Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Taasisi za Kiraia
katika kuona malengo na dhamira zilizojipangia katika kuwahudumia
Wananchi zinafanikiwa vyema.
Alisema Taasisi nyingi za Kiraia zilizoanzishwa Nchini zimeonyesha
mwanga wa matumaini katika kusaidia huduma za Kijamii hasa kwenye Sekta
na miradi ya Elimu jambo ambalo Serikali inastahiki kujivunia na
kuendelea kuzipa ushirikiano huo.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na Uongozi wa
Taasisi ya Kiraia ya kumjengea uwezo wa Kielimu Mtoto wa Kike na
Mwanamke ya Forum for African women Educationalist {FAWE} hapo Ofisini
kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Alisema kundi kubwa la Wanawake hivi sasa tayari limeshaamka katika
kufukuzia maendeleo hasa katika masuala ya Kielimu kupitia Taasisi za
Kiraia jambo ambalo limewapa nafasi ya kushiriki katika makundi mbali
mbali ya maamuzi katika maeneo yao.
“ Kazi kubwa iliyofanywa na FAWE imewezesha kutoa msukumo kwa kundi
kubwa la wanawake kuamka katika kufukuzia maendeleo”. Alisema Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar.
Alieleza kwamba Historia inaonyesha wazi jinsi gani Mwanamke alivyokuwa
akikosa fursa kwa Karne nyingi zilizopita kutokana na mfumo dume
uliokuwa ukitumika kuwanyima haki zao hasa katika fursa za Uongozi na
Maamuzi ya msingi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliipongeza Taasisi hiyo ya FAWE kwa
kazi kubwa inayowajibika ya kumfinyanga Mtoto wa kike na Mwanamke katika
kumjengea msingi mzuri wa kujiamini Kimaisha kupitia Elimu.
Balozi Seif alisema jambo hili linapendeza kwa kuwaona Wazazi wenyewe
wameelimika na kutoa ushirikiano kwa watoto wao Kielimu. Hivyo aliupa
matumaini Uongozi huo wa FAWE kwamba atafanya juhudi za makusudi kwa
kuziomba Taasisi zilizoendelea kusaidia Miradi ya Maendeleo
iliyoanzishwa na Taasisi hiyo.
Mapema Mratibu wa Taasisi ya Kiraia ya kumjengea uwezo wa Kielimu Mtoto
wa Kike na Mwanamke ya Forum for African women Educationalist {FAWE}
Bibi Hinda Abdulla Ajmin alisema Taasisi hiyo iliyoasisiwa mnamo Mwaka
2002 ililenga kumshajiisha Mtoto wa Kike na Mwanamke katika Elimu ili
ajitambue.
Bibi Hinda alisema Fawe ilitekeleza Miradi Miwili mikubwa ya Tuseme
katika kumjengea uwezo wa kujiamini Mtoto wa Kike katika harakati zake
za Kimasomo pamoja na ule wa Stamp uliolenga kumjenga Mtoto wa Kike
kupenda masomo ya sayansi.
Mratibu huyo wa FAWE Zanzibar alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar kwamba yapo mafanikio makubwa yaliyopatikana kupitia Miradi
hiyo Miwili ambayo ilijumuisha jumla ya Skuli 150 za Sekondari Unguja na
Pemba iliyokwenda sambamba na kufunguliwa kwa Klabu zilizojumuisha
Watoto watano.
Bibi Hinda alifafanua kwamba Taasisi hiyo hivi sasa imepata changamoto
kubwa katika kuendesha ratiba zake kiufanisi kutokana na wafadhili
waliokuwa wakiiunga mkono kumaliza muda wao wa mkataba mnamo mwaka
2017.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
alikutana na Viongozi wa Dini pamoja na wa Wizara ya Kazi, Uwezeshaji,
Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto kuzungumzia Wimbi la vitendo vya
udhalilishaji wa Kijinsia na kuangalia Mikakati ya kupambana na janga
hilo.
