Na Chalila Kibuda, Globu ya Jamii
MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari (TPA) imeadhimisha miaka 13 tangu
kuanzishwa huku ikijivunia mafanikio ya kuongezeka kwa biashara kuanzia
mwaka 2011.
Pia mapato yamekuwa yakiendelea kupanda na kuanzia Julai mwaka 2017
hadi mwaka 2018 shehena iliyokuwa ikiingia ilianza kupanda na meli
zinazoingia kufikia takriban 3000 kwa mwezi.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa TPA
wakati akielezea Wiki ya Mamlaka hiyo iliyoanza jana na kilele chake
kufikiwa Jumapili.Ambapo watatumia maadhimiaho hayo kueleza walikotoka
tangu April 2005, walipo na wanakotarajia kwenda kwa ajili ya kuboresha
zaidi huduma kwa biashara.
Amesema TPA imekuwa ikiendelea kuboresha utoaji wa huduma na kuongeza
masoko huku wakikusanya Sh.bilioni 420 kwa kipindi cha miezi sita
iliyopita."Mamlaka hiyo, inalenga kuboresha zaidi huduma zake, kwa
kuandaa mazingira ya serikali kupata mapato yake kwa kuwa kati ya
asilimia 45 hadi kufikia 55 ya kodi inayokusanywa na Mamlaka ya Mapato,
hupatikana TPA," amesema.
Kakoko amesema wanatarajia kutekeleza mradi ya ujenzi wa bandari kavu
katika baadhi ya mikoa ikiwemo Kigoma, Arusha, Mbeya na hata Mwanza
wanalenga kuwapa unafuu wateja wao kutoka nje ya nchi wanaokuwa
wakifuatilia bidhaa katika Mamlaka hiyo.
Kuhusu maadhimisho hayo ya miaka 13,amesema watatoa elimu kwa wadau
mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara namna ya utendaji wa Mamlaka
hiyo.Pia, kuchangia damu kwa wagonjwa, kutoa viti vya walemavu vya
magurudumu mawili na vifaa vya kisasa vya kupima joto mwilini.
“Nia ya bandari ni kuongoza katika biashara kwa utoaji huduma ya
uhakika katika mtandao wa uchukuzi katika Kanda zinazozunguka."Ikiwa
pamoja na kuongeza mapato kwa kusimamia bandari katika kutoa huduma bora
na nafuu kwa kutumia mbinu na teknolojia kisasa Ukanda wa Mashariki,
Kati na Kusini mwa Afrika ,”amesema Kakoko
Ameongeza Mamlaka hiyo inatekeleza miradi katika kuboresha utoaji wa
huduma na katika eneo la miundombinu, wana mpango wa kuchimba lango kuu
ya kuingilia bandari katika eneo la Feri, jijini Dar es Salaam.Amesema
jambo hilo litasaidia kuingia kwa wingi meli kubwa pamoja na makasha
mengi zaidi.
Pia amesema Mamlaka inatekeleza miradi ya maendeleo mbalimbali katika
bandari ya Dar es Salaam, Tanga, Mtwara na katika bandari zilizopo
maziwa makuu ya Viktoria, Tanganyika na Nyasa kwa kujenga magati na
kuboresha yaliyopo.Ameongeza pia ununuzi wa vifaa mbalimbali ili kuweza
kuwa na bandari za kisasa zitakazokuwa na uwezo wa kuhudumia shehena
kubwa zaidi.
“Uboreshwaji wa miundombinu ya bandari si tu kwa Bandari ya Dar es
Salaam lakini na Mtwara na Tanga na hata katika maziwa yote makuu,”
amesema.Akizungumzia usalama Kakoko amesema wameendelea kuboreshwa
ulinzi na wana mpango wa kuweka mashine za kukagulia mizigo (scanning
machine) katika mipaka yote na ofisi zote
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bodi ya TPA, Profesa Ignatus
Rubalatuka amesema ili Mamlaka iyafikie malengo yake inatekeleza
vipaumbele vitano ambavyo ni maendeleo ya rasilimali watu, uboreshwaji
wa miundombinu,matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA),
kudumisha ulinzi na usalama pamoj ana kuongeza juhudi za kimasoko.
Amesema suala la ulinzi na usalama wa mali za wateja alisema ni jambo
linalopewa kipaumbele kwa kuhakikisha ipo miundombinu ya vifaa vya
ulinzi vya kisasa.
Mwenyekiti
wa Bodi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Profesa Ignas
Rubaratuka akizungumza kuhusiana na maadhimisho ya miaka 13 ya Mamlaka
usimamizi wa bandari yaliyoanza leo , jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi
Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Mhandisi Deosdidit
Kakoko akizungumza na waandishi kuhusiana na mafanikio ya kuanzishwa kwa
mamlaka ya usimamizi wa bandari, leo jijini Dar es Salaam.
Kaimu
Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Fransisca Muindi akizungumza na waandishi
wa habari kuhusiana na huduma watazozitoa katika maadhimisho ya miaka 13
ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari, leo jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment