Pages

May 29, 2015

Mbio za Urais, Majambazi wavamia Maafisa wa NEC na Wabunge wamshukia NYALANDU…#MAGAZETINI MAY29


RD

NIPASHE
Wakati wananchi wakilalamikia uandikishaji katika Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa mfumo mpya wa kielektroniki wa Biometric Voters Registration (BVR), maofisa 10 wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) wameshambuliwa na kujeruhiwa na watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wakati wakienda kuandikisha wapigakura wilayani Momba, mkoani Mbeya.
Walikumbwa na mkasa huo katika msitu wa Nyimbili, wakiwa njiani kutokea katika kata ya Chitete walikokuwa wanaandikisha wapigakura.
Mbali ya maofisa hao, dereva wa gari la halmashauri ya wilaya hiyo, Pius Kajula  ambaye ni mkazi wa Kamsamba, alijeruhiwa vibaya katika tukio hilo.
Akizungumza wodini katika Hospitali ya Serikali Mbozi, Kajula alisema tukio hilo lilitokea juzi usiku wakiwa njiani kutoka katika kijiji cha Chilulumo kuelekea kijiji cha Chitete baada ya kumaliza kuandikisha kata za Chilulumo, Ivuna na Mkomba.
Alisema saa 2:30 usiku akiwa anaendesha gari katika msitu huo ambao ni mkubwa na wenye kona nyingi, ghafla alikuta barabara imefungwa kwa magogo.
Alisema baada ya kuona hali hiyo alitambua kuwa kuna jambo la hatari na alipoanza kurudi nyuma ili kutafuta mwanya wa kugeuza gari kurudi walikotoka ili kuokoa maisha yake na aliowabeba walijikuta wameshazungukwa na watu hao.
Alisema akiwa kwenye harakati hizo, lilitokea kundi la watu kutoka ndani ya msitu huo wakiwa na mapanga na marungu na kuwaamuru waliokuwa ndani ya gari hilo kushuka.
Kajula alisema alijitahidi kupambana nao ili kuokoa maisha yao lakini ilishindikana na watu hao walianza kupiga gari hilo kwa mawe na kuvunja vioo vyote.
Alisema kutokana na mashambulizi hayo alilazimika kusimamisha gari na kuwaeleza maofisa hao washuke ili kujinusuru.
Alisema wakiwa wanashuka, watu hao walianza kuwashambulia kwa silaha hizo na katika harakati za kujiokoa alijeruhiwa kwa kukatwa mkono wa kulia na kichwani.
Alisema watu hao waliwaamuru kulala chini na kuwapekua na kuwapora vitu mbalimbali, ikiwamo simu na Sh. 175,000 taslimu.
Kajula alisema baada ya uporaji huo, watu hao walitoa magogo barabarani na kumlazimisha kuondoa gari ambalo aliendesha kwa mkono mmoja hadi Kituo cha Polisi Itaka kabla ya kwenda hospitali kwa matibabu.
Muuguzi Msaidizi wa Hospitali ya Mbozi, Tulakela Kilatu, alisema majeruhi wote walipokelewa katika hospitali hiyo juzi majira ya saa 9:00 usiku na kutibiwa kabla ya kuruhusiwa isipokuwa dereva huyo.

NIPASHE
Taasisi tano za serikali zimeisababishia serikali hasara ya Sh. bilioni 10 kwa kipindi cha miaka miwili.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) Prof. Mussa Juma Assad, ya mwaka 2013/14 inaonyesha uwapo wa mashaka makubwa juu ya uwezo wa taasisi hizo kuendelea kujiendesha endapo hatua za makusudi hazitachukuliwa na serikali katika kuzinusuru.
Taasisi hizo ni Taaisi ya teknolojia Dar es Salaam (DIT), Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB), Chama cha hakimiliki na Hakishirikishi Tanzania (COSOTA), Chuo Kikuu Huria (OUT) na TFC.
Aidha, CAG amebaini mapungufu katika mradi wa ujenzi wa jengo la ‘Linear Accelerator Treatment’ katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road wa Sh. Bil 3.333.
Taarifa hiyo imebainisha kuwa kwa mujibu wa mkataba huu, ujenzi ulitakiwa kumalizika ndani ya wiki 32, lakini hadi kufikia Disemba mwaka jana kazi pekee iliyokamilika ni maandalizi ya eneo la ujenzi.
“Kiasi cha fedha kilichokuwa kimelipwa kwa mujibu wa hati ya malipo kilikuwa Sh. milioni 349 ikijumuisha bima na malipo ya awali,” ilifafanua.
CAG alibainisha kuwa kwa mujibu wa Menejimenti ya Taasisi ya ORCI mkataba huo ulitekelezwa kwa kuzingatia bajeti iliyotengwa ya Sh. bilioni nane kutoka serikalini na hakuna kiasi chochote kilichokuwa kimepokelewa kwa kipindi cha mwaka wa fedha.

