Pages

July 18, 2017

RC NCHIMBI : WATUMISHI PUNGUZENI KULALAMIKA

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi amewataka watumishi kupunguza malalamiko na kuelekeza nguvu zao katika kuhudumia wananchi kwa mambo yanayoonekana kwa macho.

Dkt Nchimbi ameyasema hayo katika baraza maalumu la madiwani wa halmashauri ya Itigi ambapo amewataka watumishi na watendaji kupunguza muda wa vikao ili waende kuwatumikia wananchi.

Amesema kumekuwa na tabia ya kulalamika ambayo pia inaambukiza kwa watumishi na watendaji wengine badala ya kutoa suluhisho kwa changamoto ambazo zitawasaidia wananchi.

Dkt Nchimbi ameongeza kuwa watendaji na madiwani wasitumie muda mwingi ofisini pamoja na kusubiria taarifa za makaratsi ambazo hazina uhalisia wa matukio na hali halisi inayoendelea kwa wananchi.

Ameongeza kuwa utendaji wa mazoea na kulalamika ndiyo husababisha halmashauri kupata hoja za mkaguzi na mdhibiti wa hesabu za serikali licha ya kuwa na wataalamu wa kutosha ambao wana vyeti halisi.

Dkt Nchimbi amesema watumishi, watendaji na madiwani wanapaswa kuzingatia kuwaheshimu, kuwatambua, kuwathamini na kutowadanganya wananchi katika kuwatumikia kwakuwa wananchi wana uelewa wa kutosha juu ya mambo mbalimbali.

Aidha katika baraza hilo maalumu, madiwani wamepokea hoja 37 za mkaguzi na mthibiti wa hesabu za serikali ambapo halmashauri ya itigio imepata hoja 37 na hatiu inayodhirisha.

Dkt Nchimbi amewasisitiza watumishi, madiwani na viongozi wa halmashauri ya Itigi kufanya kazi kwa kuzingatia uadilifu na uaminifu ili waweze kuepuka kutengeneza hoja.

Ameongeza kuwa madiwani wasimamie kwa umakini miradi na shughuli za serikali ili thamani ya fedha iweze kuonekana kwa miradi hiyo huku akiwashauri kumtumia mkaguzi wa ndani kama kioo cha kuangalia dosari zao na kuzirekebisha mapema.

Kwa upande wake Mkaguzi wa Nje wa Hesabu za Serikali  Anna Kakunguru ameishukuru halmashauri ya Itigi  kwa ushirikiano na kuwaasa wasiwe wataalamu wa kujibu hoja bali wawe wataalamu wa kuzuia hoja.

Kakunguru amesema ofisi ya Mkaguzi wa nje itaendelea kushirikiana na halmashauri kwakuwa kazi yake kubwa ni kusimamia sheria zinafuatwa bila kupindishwa.

Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Dkt Angelina M Lutambi amewasa watendaji kuendelea kufuata maadili ya utumishi wa umma pamoja na maadili na maelekezo wanayopewa ili kuboresha utendaji wao.

Lutambi ameongeza kuwa kukiuka maadili na kutowahudumia wananchi ipasavyo ni kitengo cha kurudisha nyuma jitihada za Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania za kuwakomboa wananchi kiuchumi.

Awali katika baraza hilo Mkuu wa Mkoa wa Singida ametoa vyeti kwa madiwani wa halmashauri ya Itigi baada ya kuhitimu mafunzo ya kuibua na kusimamia miradi na ruzuku za serikali.
 Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi akimkabidhi Mwenyekiti wa halmashauri ya itigi Ally Minja cheti cha mafunzo ya usimamizi wa miradi ya serikali.
 Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi akizungumza na watumishi, watendaji na madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Itigi (hawapo pichani).
 Baadhi ya watumishi wa halmashauri ya Wilaya ya Itigi wakimsikiliza kwa makini Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi.
Mkaguzi wa Nje wa Hesabu za Serikali  Anna Kakunguru akizungumza katika baraza maalumu la halmashauri ya Wilaya ya Itigi.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...