Katika mazungumzo yao Viongozi wa Dini Sheikh Fadhil Suleiman Soraga,
Sheikh Salim Mohammed Hassan na Padre Charles Nundu walisema Jamii
imefikia pahali pa kuona aibu kiasi kwamba nguvu za pamoja zinahitajika
katika kukabiliana na janga hilo la udhalilishaji.
Walisema Jamii bado ina usiri wa kutoa ushahidi kwa kesi za
Udhalilishaji na hatma yake zinakuwa sugu katika utekelezaji wake na
kupelekea kuchangia uvurugaji wa Amani ya Nchi kwa Watu kuamua
kujichukulia hatua mikononi Mwao.
Walieleza kwamba yapo baadhi ya matukio ya Kisiasa katika maeneo tofauti
Nchini yanayoambatanishwa na kesi za udhalilishaji jambo ambalo ni
hatari kwa Amani ya Taifa na Watu wake.
Viongozi hao wa Kidini wamependekeza kuanzisha kwa Kampeni na Operesheni
Maalum Mitaani ya kuwafichuwa wadhalilishaji wa Kijinsia kwa kuwapa
fursa Wananchi kuwataja wahusika wa Vitendo hivyo ambao wanajuilikana
katika maeneo yao.
Nao Viongozi wa Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na
Watoto walisema Serikali kupitia Wizara hiyo tayari imeshazindua Mpango
Mtambuka wa Miaka Mitano wenye lengo la kupambana dhidi ya vitendo vya
Udhalilishaji wa Kijinsia Nchini.
Walisema Mpango huo unatoa fursa pana zaidi ya ushiriki wa kila mwana
Jamii, Viongozi na hata Taasisi za Kiraia kutoa nguvu zao za pamoja
katika azma ya kuona vitendo hivyo viovu vipakwisha au kupungua kwa
kiasi kikubwa.
Viongozi hao wa Wizara inayosimmaia Wanawake na Watoto walifahamisha
kwamba zipo dalili za mafanikio katika utekelezaji wa Mpango huo
Mtambuka kuafuatia baadhi ya sheria kufanyiwa marekebisho ili kukidhi
mahitaji ya sasa ya kukomesha tatizo hilo sugu.
Akitoa nasaha zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Iddi alisema vitendo vya udhalilishaji wa Kijinsia vinavyowaathiri zaidi
Akinamama na Watoto vinaendelea pia kuidhalilisha Nchi na Jamii kwa
ujumla.
Balozi Seif alisema Zanzibar hivi sasa imekumbwa na wimbi la Dawa za
Kulevya ambalo limefikia hatua ya kuundiwa Taasisi ya kupapambana na
changamoto hilo kiasi kwamba ipo haja pia ya kuangalia uwezekano wa
kuunda Taasisi itakayosimamia masuala ya kupiga vita udhalilishaji wa
Kijinsia.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kati kati akizungumza
na Uongozi wa Taasisi ya Kiraia ya kumjengea uwezo wa Kielimu Mtoto wa
Kike na Mwanamke ya Forum for African women Educationalist {FAWE}
hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar. Wa kwanza kutoka kushoto ni
Mratibu wa FAWE Bibi Hinda Abdullah Ajmin na wa kwanza kutoka Kulia ni
Mshika Fedha wa FAWE Bibi Sabra Issa Mohammed.
Mratibu wa Fawe Bibi Hinda Abdullah Ajmin Kushoto akimfafanulia Balozi
Seif Miradi mbali mbali iliyoanzishwa na Taasisi hiyo ambayo tayari
imeshamsaidia Mtoto wa Kike kujikomboa Kielimu.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alizungumza na
Viongozi wa Dini pamoja na wa Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana,
Wanawake na Watoto kujadiliana Wimbi la vitendo vya udhalilishaji wa
Kijinsia na kuangalia Mikakati ya kupambana na janga hilo. Picha na –
OMPR – ZNZ
No comments:
Post a Comment