Pages

April 7, 2018

KATIBU MKUU NISHATI, AFANYA ZIARA KATIKA KAMPUNI YA TIPPER


Na Rhoda James, Dar es Salaam
 Tarehe 5 Aprili, 2018 Katibu Mkuu wa Nishati Dkt.  Hamisi Mwinyimvua alifanya ziara katika kampuni ya kuhifadhi mafuta  ya TIPPER iliyopo Kigamboni Jijini Dar e Salaam. Lengo la ziara hiyo lilikuwa ni kufahamu utendaji kazi wa kampuni pamoja na kutatua changamoto mbalimbali.

Akitoa maelezo kwa Dkt. Mwinyimvua, Mkurugenzi Mtendaji wa TIPPER, Stephane Gay alisema kampuni hiyo ina uwezo wa kuhifadhi mafuta  takriban mita za ujazo 212, 000 na kuongeza kuwa ujenzi wa upanuzi bado unaendelea ili kuwa na uwezo wa kuhifadhi mafuta mengi zaidi.

Alisisitiza kuwa tayari matanki mawili yenye uwezo wa kuhifadhi mita za ujazo 30,000 yanajengwa kwa ajili ya upanuzi. Alifafanua kuwa nafasi ya kuhifadhi mafuta kwa sasa ni ndogo.

Akijibu swali la Katibu Mkuu Mwinyimvua aliyetaka kufahamu kiasi cha mafuta kinachotumika nchini na kinachosafirishwa nje ya nchi, Gay alisema kuwa, kwa sasa mafuta yanayosafirishwa kwenda nchi jirani ni asilimia 55 na yanayotumika nchini ni asilimia 45.

Akielezea changamoto za kampuni hiyo, Gay alisema kwa sasa kampuni inahifadhi tu mafuta tofauti na awali ambapo ilikuwa ikisafisha na kusafirisha mafuta na ukosefu wa eneo kwa ajili ya kupakia mafuta kwenye magari makubwa kabla ya kusafirishwa.


Akielezea hatua zilizofikiwa katika uboreshaji wa utendaji kazi wa kampuni, Gay alisema kwa sasa kampuni imefanikiwa kuweka flow meters mbili pamoja na kuanza ujenzi wa matanki mawili ya kuhifadhia mafuta.


Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Nishati, Dkt. Hamisi Mwinyimvua aliupongeza uongozi wa kampuni ya TIPPER na kusema kuwa Wizara ya Nishati itafanyia kazi changamoto zilizowasilishwa.
 Katibu Mkuu wa Nishati Dkt.  Hamisi Mwinyimvua (katikati) akipata maelezo kuhusu flow mita mbili mpya zilizopo katika eneo la kampuni ya TIPPER. Wengine katika picha ni Viongozi Waandamizi kutoka Wizara ya Nishati na Uongozi kutoka Kampuni ya TIPPER.
 Katibu Mkuu wa Nishati Dkt.  Hamisi Mwinyimvua (wa pili kulia) akimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji kutoka TIPPER, Stephane Gay (hayupo pichani) aliyekuwa akitoa hotuba fupi kuhusu kampuni ya TIPPER. Wa kwanza kulia ni Kamishna wa Nishati, Mhandisi Innocent Luoga, wa tatu Kamishna Msaidizi wa Petroli, Mwanamani Kidaya na wa  nne Mjiologia Agnes Matulanya.
 Mkurugenzi Mtendaji kutoka TIPPER, Stephane Gay (wa pili kushoto) akimweleza jambo Katibu Mkuu wa Nishati Dkt.  Hamisi Mwinyimvua (hayupo pichani) kuhusu kampuni ya TIPPER. Wa kwanza kushoto ni Meneja Mahusiano wa TIPPER, Emmanuel Kondi, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa TIPPER, Paul Mnzava na  Meneja wa Terminal TIPPER, Martin Mosha.
 Meneja wa Terminal kutoka kampuni ya TIPPER, Martin Mosha akifafanua jambo kuhusu Flow mita kwa Katibu Mkuu wa Nishati Dkt.  Hamisi Mwinyimvua (katikati).
Muonekano wa matenki, mabomba mbalimbali yaliyopo katika eneo la kampuni ya TIPPER.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...