EAC INAIMARISHA USALAMA WA AFYA KWA KUZINDUA TAASISI YA UTAFITI WA VIRUSI YA UGANDA KAMA KITUO CHA KIKANDA CHA UBORA KATIKA ELIMU YA VIRUSI (VIROLOGY)


Uwezo wa kanda wa kuzuia, kugundua na kukabiliana na milipuko ya magonjwa ya kuambukiza umeimarishwa kwa kiasi kikubwa kufuatia uzinduzi rasmi na uendeshaji wa Taasisi ya Uhafiti wa Virusi ya Uganda (UVRI) kama Kituo cha Kikanda cha Ubora cha Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) katika Elimu ya Virusi (Virology) huko Entebbe, Uganda.
Kituo hiki kitatumika kama kitovu cha kikanda cha utafiti wa hali ya juu wa virusi, mafunzo maalum ya maabara, ufuatiliaji wa magonjwa, utambuzi (diagnostics) na ushiriki wa maarifa, na hivyo kuongeza uwezo wa Nchi Wanachama wa EAC kujiandaa na kukabiliana na matishio ya afya ya jamii, ikiwa ni pamoja na Ebola, Marburg na magonjwa mengine ya virusi yanayoibuka na yanayojirudia.
Uzinduzi huo ulifanywa rasmi na Waziri Mkuu wa Uganda na Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni, Mhe. Robinah Nabbanja, akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Uganda, Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mhe. Nabbanja alisema uzinduzi huo ni wito wa kuwajibika kwa kanda kufanya mengi zaidi katika kuimarisha usalama wa afya. Alibainisha kuwa ulimwengu unabadilika kwa kasi sambamba na mabadiliko ya mahitaji na sera za afya.
“Kupitia safari hii, tumeona na kujifunza kwamba taifa linalochunguza vimelea vyake lenyewe ni taifa linalojitegemea. Tunahadi kuongeza ufadhili wa utafiti,” alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la EAC, Mhe. Rebecca Alitwala Kadaga, ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza wa Uganda na Waziri wa Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, alisifu kuanzishwa kwa Kituo hicho, akibainisha kuwa kunakuja wakati ambapo matishio ya magonjwa ya kuambukiza yanaendelea kutoa changamoto kwa kanda na ulimwengu.
“Mlipuko wa COVID-19 ulionyesha kuwa magonjwa hayaheshimu mipaka, na mlipuko unaoibuka katika Nchi moja Wanachama unaweza kuwa jambo la kusononekesha kanda nzima kwa haraka,” alibainisha.
Wakati Nchi Wanachama wa EAC zikiwa zimeendelea kuimarisha mifumo yao ya maabara, tofauti bado zipo katika uwezo wa kiufundi, utaalamu na rasilimali. Uendeshaji wa Vitovu vya Kikanda vya Ubora unatoa mfumo wa Nchi Wanachama kushiriki maarifa maalum, kuimarisha ushirikiano wa kisayansi na kuboresha ujiandaaji na ukabilianaji wa pamoja.
Akimwakilisha Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu wa EAC anayesimamia Miundombinu, Sekta za Uzalishaji, Jamii na Siasa, Mhe. Ariik Aguer Malueth, alibainisha kuwa Kituo cha Kikanda cha Ubora cha EAC ni taasisi maalum inayotambuliwa na Jumuiya kutoa utaalamu wa hali ya juu, utafiti, mafunzo, uvumbuzi na usaidizi wa kiufundi katika eneo lenye umuhimu wa kikanda.
“Vitovu hivi vinahakikisha kwamba maarifa ya kisayansi na uwezo maalum uliotengenezwa katika Nchi moja Wanachama unakuwa rasilimali ya pamoja ya kikanda inayofaidisha Waafrika Mashariki wote,” alibainisha.
Mhe. Ariik aliongeza kuwa Kituo cha Kikanda cha Ubora cha EAC katika Elimu ya Virusi (Virology) pale UVRI ni miongoni mwa Vitovu saba vya Kikanda vya Ubora vya Utambuzi wa Matibabu vilivyoainishwa chini ya Mfumo wa Kipaumbele wa Uwekezaji wa Afya wa EAC 2018–2028, ulioidhinishwa na Mkutano wa 19 wa Wakuu wa Nchi wa EAC.
“Uongozi wa Uganda katika elimu ya virusi unaonyesha utaalamu unaotambulika kimataifa wa UVRI na mchango wake wa miongo kadhaa katika utafiti wa virusi, ufuatiliaji wa magonjwa na ukabilianaji wa milipuko,” alisema.
