JAMHURI YAFUNGA USHAHIDI KESI YA UHAINI YA TUNDU LISSU, MASHAHIDI 17 WAKAMILISHA UTOAJI USHAHIDI


Na Janeth Raphael - MichuziTv

Upande wa Jamhuri umefunga ushahidi wake baada ya kuwasilisha ushahidi wa mashahidi 17 katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu.

Hatua hiyo imefikiwa leo Jumatatu, Agosti 17, 2026, katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo, Dar es Salaam, wakati kesi hiyo ikiendelea kusikilizwa mbele ya jopo la majaji watatu.

Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga, ameieleza Mahakama kuwa baada ya upande wa Jamhuri kupitia kwa kina ushahidi uliotolewa na mashahidi wake pamoja na hoja mbalimbali zilizowasilishwa wakati wa usikilizwaji wa kesi, umefikia uamuzi kuwa ushahidi uliopo unatosheleza.

Kwa mujibu wa Katuga, uchambuzi wa ushahidi uliowasilishwa mahakamani umeifanya Jamhuri kuona hakuna ulazima wa kuongeza mashahidi wengine, hivyo upande huo umefunga rasmi ushahidi wake.

“Baada ya kupitia ushahidi uliowasilishwa hapa mahakamani na kuangalia ushahidi wa mashahidi waliobakia, tumechambua na kuangalia hoja zilizowasilishwa mahakamani hapa. Hata hivyo, upande wa Jamhuri tunaona ushahidi ambao tumeutoa ni ushahidi toshelezi zaidi kuleta mashahidi wengine,” amesema Katuga.

Uamuzi huo unaweka kesi hiyo katika hatua muhimu, baada ya upande wa mashtaka kukamilisha uwasilishaji wa ushahidi wake kupitia mashahidi 17.

Kesi hiyo inasikilizwa na jopo la majaji watatu likiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, akisaidiwa na Jaji James Karayemaha na Jaji Ferdinand Kiwonde.

Kufungwa kwa ushahidi wa Jamhuri kunafungua hatua nyingine ya kisheria katika mwenendo wa kesi hiyo, huku taratibu za mahakama zikiendelea kuamua hatua zinazofuata.

Post a Comment

أحدث أقدم