Mkuu wa mkoa wa Arusha,Amos Makalla akizungumza kwenye mkutano na maafisa usafirishaji wa abiria kwa kutumia Pikipiki na Bajaji mkoa wa Arusha uliofanyika kwenye viwanja vya Makumbusho.
Na Mwandishi
Wetu,Arusha
Mkuu wa mkoa
wa Arusha,Amos Makalla ametoa wito kwa maafisa usafirishaji wa Bodaboda na
Bajaj kumwombea dua njema ili uteuzi utakapofanyika aendelee kuwa Arusha
abadilishe sekta hiyo iwe ya kisasa kwa kuwapeleka viongozi wa umoja wao
kujifunza kwa wenzao katika jiji la Kigali,Rwanda.
Ametoa kauli
hiyo wakati akizungumza na maafisa hao
akiwa ameambatana na Wakuu wa wilaya zote sita
aliowaita kusikiliza changamoto zao katika utaratibu aliojiwekea wa
kusikiliza wananchi katika makundi mbalimbali ili kuzipatia ufumbuzi wa haraka.
“Wakati
mwingine sio vizuri kutoa ahadi ukiwa na furaha,mniombee kwa mwenyezi
Mungu mkeka ukitoka nami niendelee
kuwepo Arusha,nitawapeleka baadhi ya viongozi wenu kwenye jiji la Kigali
kujifunza kama nilivyofanya wakati nikiwa Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam na
sekta hiyo ilibadilika,”
“Niliwaambia
viongozi wenzangu wakati nipo mkoa wa Mbeya, hii kazi ya usafirishaji wa abiria
kwa kutumia Pikipiki na Bajaj ni kazi kama zilivyo kazi nyingine, wanafanya kazi muhimu ya
kutunza familia zao pia ni wasomi wa ngazi mbalimbali hivyo itengenezewe
mazingira mazuri ,”amesema Makalla
Amewakata
wakuu wa wilaya za mkoa huo kuweka utaratibu wa kusikiliza kero za wananchi
kwenye Kata zao na kupitia halmashauri za wilaya kuweka utaratibu wa
kuwakopesha waendesha Bodaboda na Bajaj kama yalivyo makundi mengine
wanaonufaika na mikopo ya asilimia 10.
Awali Katibu
wa Umoja wa Bodaboda mkoa wa Arusha,Hakimu Msemo akisoma risala ya umoja wao
amesema shughuli zao zinatoa mchango mkubwa kiuchumi kwa kutoa ajira kwa vijana
na kupunguza ukosefu wa usalama kwenye jamii.
Mbali na
kujikwamua kiuchumi ameongeza kuwa usafishaji huo unakuza sekta ya utalii wa
ndani kutokana na madereva wa vyombo hivyo kuwafikisha wateja wao maeneo
mbalimbali kwa haraka na wamekua wakishiriki shughuli za kijamii ikiwemo
kufanya usafi kwenye vituo vya mabasi na hospitalini.
“Mkuu wa
mkoa katika kipindi kilichopita tumeshuhudia mahusiano kati ya umoja wetu na
serikali yakiimarika kwa kutambua kazi yetu na kuwaingiza kwenye mfumo wa kanzi
data madereva kwenye vituo vyao ili watambulike kirahisi na kuepuka wasio na
nia njema kujiingiza kwa manufaa binafsi,”amesema Msemo
Amesema
licha ya mafanikio hayo zipo changamoto zinazowakabili zikiwemo kukosekana na
vituo vya kudumu,ukosefu wa mafunzo ya udereva kwa baadhi ya watoa
huduma,kuendesha pikipiki na Bajaj bila leseni na ukosefu wa mikopo rafiki ya
kuboresha kazi zao.
Naye Katibu
wa waendesha Bajaj mkoa wa Arusha,Salim Lyimo amesema umoja wao una wanachama
3,000 katika Jiji la Arusha ambao wamekua wakijipatia kipato cha kuendesha
maisha yao lakini zipo changamoto zinazowakabili na kumwomba Mkuu wa mkoa
azipatie ufumbuzi.
Amezitaja
changamoto hizo kuwa ni kuondolewa kwenye vituo vyenye abiria wengi na
kupelekwa sehemu ambako ambako hakuna abiria na miradi ya pamoja waliyokua
wameianza kushindwa kuendelea baada ya kufutwa kwa vituo vilivyokua
vinawaunganisha pamoja.
“Tunaomba
vituo vya Bajaj vipangwe upya hasa maeneo yenye majengo
makubwa,masoko,hospitali na vituo vya magari ili tuweze kufanya biashara,pia
maeneo yasiyo na usafiri wa daladala ambayo ni Kijenge Juu,Ngusero,Lemara na
maeneo mengine tupewe kipaumbe,”amesema Lyimo
Kwa upande
wake Kiongozi wa waendesha Bajaj wenye mahitaji maalumu,Protas Ulomi ameshauri
miundombinu ya Jiji la Arusha iboreshwe ili iendane na ongezeko la idadi ya
watu pamoja na vyombo vya usafirishaji badala ya serikali kuchagua njia moja ya
kuviondoa vyombo hivyo Katikati ya mji.
mwisho



إرسال تعليق