Na Teresia Mhagama, DSM
Waziri
wa Nishati, Dkt Medard Kalemani na Waziri wa Mafuta na Gesi wa Oman,
Dkt. Mohamed Al Rumhi wamekutana jijini Dar es Salaam na kujadiliana
masuala mbalimbali ya ushirikiano lengo likiwa ni kuendeleza Sekta ya
Nishati nchini.
Kikao
hicho kimefanyika katika Ofisi za Wizara jijini Dar es Salaam ambapo
Waziri huyo kutoka Oman aliambatana na Waziri wa Uwekezaji na Biashara
ya Nje wa Oman, Naibu Waziri wa Utalii na Balozi wa Oman nchini
Tanzania.
Kwa
upande wa Tanzania, viongozi mbalimbali walishiriki katika majadiliano
hayo akiwemo Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, Naibu Katibu Mkuu,
Dkt Mhandisi Juliana Pallangyo na watendaji wengine kutoka Idara ya
Nishati na Sheria.
Kwa
upande wake Waziri wa Mafuta na Gesi wa Oman, Dkt. Rumhi, alisema kuwa
lengo la Ujumbe huo kufika wizarani ni kujadiliana na watendaji wa
Wizara ya Nishati kuhusu maeneo ambayo ingependa ishirikiane na nchi
hiyo ya Oman na kwamba nchi hiyo ipo tayari kushirikiana na Tanzania.
“
Hapo zamani, Sisi Oman hatukutumia Gesi yetu vizuri kwa kuwa tulifanya
haraka kuiuza nje ya nchi lakini ninyi mnayo fursa sasa ya kuitumia gesi
yenu ndani ya nchi ili kutengeneza ajira pamoja na kuiendeleza kwa
matumizi mbalimbali, na ikiwa ziko fursa za ushirikiano ili kuendeleza
nishati hii, sisi tupo tayari,” alisema Dkt. Rumhi.
Akizungumzia
uhusiano uliopo kati ya Tanzania na Oman, Dkt. Rumhi alisema kuwa,
nchi hiyo inauthamini undugu uliopo na kwamba watalizingatia hilo katika
kutekeleza miradi ya ushirikiano ambayo itahusisha wasomi watanzania
ambao wameonyesha kuwa na uwezo wa kuendeleza Sekta ya Nishati.
Kwa
upande wake Waziri wa Nishati wa Tanzania, Dkt Kalemani, alisema kuwa
Tanzania imegundua Gesi Asilia kiasi cha futi za ujazo trilioni 57.25
huku matumizi yakiwa ni chini ya asilimia 30 hivyo bado kuna Gesi ya
kutosha kwa ajili ya miradi mipya ya uzalishaji Umeme na katika
kuanzisha viwanda kama vya kemikali na mbolea.
Alisema
kuwa kwa sasa Umeme unaotumika nchini, unazalishwa kwa kutumia Gesi
Asilia kwa zaidi ya asilimia 50 na kueleza kuwa, Serikali inahitaji
kuzalisha Umeme mwingi zaidi kwa kutumia Gesi hiyo.
“
Pamoja na hayo kwa leo napenda kuomba mambo manne ya ushirikiano ambayo
yatawafaidisha watanzania. Jambo la kwanza ni kuendeleza ushirikiano
katika utafiti wa mafuta katika Ziwa Tanganyika na Bonde la Eyasi
Wembere ambayo katika tafiti za awali yameonesha kuwa na viashiria vya
mafuta, hivyo ni muhimu kushirikiana katika tafiti zinazofuta na
hatimaye kuthibitisha endapo maeneo hayo yana mafuta kama viashiria
vinavyoonesha,” alisema Dkt Kalemani.
Alitaja
eneo la Pili ambalo Tanzania inahitaji ushirikiano ni kujenga uwezo wa
Wataalam ikiwemo utoaji wa mafunzo ya muda mrefu na mfupi kwa kuwa
Tanzania bado inakua katika Sekta ya mafuta na Gesi hivyo ni muhimu kwa
Tanzania kuwa na wataalam wengi zaidi.
Alitaja
jambo la Tatu la ushirikiano kuwa ni uzalishaji Umeme kwa kutumia Gesi
asilia jambo litakalopelekea gharama za nishati hiyo kupungua kwa
wateja na vilevile kuongeza kiasi cha Umeme nchini tofauti na megawati
1451 zilizopo sasa kwani lengo ni kufikia megawati 5000 ifikapo mwaka
2020 na megawati 10,000 ifikapo mwaka 2025.
