POLISI NA MADEREVA WA BAJAJI WASHIRIKI KUTOA FARAJA KWA WENYE MAHITAJI WILAYANI ILEJE.


Kikosi cha usalama barabarani Wilaya ya Ileje kimeungana na wasafirishaji wa abiria kwa kutumia bajaji kuwafariji na kuwasaidia wagonjwa waliolazwa katika Wodi ya Wazazi ya Hospitali ya Wilaya ya Ileje pamoja na wanafunzi wa Shule ya Msingi Mpakani waliofiwa na wazazi wao kwa kuwapatia mahitaji mbalimbali, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na jamii kupitia matendo ya huruma kwa jamii. (Bajaji Day)

Tukio hilo limefanyika Julai 22, 2026 na kuongozwa na Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Wilaya ya Ileje, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Krisbert Kapondo, likihusisha viongozi na wanachama wa umoja wa wasafirishaji wa abiria kwa kutumia bajaji. 

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, ASP Kapondo aliwapongeza wasafirishaji hao kwa moyo wao wa kujitolea na kuwahimiza kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi katika shughuli mbalimbali za maendeleo ya jamii, akieleza kuwa vitendo vya huruma na upendo vinaimarisha mshikamano, amani na ustawi wa wananchi.

Kwa upande wao, viongozi wa wasafirishaji wa bajaji wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bajaji Wilaya ya Ileje, Bw. Domenick Kamwela, pamoja na Diwani wa Kata ya Isongole, Mh Obeid Mwambene walieleza kuwa wataendelea kushiriki katika shughuli za kijamii zinazolenga kuwasaidia wenye uhitaji, huku wakitoa wito kwa wadau wengine kuendeleza utamaduni wa kusaidiana ili kujenga jamii yenye mshikamano, upendo na uwajibikaji. 









Post a Comment

Previous Post Next Post