WAKALA WA VIPIMO WAITIKIA WITO WA RAIS SAMIA KUHUSU UPANDAJI MITI

  

Na WMA – Dodoma

Watumishi wa Wakala wa Vipimo (WMA), wameitikia wito wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unaowataka watanzania kupitia makundi mbalimbali kupanda miti katika maeneo yao ili kuhifadhi mazingira.

Akiongoza zoezi la upandaji miti katika eneo ilipo Ofisi Kuu ya WMA Medeli jijini Dodoma, mapema leo Machi 20, 2026 Meneja Utawala na Rasilimali Watu, Charles Mavunde amewasisitiza watumishi wa Wakala hiyo nchi nzima kuzingatia maelekezo ya Serikali kwa kupanda miti na kuitunza ili kulinda mazingira.

Amesema kuwa, Mheshimiwa Rais Samia amekuwa akisisitiza mara kwa mara kuhusu upandaji miti katika maeneo mbalimbali na kwamba yeye mwenyewe ameonyesha mfano kwa kuwa kinara wa upandaji miti, hivyo WMA imeona ni vyema pia iitikie wito huo.

“Mtakumbuka kwamba, hata Mheshimiwa Dkt. Emmanuel Nchimbi, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akimwakilisha Mhe. Rais katika maadhimisho ya siku ya upandaji miti duniani na maadhimisho ya upandaji miti kitaifa, jana Machi 19, 2026 kule Lindi aliagiza kuwa makundi mbalimbali ya watanzania waendeleze utamaduni wa kupanda miti,” ameeleza Mavunde na kuhitimisha kuwa WMA imeyachukulia kwa uzito maelekezo ya viongozi hao na itayatekeleza kikamilifu.

Viongozi na watumishi mbalimbali wa WMA Makao Makuu wameshiriki zoezi hilo la upandaji miti akiwemo Mkurugenzi wa Huduma za Biashara Phanuel Mtuki, Meneja Sehemu ya Fedha, CPA Ibrahim Mbinga, Meneja Mkoa wa Dodoma Said Ibrahim, Meneja Mawasiliano Veronica Simba na Mkuu wa Kitengo cha Mipango, Nelson Ruturagara.

Wengine walioshiriki ni watumishi kutoka Idara mbalimbali wakiwemo maafisa, maafisa usafirishaji na wasaidizi wa ofisi.

WMA ni wakala ya serikali iliyo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara yenye jukumu kuu la kumlinda mlaji kupitia usimamizi wa matumizi sahihi ya vipimo katika sekta mbalimbali.

           

Post a Comment

أحدث أقدم