SERIKALI YATOA UHAKIKA WA CHAKULA CHA SAMAKI, BUNDA KUNUFAIKA NA MPANGO WA BODI ZA KISASA


Na Janeth Raphael - Dodoma

WIZARA ya Mifugo na Uvuvi imewahakikishia wafugaji wa samaki kwa vizimba nchini kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha upatikanaji wa chakula cha samaki na vifaa muhimu vya ufugaji unaboreshwa ili kukuza tija katika sekta hiyo inayokua kwa kasi nchini.

Kauli hiyo imetolewa leo Mei 26, 2026 bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dkt. Bashiru Ali, wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya (CCM), aliyehoji kuhusu changamoto ya upatikanaji wa chakula cha samaki kwa wafugaji wa vizimba pamoja na mpango wa Serikali wa kuwapatia boti za kisasa wafugaji wa Wilaya ya Bunda.

Akijibu swali hilo, Dkt. Bashiru amesema Serikali inatambua uwepo wa changamoto ya upungufu wa chakula cha samaki, hasa kutokana na kuongezeka kwa kasi kwa shughuli za ufugaji wa samaki kwa vizimba katika maeneo mbalimbali nchini.

Amesema ufugaji wa samaki kwa vizimba ni moja ya sekta mpya zinazokua kwa kasi kubwa na zimeendelea kuvutia wawekezaji pamoja na wananchi wengi wanaotafuta fursa za kiuchumi kupitia sekta ya uvuvi na ufugaji wa samaki.

“Kadri shughuli hizi zinavyopanuka, mahitaji ya chakula cha samaki nayo yanaongezeka kwa kiwango kikubwa, jambo ambalo kwa kipindi fulani limekuwa likisababisha changamoto ya upatikanaji wa chakula hicho kwa wakati,” amesema Dkt. Bashiru.

Hata hivyo, Waziri huyo amesema hali hiyo inaanza kuimarika kutokana na kuongezeka kwa uwekezaji katika viwanda vya uzalishaji wa chakula cha samaki nchini.

Amevitaja baadhi ya viwanda hivyo kuwa ni pamoja na kiwanda kilichopo Dar es Salaam pamoja na viwanda vingine vilivyoanzishwa jijini Mwanza na katika maeneo mengine kupitia wawekezaji binafsi waliovutiwa na mahitaji makubwa ya soko.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, kuongezeka kwa wazalishaji wa chakula cha samaki kutasaidia kushusha bei ya bidhaa hiyo na hivyo kupunguza gharama kwa wafugaji wa samaki nchini.

“Kadri wazalishaji wa chakula cha samaki wanavyoongezeka, ushindani unaongezeka na bei zinaendelea kushuka, jambo ambalo litasaidia kufanya shughuli za ufugaji wa samaki kuwa nafuu zaidi kwa wananchi,” amesema.

Aidha, Dkt. Bashiru amesema Serikali inaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji wa sekta hiyo ili kuhakikisha uzalishaji wa chakula cha samaki unaongezeka sambamba na mahitaji yaliyopo sokoni.

Amefafanua kuwa gharama za chakula cha samaki ndizo zinazobeba sehemu kubwa ya matumizi katika ufugaji wa samaki kwa vizimba, ambapo zaidi ya asilimia 70 ya gharama zote za uzalishaji hutokana na ununuzi wa chakula hicho.

Kutokana na hali hiyo, amesema Serikali inalenga kuhakikisha upatikanaji wa chakula hicho unakuwa wa uhakika na kwa bei nafuu ili kuongeza faida kwa wafugaji na kuvutia wananchi wengi zaidi kuingia kwenye sekta hiyo.

Kuhusu suala la upatikanaji wa boti za kisasa kwa wafugaji wa samaki kwa vizimba wilayani Bunda, Waziri huyo amesema Serikali tayari imeunda tume maalumu yenye jukumu la kupitia na kuboresha mfumo wa utoaji wa boti hizo.

Amesema lengo la hatua hiyo ni kuhakikisha boti zitakazotolewa zinakidhi viwango vinavyotakiwa na mahitaji halisi ya wafugaji ili ziweze kusaidia shughuli za ufugaji kwa ufanisi zaidi.

Dkt. Bashiru ameongeza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya uvuvi na ufugaji wa samaki ili kuimarisha uchumi wa wananchi kupitia sekta hiyo ambayo imeendelea kuonekana kuwa na mchango mkubwa katika ajira, lishe na ukuaji wa uchumi wa Taifa.


Post a Comment

أحدث أقدم