WATANZANIA WAONGOZA UBUNIFU WA BENDERA NA NEMBO ZA EAC

Filbert Rweyemamu,Arusha
Idadi ya vijana wa Tanzania walioshiriki mashindano ya kubuni alama za mwonekano mpya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki(EAC) zikiwemo bendera na nembo imekua kubwa ukilinganisha na washiriki wa nchi nyingine kwa pamoja.

Jumla ya kazi za ubunifu 373 zilizowasilishwa kutoka nchi sita ambazo ni wananchama wa EAC watanzania pekee walioshiriki kwa kutuma ubunifu wao ni 238.

Mratibu wa Mawasiliano katika Sekretariati ya EAC,Florian Mutabazi ameliambia Mwananchi kuwa waliotuma kwa njia ya barua pepe walikua 141 na posta 97 huku washiriki saba wakishindwa kutambulisha utaifa wao.

Ametaja idadi ya washiriki kutoka nchi nyingine kuwa Uganda ni 54, Kenya 40, Rwanda 19, Burundi 13 na mwanachama mpya wa EAC,Sudani Kusini ilipata washiriki wawili tu.

Jumuiya ya Afrika Mashariki inakusudia kupitia mashindano hayo kupata mwonekano mpya utakaokidhi matakwa ya sasa ya idadi ya wanachama na kuwa na utambulisho ambao ni rahisi kwa mwananchi yeyote kuutambua.

Pia EAC ina taasisi kadhaa miongoni mwa hizo ni Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki(EAKC) yenye makao yake Zanzibar,Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria(LVBC) na nyingine ambazo zipo katika utaratibu maalumu wa kuwa na utambulisho unaojiungamanisha na nembo ya EAC.
 
Mradi huu ukiacha zawadi watakazopata washindi wa watatu wa mwanzo jumla ya dola 35,000 ambazo ni zaidi ya Sh 77 milioni pia gharama nzima ya kuipatia EAC na taasisi zake utambulisho mpya  inafikia dola  200,000 sawa na Sh 446 milioni.

Post a Comment

Previous Post Next Post