NIPASHE
Matukio ya kuvamia askari wakiwa lindoni, vituo na vizuizi vya polisi nchini yameendelea kulitafuna Jeshi la Polisi na safari hii, Askari wa Kikosi cha Tazara, Jijini Dar es Salaam, ameporwa SMG na kujeruhiwa vibaya.
Tukio hilo lilitokea juzi usiku saa sita kwa watu wanaosadikiwa ni majambazi wakiwa na silaha za jadi kumvamia askari huyo akiwa kwenye lindo la Tazara na kupora silaha hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka eneo la tukio, watu wawili wakiwa na silaha za jadi, nyakati za saa sita usiku walivamia eneo hilo na kupora silaha hiyo na kutokomea nayo.
Taarifa hizo zinafafanua kuwa askari huyo alijeruhiwa vibaya sehemu mbalimbali za mwili na amelazwa hospitali kwa matibabu zaidi, ingawa  jina lake halikutajwa wala hospitali aliyolazwa.
Kamanda wa Kikosi hicho, Kamanda Bieteo, alithibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kusema kuwa hawezi kutoa ufafanuzi kwa simu bali kwa taarifa ya maandishi.
“Tukio lipo ni kweli wamemvamia askari akiwa lindoni kumjeruhi na kumpora silaha…siwezi kutoa ufafanuzi zaidi kwa simu, leo nitatoa  taarifa kwa maandishi,”.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alipoulizwa, alithibitisha, lakini akamuelekeza mwandishi kuwasiliana na Kamanda Bieteo.
Hivi karibuni, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe, alisema idadi ya matukio ya uvamizi wa vituo vya polisi imeongezeka kutoka sita kwa mwaka 2014 hadi nane kwa mwaka 2015.
Alisema katika matukio hayo jumla ya askari saba waliuawa kwa mchanganuo kwenye mabano Chamazi (2), Mkuranga (2) na Ushirombo (3)

