Pages

April 10, 2018

JENGO LA MAMLAKA YA HIFADHI NGORONGORO KIVUTIO CHA KIHISTORIA UTOAJI HUDUMA ZA UTALII JIJINI ARUSHA




Na Hamza Temba - WMU

........................................................
JENGO la kitega uchumi la Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro jijini Arusha ambalo ujenzi wake unatarajiwa kukamilika mwezi juni mwaka huu litakuwa kivutio cha kihistoria cha utoaji wa huduma za utalii hapa nchini.

Hayo yameelezwa jana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla muda mfupi baada ya kukagua jengo hilo ambalo linasemekana kuwa refu kuliko majengo yote jijini Arusha likiwa na jumla ya ghorofa 18.

Alisema jengo hilo ambalo linatizamana na Round About ya AICC katikati ya jiji hilo, limekusudiwa kuwa Kituo Kimoja (One Stop Centre) cha shughuli zote za utoaji wa huduma za utalii jijini humo kuanzia uwekezaji, utangazaji na menejimenti kwa ujumla.

Alisema jengo hilo litatoa fursa kwa wadau mbalimbali wanaotoa huduma za utalii kuweka ofisi zao ikiwemo mabenki, watoa huduma za usafiri, mashirika ya ndege, mawakala wa safari za utalii na huduma, maduka ya bidhaa za utalii na mahoteli.

"Tutapamba pia jengo hili na" live screen" (Mabango ya Video Mubashara) za vivutio, hivyo wanyama wakiwa wanapita huko porini watakuwa wanaonekana "LIVE" (Mubashara) kwenye jengo hili kupitia LED Screen ambazo zitakuwa zimezunguka jengo hili" alisema Dk. Kigwangalla.Alisema huduma nyingine zitakazotolewa katika Jengo hilo ni pamoja na zile za kuangalia jiji la Arusha kupitia darubini, huduma za burudani ikiwemo kumbi za starehe na migahawa.

Kwa upande wake Mkandarasi wa jengo hilo, Mhandisi Bismas Meela wa Kampuni ya Inter-Consult limited alisema ujenzi wa jengo hilo ambalo ulianza mwezi Novemba, 2013 unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi juni mwaka huu.Alisema jengo hilo ambalo lina uwezo wa kupaki magari 67 kwa wakati mmoja katika ghorofa za chini linagharimu shilingi za Kitanzania bilioni 45.

Katika ziara hiyo ya siku moja ya ukaguzi wa jengo hilo, Dk. Kigwangalla aliongozwa na Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro, Dk. Fredy Manongi na Naibu Mhifadhi wa Huduma za Uendeshaji wa Mamlaka hiyo, Asangye Bangu. 
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla (wa pili kushoto) akipata maelezo kutoka kwa Naibu Mhifadhi wa Huduma za Uendeshaji wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro, Asangye Bangu kuhusu jengo la kitega uchumi la mamlaka hiyo lililopo katikati ya Jiji la Arusha ambalo limekusudiwa kuwa Kituo Kimoja cha shughuli zote za utoaji wa huduma za utalii jijini humo kuanzia uwekezaji, utangazaji na menejimenti kwa ujumla. Kulia ni Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dk. Fredy Manongi.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiangalia mandhari ya Jiji la Arusha akiwa juu ya Jengo la kitega uchumi la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro. Kutoka kulia ni Naibu Mhifadhi wa Huduma za Uendeshaji wa Mamlaka hiyo, Asangye Bangu na  Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dk. Fredy Manongi. 
Dk. Kigwangalla akiendelea kupata maelezo kuhusu jengo hilo kutoka kwa Naibu Mhifadhi wa Huduma za Uendeshaji wa mamlaka hiyo, Asangye Bangu. 

 Dk. Kigwangalla na msafara wake wakiangalia umbo la uso wa simba uliotengengenezwa katika moja lango la kuingilia kwenye lift ndani ya jengo hilo. Milango yote ya kuingilia kwenye lift ndani ya jengo hilo itapambwa kwa taswira mbalimbali za wanyamapori.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akishuka kwenye ngazi maalum zinazotumia nishati ya umeme ndani ya Jengo hilo. Kulia ni Naibu Mhifadhi wa Huduma za Uendeshaji wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro, Asangye Bangu na nyuma yake ni Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dk. Fredy Manongi. \
Waziri Kigwangalla akikagua kabati la kuhifadhia vitu katika moja ya Hotel Aprtment ndani ya jengo hilo. Kulia ni Naibu Mhifadhi wa Huduma za Uendeshaji wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro, Asangye Bangu.
Muonekano wa jengo hilo kutokea barabara ya Makongoro Jijini Arusha.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...