Hafla hiyo ilifanyika sambamba na maadhimisho ya miaka 90 ya UVRI chini ya kauli mbiu, “Kusherehekea Miaka 90 ya Ugunduzi na Athari Duniani.”
Akizungumza katika uzinduzi huo, Prof. Pontiano Kaleebu, Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Virusi ya Uganda, alishukuru ushirikiano na EAC na washirika, akithibitisha kujitolea kwa UVRI katika kuendeleza usalama wa afya wa kikanda.
“Kama kitovu cha kikanda, UVRI itasaidia utafiti wa hali ya juu wa virusi, mafunzo maalum ya maabara, utambuzi, ufuatiliaji na ushiriki wa maarifa katika kanda yote ya EAC,” alisema.
Kituo hiki kitaimarisha uwezo wa Nchi Wanachama kugundua, kuthibitisha na kukabiliana na magonjwa ya virusi kupitia mitandao iliyoimarishwa ya maabara na ushirikiano wa kisayansi. UVRI tayari inacheza nafasi muhimu ya kikanda kwa kusaidia uthibitisho wa sampuli zinazotumwa kutoka Nchi Wanachama kabla ya milipuko ya magonjwa kutangazwa, na kuhakikisha kuwa maamuzi ya afya ya jamii yanaongozwa na ushahidi wa kisayansi.
Uzinduzi huu unajenga juu ya mafanikio ya mradi wa Mtandao wa Kikanda wa Maabara za Marejeleo za Magonjwa yanayoambukiza (EAC Regional Network of Reference Laboratories for Communicable Diseases Project), ambao umeimarisha ujiandaaji na ukabilianaji wa kikanda dhidi ya magonjwa ya virusi ya hatari kubwa.
Kupitia Mtandao wa Maabara Zinazotembea wa EAC (EAC Mobile Laboratory Network), ulioanzishwa mnamo mwaka 2017, kanda imeimarisha uwezo wake wa kukabiliana haraka na milipuko kwa kupunguza muda wa kutoa majibu ya vipimo vya maabara kutoka takriban saa 72 hadi saa 8, na hivyo kuwezesha maamuzi ya afya ya jamii ya haraka zaidi na yenye taarifa sahihi.
Kituo hiki kitaendeleza zaidi mbinu ya EAC ya Afya Moja (One Health approach) kwa kuimarisha ushirikiano katika sekta za afya ya binadamu, afya ya wanyama na mazingira, ikitambua uhusiano wa karibu wa matishio ya magonjwa ya kuambukiza yanayoibuka.
Uendeshaji wa UVRI kama Kituo cha Kikanda cha Ubora cha EAC katika Elimu ya Virusi umesaidiwa kupitia Mradi wa Mtandao wa Kikanda wa Maabara za Marejeleo za Magonjwa yanayoambukiza, kwa usaidizi kutoka Serikali ya Jamhuri ya Shirikisho ya Ujerumani kupitia KfW na usaidizi wa kiufundi kutoka Bernhard Nocht Institute for Tropical Medicine (BNITM).
Akizungumza katika uzinduzi huo, Bw. Jan Alber, Mkurugenzi wa KfW nchini Uganda, alithibitisha upya kujitolea kwa KfW katika kusaidia usalama wa afya wa kikanda na mifumo thabiti ya afya.
“KfW ina fahari kusaidia hatua hii muhimu katika kuimarisha uwezo wa Afrika Mashariki wa kuzuia, kugundua na kukabiliana na matishio ya magonjwa ya kuambukiza. Tunaendelea kujitolea kuunga mkono kanda kama chanzo cha kudumu cha utafiti, uvumbuzi na uthabiti kupitia mifumo na ushirikiano imara wa maabara,” alisema.
Kwa upande wake, Naibu Balozi wa Ujerumani nchini Uganda, Peter Primus, alibainisha kuwa maabara sita za kontena kwa sasa zipo katika mchakato wa ununuzi na zitasaidia utambuzi wa magonjwa ya kuambukiza, usindikaji wa sampuli za bakteria na upimaji wa usugu wa dawa dhidi ya viuavijasumu (antibiotics) vinavyotumiwa sana.

 Hatua hii inafanya ufuatiliaji wa usugu wa vimelea dhidi ya dawa (AMR) unaofanyika maabarani kuwa sehemu kuu ya mikakati ya kitaifa na kikanda katika eneo ambalo magonjwa na vifo vinavyohusiana na AMR viko juu na vinaendelea kuongezeka.



Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC),Andrea Ariik akizungumza na waandishi wa habari baada ya uzinduzi huo.

Post a Comment

Previous Post Next Post