MTANZANIA
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, jana alijikuta katika wakati mgumu baada ya wabunge wengi kushutumu utendaji wake wakisema umekuwa chanzo cha wizara hiyo kuzorota katika maendeleo.
Kwa mujibu wa wabunge hao, kitendo cha waziri huyo kushindwa kutekeleza agizo la mahakama kuhusu tozo mpya katika hoteli za utalii kimefanya Serikali kupoteza zaidi ya Sh bilioni 20 kila mwaka.
Wabunge hao pia walishangazwa na kitendo cha wizara hiyo kulazimisha mfumo wa ‘Double Entry’ unaosababisha hasara badala ya mfumo wa ‘Single Entry’ unaotaka mtalii kulipa ada ya kiingilio kila anapoingia hifadhini.
Waliyasema hayo walipojadili makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2015/2016.
Akisoma maoni ya wabunge, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli alisema licha ya kamati yake kutoa ushauri na Bunge kutoa maagizo, waziri huyo amegoma kuyatekeleza.
Takwimu zinaonyesha kwa miezi 10 yaani Julai, 2014 hadi Machi, 2015 Hifadhi ya Serengeti na Hifadhi ya Ziwa Manyara zilipoteza zaidi ya Sh bilioni 1.4 kutokana na wizara kulazimisha mfumo wa ‘Double Entry’. Kamati inahoji kuna maslahi gani waziri kutetea mfumo ambao unaipotezea Serikali mapato?” alihoji Lembeli.
Lembeli alisema katika mkutano wa 18 wa Bunge, kamati ilishauri na Bunge likaazimia kwamba waziri huyo atekeleze hukumu ya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, iliyomtaka Nyalandu kutangaza katika gazeti la Serikali tozo mpya zitakazotumika katika hoteli za utalii nchini.
Akiwasilisha hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema) alisema kinachoonekana ni wizara hiyo kukosa dira kufikia malengo yake.
Msigwa alisema changamoto ambazo zipo ni sawa na zile za kamati ya bunge, hivyo ni wajibu wa waziri kuweka wazi kuwa ana maslahi gani na migogoro mingine ambayo imefikiwa mwafaka hata ile ya uamuzi wa mahakama.
Nashindwa kujua hivi hata hili la kuwa tumepoteza Sh bilioni 1.4 na Sh biloni 3 linakuwa gumu kufanyiwa uamuzi ni kwa maslahi ya nani au ndiyo mnajenga mazingira mazuri ya Ukawa kuchukua nchi,” alisema.
Awali, akiwasilisha bajeti yake, Waziri Nyalandu alisema wizara yake imejipanga kuhakikisha inatatua migogoro yote baina ya wananchi na maeneo yaliyohifadhiwa na kuhakikisha uhifadhi na matumizi endelevu ya maliasili kwa maendeleo ya utalii yanalindwa kwa ukamilifu kwa mujibu wa sheria.
Alisema katika kuhakikisha migogoro ya mipaka na uvamizi na maeneo yaliyohifadhiwa inakomeshwa, wizara itaendelea kurekebisha na kuweka alama za kudumu za mipaka na kufanya doria za mara kwa mara na kuelimisha umma.
Nyalandu alisema tayari ameipatia ufumbuzi wa kudumu migogoro mbalimbali ya ardhi ukiwamo ule wa Mbarali, ambao umedumu kwa miaka saba bila kupatiwa suluhisho.
Kwa mujibu wa Nyalandu, Tanzania inafuatiwa na Botswana, Kenya, Zambia, Afrika Kusini, Namibia, Uganda, na Zimbambwe.

MTANZANIA
Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, ametangaza rasmi kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Amesema kwa kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza rasmi kwa wanachama wake wenye sifa kujitokeza kuwania nafasi hiyo kubwa ya uongozi nchini, ameona hana budi kutangaza rasmi azma yake.
Dk. Magufuli, mmoja wa mawaziri ambao kwa muda mrefu wamehusishwa kwenye kinyang’anyiro cha nafasi hiyo, alisema anaingia kwenye mchuano huo akiwa na sifa zote stahiki za kupiga na kupigiwa kura.
Alitangaza azma yake nje ya ukumbi wa Bunge mjini Dodoma, muda mfupi baada ya kumalizika kipindi cha maswali na majibu bungeni, jana asubuhi.
Baada ya kuulizwa kama ana mpango huo, mara moja alisema: “Swali hili nimeulizwa mara nyingi. Mara zote nimekataa kulijibu kwa sababu chama chetu (CCM) kuna utaratibu wake wa namna ya kuomba nafasi ya uongozi. Muda ulikuwa haujawadia.
“Lakini utakumbuka wiki hii hapa hapa Dodoma, vikao vya juu vya chama chetu vimetoa ratiba kwa wanaotaka kuwania nafasi mbalimbali kujitokeza.
“Kwa maana hiyo sasa niko huru kujibu swali lako kwa kusema rasmi ‘nitagombea urais’. Nafanya hivyo kwa sababu naamini ninazo sifa za kuchagua na kuchaguliwa kama mwanachama wa CCM kwa nafasi yoyote inayojitokeza kulingana na Katiba ya chama chetu na pia Katiba ya nchi,”  Dk. Magufuli.
Alisema siku ya kuchukua fomu ataitangaza baadaye pindi akishakamilisha taratibu za namna ya kuanika hadharani mambo anayokusudia kuyatekeleza endapo wana CCM watampa ridhaa ya kupeperusha bendera ya chama hicho.
Dk. Magufuli, amekuwa mbunge tangu mwaka 1995. Baada ya kushinda ubunge mwaka huo, alichaguliwa kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi; Wizara iliyokuwa ikiongozwa na Anna Abdallah.

