ndoto ya elimu bure, ajira kwa vijana, kuondoa umaskini zitafanikiwa
baada ya kuanza safari yake hiyo hapo jana.
Alisema wakati ukifika wa kutangaza
rasmi nia hiyo, ataeleza mengi na akawataka wanaomuunga mkono wasiwe na
shaka... “WanaCCM msiwe na shaka, tutavuka kwa nguvu zetu... wingi wenu huu
unanipa faraja kuwa katika safari yetu na kwa kumtegemea Mungu tutashinda.”
Lowassa aliwataka waungane na kaulimbiu
yake, ‘Tulifurahi pamoja, tulihuzunika pamoja na tutashinda pamoja’ na baada ya
kusema maneno hayo, alipokewa kwa sauti za CCM... CCM... CCM.
Waalikwa
wazungumza
Akizungumza katika hafla hiyo, Msindai
ambaye aliwaongoza wenzake Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Hamis Mgeja na
Onesmo Nangole wa Mkoa wa Arusha alisema wanamuunga mkono, Lowassa katika
safari yake hiyo.
Alisema anamfahamu Lowassa kwa muda
mrefu na kumwelezea kwamba ni kiongozi bora mwenye uamuzi na kwamba haoni
sababu ya kutokumuunga mkono.
Mgeja alisema anawashangaa watu wachache
ambao wameanza tabia ya kulazimisha watu kuwachagulia marafiki na kuwachafua
wengine.
Alisema hakuna ambaye hafahamu kuwa
Lowassa ndiye tumaini la Watanzania akisema jina lake linatajwa kila kona kwa
kuwa ana uwezo na sababu za kuwa kiongozi wa Taifa.
Mgeja alionya kuwa kuna kundi la watu
linalodhani kuwa CCM ni mali ya viongozi kitu ambacho alisema si sahihi, bali
ni mali ya wanachama ambao alisema ndiyo wenye uamuzi.
Nangole alisema Lowassa ni kiongozi
msikivu na makini ambaye ni tegemeo la Watanzania katika kuwaunganisha kuwa
kitu kimoja.
Wakizungumza katika hafla hiyo, viongozi
hao wa CCM, walisema wanamuunga mkono Lowassa kutokana na uwezo mkubwa alionao.
Manko kwa upande wake alisema UVCCM ina
imani kubwa na Lowassa kwani ni mmoja wa makada wa CCM wenye historia ndefu
katika chama hicho.
Kwa upande wake, Mbunge wa Chemba Kondoa
(CCM), Juma Nkamia alisema Lowassa sasa ni sawa na Simba na kusema wanaomchukia
walie tu kwani ni kiongozi bora.
Mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM, Hussein
Bashe aliwataka wananchi wa Monduli kutunza heshima ya Lowassa na kwamba kazi
nyingine watafanya wao.
Alisema safari ya Lowassa ndiyo, imeanza
inawezekana na kwamba alipoanguka mwaka 2008, ilikuwa ni mipango ya Mungu
kuwezesha safari hiyo. “Lowassa ana sifa zote za uongozi... tunachokiomba kwenu
ni ushirikiano tu.”
Chanzo.Mwananchi
Chanzo.Mwananchi
No comments:
Post a Comment