
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
MAMLAKA ya Serikali Mtandao (e-GA) inaendelea kushirikiana na Wizara ya Kilimo katika kuimarisha matumizi ya mifumo ya kidijitali inayolenga kurahisisha utoaji wa huduma, kuongeza uwazi na kuboresha usimamizi wa shughuli za kilimo nchini.
Akizungumza jana katika Maonesho ya Wakulima ya Kitaifa yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Samwel Malecela jijini Dodoma, Meneja wa Mawasiliano wa e-GA, Subira Kaswaga, alisema mamlaka hiyo imeshiriki katika ujenzi wa mifumo mbalimbali inayotumika katika sekta ya kilimo.
Alisema mifumo hiyo inaiwezesha Wizara ya Kilimo kupata taarifa za wakulima nchini, kufuatilia shughuli za taasisi zilizo chini ya wizara hiyo pamoja na kutoa taarifa muhimu za kilimo kwa wadau.
Kaswaga alisema e-GA pia imeshirikiana na Tume ya Maendeleo ya Ushirika kutengeneza Mfumo wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (MUVU), unaolenga kuongeza uwazi na uwajibikaji katika uendeshaji wa vyama vya ushirika.
Alisema mfumo huo pia unawawezesha wakulima kufuatilia mauzo ya mazao yao, bei pamoja na malipo wanayostahili kupata.
“Hadi sasa, zaidi ya vyama 6,000 vya ushirika vinatumia mfumo huo, jambo ambalo limesaidia kuboresha usimamizi wa mapato na kuongeza uwajibikaji katika sekta ya ushirika,” alisema.
Alieleza kuwa e-GA ina jukumu la kuandaa na kusimamia mifumo mbalimbali ya TEHAMA inayotumika serikalini kwa lengo la kuboresha utendaji kazi wa taasisi za umma na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.
Aidha, alisema e-GA imeshirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kuanzisha Fertilizer Information System (FIS), mfumo unaosaidia kusimamia wazalishaji na waingizaji wa mbolea, kufuatilia mwenendo wa soko na kuhakikisha wauzaji wanazingatia bei elekezi zinazotolewa na Serikali.
Kwa mujibu wa Kaswaga, mfumo huo unaisaidia Serikali kudhibiti soko la mbolea na kuhakikisha wakulima wanapata pembejeo hizo kwa bei stahiki, hatua inayolenga kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao.
Mbali na mifumo hiyo, alisema taasisi za sekta ya kilimo zinaendelea kutumia mifumo mingine ya Serikali, ikiwemo Government Email System na Mfumo wa Ofisi Mtandao, ambayo imechangia kuboresha mawasiliano na utendaji kazi ndani ya taasisi za umma.
Mamlaka hiyo imewataka wananchi kutembelea banda la e-GA katika maonesho yanayoendelea jijini Dodoma ili kupata elimu zaidi kuhusu mifumo ya kidijitali inayotumika kuboresha utoaji wa huduma za Serikali na mchango wake katika maendeleo ya sekta ya kilimo.

إرسال تعليق