“Jambo
la Nne, ni nchi ya Oman kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Petroli
Tanzania katika mradi wa usambazaji Gesi majumbani, viwandani na kwenye
magari jambo litakalopelekea ajira kwa wananchi wetu, kutunza mazingira
na kuongeza idadi ya viwanda nchini ikiwemo kiwanda mnachotarajia
kujenga hapa nchini,” alisema Dkt Kalemani.
Alisema
kuwa kwa sasa mradi wa majaribio ya usambazaji Gesi majumbani
umeshaanza, ambapo nyumba 70 zimesambaziwa Gesi hiyo jijini Dar es
Salaam huku lengo likiwa ni kuendelea kusambaza Gesi hiyo jijini Dar es
Salaam, Lindi, Mtwara na kisha katika mikoa mingine nchini.
Naye
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu alishukuru Ujumbe wa Oman kwa
kuitembelea Wizara ya Nishati na Ujumbe huo kutoa matumaini katika
kuyafanyia kazi maombi ya Waziri wa Nishati na kwamba ana imani undugu
baina ya pande hizo mbili utaendelezwa hasa katika kuendeleza miradi ya
Nishati nchini.
Waziri
wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (wa Tano kulia), Waziri wa Mafuta na
Gesi wa Oman, Dkt. Mohamed Al Rumhi (wa Nne kushoto) wakiwa katika picha
ya pamoja katika Ofisi za Wizara ya Nishati jijini Dar es Salaam.
Wengine katika picha ni Waziri wa Uwekezaji na Biashara ya Nje wa Oman,
Dkt. Salim Al Ismaily (wa tatu kushoto), Naibu Waziri wa Utalii wa Oman,
Maitha Al Mahrouqi, (wa pili kushoto), Balozi Mteule wa Oman hapa
nchini, Ali Al Mahruqi (wa kwanza kushoto), Naibu Waziri wa Nishati,
Subira Mgalu (wa nne kulia), Naibu Katibu Mkuu wa Wizara, Dkt. Mhandisi
Juliana Pallangyo (wa Tatu kulia), Kaimu Kamishna wa Nishati, Mhandisi
Innocent Luoga (wa kwanza kulia) na Balozi wa Tanzania nchini Oman,
Abdallah Kilima, (wa pili kulia).
Waziri
wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (wa nne kushoto), Waziri wa Mafuta na
Gesi wa Oman, Dkt. Mohamed Al Rumhi (wa Nne kulia) wakiwa katika Ofisi
ya Waziri wa Nishati jijini Dar es Salaam. Wengine katika picha ni
Waziri wa Uwekezaji na Biashara ya Nje wa Oman, Dkt. Salim Al Ismaily
(wa tatu kulia), Naibu Waziri wa Utalii wa Oman, Maitha Al Mahrouqi, (wa
pili kulia), Balozi Mteule wa Oman hapa nchini, Ali Al Mahruqi (wa
kwanza kulia). Wengine ni Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (wa tatu
kushoto), Naibu Katibu Mkuu wa Wizara, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo
(wa pili kushoto), na Balozi wa Tanzania nchini Oman, Abdallah Kilima,
(wa kwanza kushoto).
Waziri
wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (wa Tano kulia), Waziri wa Mafuta na
Gesi wa Oman, Dkt. Mohamed Al Rumhi (wa Tatu kushoto) wakiagana mara
baada ya kikao kilichofanyika katika Ofisi za Wizara ya Nishati jijini
Dar es Salaam. Wengine katika picha ni Waziri wa Uwekezaji na Biashara
ya Nje wa Oman, Dkt. Salim Al Ismaily (wa pili kushoto), Naibu Waziri wa
Utalii wa Oman, Maitha Al Mahrouqi, (wa kwanza kushoto), Naibu Waziri
wa Nishati, Subira Mgalu (wa nne kulia), Naibu Katibu Mkuu wa Wizara,
Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo (wa Tatu kulia), Kaimu Kamishna wa
Nishati, Mhandisi Innocent Luoga (wa kwanza kulia) na Balozi wa Tanzania
nchini Oman, Abdallah Kilima, (wa pili kulia).
No comments:
Post a Comment