Balozi
wa Jamhuri ya Ireland Paul Sherlock amepokea maombi ya ushirikiano
baina ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa na nchi yake yaliyolenga
kuongeza uzalishaji wa zao la alizeti mkoani humo jambo litakalopelekea
kuinua kipato cha mkulima wa mkoa wa huo.
Maombi
hayo yaliyowasilishwa na mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo kwa
balozi huyo mapema mwezi huu yalionyesha hali ilivyo ya uzalishaji wa
zao hilo kwa sasa, ambapo kati ya hekta za shamba la Alizeti 0.5 hadi 2
huzalisha tani 1.1 badala ya tani 2.5.
“Nimefurahishwa
sana na jitihada za Mh. Joachim Wangabo kwa kuona umuhimu wa kutafuta
zao mbadala la biashara katika Mkoa wa Rukwa ikiwa ni pamoja na kuinua
kulimo cha mkoa na kuinua kipato cha wakulima wadogo na hatimae
kuwatafutia namna ya kuongeza viwanda vidogo na kuongeza ajira,” Alisema
Balozi Sherlock.
Kwa
upande wake Mh. Wangabo amesema kuwa zao la mahindi linazalishwa kwa
wingi sana katika mkoa wake na wakulima hulichangamkia hilo zaidi ila
bei ikitetereka wakulima hao wanakosa pa kujishika hivyo kwakuwa zao la
alizeti ni la pili la kibiashara basi ni vyema kulitafutia mikakati liwe
sawa na zao la mahindi ili wananchi wachague.
“Kwa
mwaka 2016/2017 hekta 47,862 zililimwa alizeti na tukapata tani 53,470
ambayo ni chini ya kiwango tunachotakiwa kuzalisha kutokana na tafiti
mbalimbali zilizofanywa kwa hekta 47,862 zikilimwa vizuri tunaweza
kupata tani 119,655 ambayo ni ongezeko la asilimia 55, tunataka kufika
huko, tuzalishe mafuta ya alizeti kwa wingi, kutengeneza ajira na
kuongeza viwanda,” Alisema Mh. Wangabo.
Ameongeza
kuwa kwa kufanya hivyo kutalipunguzia taifa mzigo wa kununua mafuta nje
ya nchi jambo linalopelekea serikali kutumia pesa nyingi kufanya
manunuzi na hatimae pesa hiyo kubaki kwa wakulima wetu.
Mkoa
wa Rukwa unatarajia kushirikiana na Shirika lisilo la kiserikali la
Faida mali ambalo limefanikiwa kwa kiwango kikubwa kukuza zao la alizeti
katika Mkoa wa Singida ili kuhamishia ujuzi huo katika Mkoa wa Rukwa.
Kwa
mujibu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na uwekezaji, Tanzania hutumia
Shilingi bilioni 189.6 kila mwaka kununua mafuta ya kula nje ya nchi
huku ikizalisha tani 91,000 ambayo ni sawa na asilimia 40 za mafuta hayo
tofauti na makadirio ya tani 200,000 hadi 300,000 ya uhitaji wa bidhaa
hiyo kwa mwaka.
Mkuu
wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (kulia) akipeana mkono na Balozi wa
Jamhuri ya Ireland nchini Paul Sherlock muda mfupi baada ya maongezi ya
mikakati ya kukuza uzalishaji wa zao la Alizeti Mkoani Rukwa.
No comments:
Post a Comment