Naibu Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia,Mhandisi Stella
Manyanya amesema serikali imeshaanda
ramani na fedha Sh 1 bilioni kwaajili ya ujenzi wa Shule ya mfano yenye ubora itakayotumika kwaajili
ya mazoezi kwa walimu wa elimu maalumu katika Chuo cha Ualimu Patandi.
Akizungumza wakati akifunga mafunzo ya walimu wa elimu jumuishi katika
Chuo cha Walimu Maalumu Patandi wilaya ya Arumeru ,Mhandisi Manyanya alisema serikali
inatambua umuhimu wa kuwaelimisha wenye ulemavu na imeamua kuwekeza katika Chuo
hicho ili kisaidie kuzalisha walimu wenye maarifa.
Jumla ya walimu 187 kutoka mikoa sita ya
Mara,Singida,Arusha,Manyara, Tanga na Kilimanjaro walipewa mafunzo maalumu kwa
siku 10 kuwawezesha kumudu kuwafundisha
vyema watoto wenye matatizo ya akili na usonji .
Alisema serikali ya awamu ya tano imedhamiria kutatua changamoto
hizo na katika bajeti ya mwaka wa fedha 2017/10 imeondoa kodi zote kwa
wawekezaji watakaoanzisha viwanda kwaajili ya kutengeneza vifaa vya watu wenye
mahitaji maalumu nchini.
Mhandisi Manyanya alisema kama taifa bado linakabiliwa na
changamoto mbalimbali za utoaji wa elimu maalumu kutokana na jamii kutokua na
uelewa wa watu wenye mahitaji maalumu ikiwemo ulemavu wa akili na usonji.
Changamoto nyingine aliyoitaja ni kuendelea kuwa na uwekezaji
usiozingatia watu wenye mahitaji maalumu hasa katika miundombinu huku walimu
walio wengi kukosa mafunzo kwaajili ya watoto wenye mahitaji maalumu na elimu
jumuishi.
Alisema tayari serikali imenunua vifaa kwaajili ya kujifunzia na
kufundishia watoto wenye mahitaji hayo vyenye thamni ya Sh 3.6 bilioni
vitakavyosambazwa shule mbalimbali zitakazopokea wanafunzi wenye mahitaji
maalumu.
"Sitakubali huu ufisadi uendelee haiwezekani walimu wa masomo
ya kawaida wapewe mafunzo maalumu kwaajili ya mahitaji yaliyopo na wanaporudi
kwenye halmashauri zao wanapangiwa kufundisha vipindi vya awali huu ni ufisadi
dhidi ya rasilimali ya watu wenye ulemavu,"alisema Mhandisi Manyanya
Alisema mpango wa wizara yake ni kuanza kuwatambua walimu wote
wenye elimu maalumu na kuwapangia kazi kwenye vituo vyenye watoto wenye
matatizo ya akili na usnji ili wayatumie vyema maarifa waliyoyapata.
katika hatua nyingine alisema katika bajeti ya mwaka wa fedha wa
2017/2018 serikali imetenga Sh 1 bilioni kwaajili ya ujenzi wa kituo cha kisasa
kwaajili ya mafunzo ya walimu eneo la Patandi mkoa wa Arusha.
Awali Mratibu wa mafunzo hayo,Ahiadu Sangoda alisema jumla ya
vituo vinne nchi nzima vimetoa mafunzo kwa walimu 710 lengo likiwa kuwajengea
maarifa,stadi na mwelekeo wa kufundisha wanafunzi wenye ulemavu wa akili na
wenye usonji kwa umahiri mkubwa.
No comments:
Post a Comment