MWANANCHI
Wakati Serikali na wadau wa usafiri wakiendelea kutafuta mwarobaini wa ajali nchini, imeelezwa kuwa malori ya Tanzania yamesababisha ajali 227 nchini Zambia kati ya Januari na Mei.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa kwenye Gazeti la Lusaka Times la Zambia, imeelezwa kuwa Tanzania inatakiwa kutafuta suluhisho la kudumu la kudhibiti ajali zinazosababishwa na malori ya Tanzania wanayokwenda nchini humo.
Likikariri ripoti iliyotolewa na Kikosi cha Usalama Barabarani cha Zambia mwezi huu, gazeti hilo limesema katika ajali hizo 227, ajali 37 zilipoteza maisha ya watu 42.
“Kati ya ajali hizo waliopata majeraha makubwa walikuwa 51, wenye majeraha madogo walikuwa 59 huku ajali 133 zilisababisha uharibifu wa magari na mali,” inasema ripoti hiyo.
Ripoti hiyo ilitaja sababu kubwa ya ajali hizo kuwa ni mwendo kasi, vizuizi barabarani, uchovu wa safari ambao umekuwa ukisababisha baadhi ya madereva kuegesha malori yao vibaya na kusababisha madhara kwa watumiaji wengine wa barabara.
Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Usafirishaji na Usalama Barabarani (RTSA) Zambia, Zindaba Soko akizungumza katika mkutano uliomkutanisha na Mkurugenzi wa Usafirishaji kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini Tanzania (SUMATRA), Leo Ngowi mjini Ndola Zambia, alisema Serikali ya nchi hiyo itaondoa vikwazo barabarani ambavyo vimekuwa vikisababisha ajali.
Mkurugenzi huyo alisema iwapo nchi za Kusini mwa Afrika zitatekeleza utaratibu wa kuondoa urasimu utasaidia kupunguza muda wa kukaa mipakani, kupunguza gharama za kufanya biashara na kufanya safari nyingi kuliko ilivyo sasa kama pia watazingatia sheria za usalama barabarani.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Johansen Kahatano kutoka Kikosi cha Usalama Barabarani akizungumzia suala hilo alisema Polisi ilituma mwakilishi katika mkutano huo nchini Zambia ambapo walipata taarifa za ajali hizo.

MWANANCHI
Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad jana alichukua fomu ya kuomba kuteuliwa na chama hicho kugombea urais wa Zanzibar kwa mara ya tano huku akisema ushindi wake hautachezewa na mtu.

Mara ya kwanza Maalim Seif aliwania urais wa Zanzibar mwaka 1995 na amekuwa akifanya hivyo katika chaguzi zilizofuatia na sasa anawania tena kuingia Ikulu Oktoba.
Baada ya kuchukua fomu katika ofisi za chama hicho zilizopo Bububu jana, Maalim Seif alisema ataheshimu matokeo ya urais endapo uchaguzi utakuwa huru na wa haki.
Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, alisema matarajio yake makubwa katika uchaguzi ujao ni kwamba utafanyika katika mazingira ya amani na utulivu.

Alisema ni matumaini yake kwamba mara hii ataongoza na kuibuka kuwa rais endapo uchaguzi utakuwa huru na haki.
Kama wananchi wa Zanzibar watanipigia kura kwa wingi nawahakikishia hakuna mtu yeyote atakayechezea ushindi wangu,”  Maalim Seif.
Akizungumzia afya yake kuelekea Uchaguzi Mkuu, Maalim Seif alisema anagombea nafasi hiyo akiwa mzima wa afya na hana shaka, hivyo wananchi waondoe hofu katika hilo.
“Nachukua fomu ya urais na matarajio yangu makubwa ni kushinda katika uchaguzi mkuu ambao utafanyika katika mazingira ya amani,” alisema.
Hafla ya Maalim Seif kuchukua fomu ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwamo mawaziri katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa kutoka CUF. Maalim Seif aliwataka wanachama wengine kujitokeza kugombea nafasi hiyo kwa kuwa ni haki yao kikatiba.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...