![]() |
| Katibu wa Itikadi,Uenezi na Mafunzo wa CCM mkoa wa Arusha, Saipulan Ramsey akizungumza na waandishi wa habari. |
Filbert Rweyemamu,Arusha
Wananchi wa mkoani Arusha wametakiwa kujitokeza kwa wingi katika mikutano ya hadhara itakayofanyika wakati wa ziara ya Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi ili kuwasilisha changamoto zao zitakazopatiwa ufumbuzi na viongozi wa chama hicho pamoja na serikali.
Katibu wa Itikadi, Siasa na Uenezi wa CCM mkoa wa Arusha, Saipulan Ramsey ametoa wito huo katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu ziara ya siku tatu ya Kihongosi inayotarajiwa kuanza Juni 4 hadi 6,2026 .
Amesema ziara hiyo sio ya kisiasa kwasababu CCM ilifanya hivyo kwa miezi mitatu kwenye kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka jana na kupata ushindi mkubwa na sasa wanatekeleza ahadi kwa wananchi waliokiamini chama hicho kwa kukipa dhamana ya uongozi.
"Hii ziara sio ya kisiasa,chama chetu kimefanya siasa kwa miezi mitatu,kwahiyo sasa hivi kiongozi wetu anakuja kuhimiza na kusukuma yale tuliyoahidi wananchi,atakagua miradi ya serikali na kutolea maelekezo mahususi katika ukamikishaji au uanzishaji na umaliziaji wa miradi ambayo imeshaanza"amesema Saipulan
Saipulan amesema katika ziara ya Kihongosi atatembelea wilaya za Karatu,Arumeru na Arusha Mjini kulingana na ratiba atakagua mashina ya CCM,kukagua miradi ya serikali na chama pamoja na kufanya mikutano ya hadhara ambayo wananchi watatoa kero na changamoto na kupatia ufumbuzi.
Pia,ziara hiyo itahusisha kukagua uhai wa chama katika ngazi mbalimbali kuanzia matawi, Kata, Wilaya na mkoa kwa lengo la kuimarisha Chama Cha Mapinduzi na kuongeza ushiriki wa wanachama katika shughuli za kisiasa na maendeleo ili kiendelee kuaminiwa na wananchi.
“Kama ambavyo mmemsikia wakati akiwa mkoa wa Kilimanjaro amezungumzia kwa kina suala la mikopo ya asilimia 10 kwa makundi ya wanawake,vijana na wenye ulemavu,hili ni suala ambalo chama chetu linachukulia kwa uzito unaostahili kwasababu fedha hizo zimesaidia makundi hayo kiuchumi,”
“CCM inataka maafisa Maendeleo ya Jamii kwenye ngazi ya Kata kuyasaidia makundi hayo ili shughuli za kiuchumi wanazofanya ziwe na tija,wasiishie kutaja vikundi vilivyopo kwenye maeneo yao bali tuone tija ya fedha zinazoelekezwa huko,”amesema Saipulan
Katika hatua nyingine, ameongeza kuwa CCM mkoa wa Arusha imefanikiwa kufika katika Kata 107 kati ya kata 161 zilizopo kukagua utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi na uhai wa chama hicho ziara ya awamu ya pili inayoongozwa na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Arusha, Thomas Ole Sabaya.


إرسال تعليق