Filbert
Rweyemamu
Arusha.Hatimaye
Kijiji cha kwanza kuanzishwa katika
mfumo wa Vijiji vya Ujamaa wakati wa awamu ya kwanza ya uongozi wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere cha
Upper Kitete,Kata ya Mbulumbulu wilayani Karatu kimepata umeme kupitia mradi wa Usambazaji umeme vijijini (Rea).
Akizindua
mradi huo Waziri wa Nishati na Madini,George Simbachawene alisema katika
awamu ya pili ya usambazaji umeme vijijini kiasi cha Sh 43 bilioni zitatumika
kwajili hiyo mkoani hapa, wakati wilaya ya Karatu itatumia Sh 11 bilioni .
Aliiagiza
Shirika
la Umeme nchini Tanesco kuwaelimisha wananchi kuona umuhimu wa
matumizi ya umeme kwenye nyumba na maeneo ya shughuli za kiuchumi
kwani bila hivyo fedha zilizotumika kwenye
mradi huo hazitakua na tija iliyokusudiwa .
“Umeme
utakua na tija kwa wilaya hii iwapo utatumika ipasavyo katika huduma za kijamii katika vituo vya
afya,shule,shughuli za kiuchumi zinazohitaji matumizi ya umeme na majumbani,”alisema
Simbachawene.
Awali Mkuu
wa wilaya ya Karatu Omari Kwaangw’ alisema usambazaji umeme vijijini utafungua
fursa za ajira kwa vijana kujiajiri katika shughuli mbalimbali za uzalishaji
mali na kuwafanya waishi maisha ya kisasa kama wananchi wengine nchini.
“Kijiji chetu
kina historia ya muda mrefu,kilikua ni kwanza kuanzishwa wakati wa vijiji vya
ujamaa miaka ya 60 tujipongeze kupata umeme ambao gharama yake naamini kila
mwananchi anaimudu ya Sh 27,000 tu baada ya mwezi Juni itapanda hadi 127,000 hivyo tumieni
fursa hii ipasavyo,”alisema Kwaangw’
Alisema
amekua akipokea barua za wananchi wanaotaka kuunganishwa na umeme hasa kwenye
maeneo ya kijamii kikiwemo Kituo cha afya katika Kata ya Baray ili kuwezesha
huduma za afya kupatikana muda wote.
Meneja wa
Tanesco Kanda ya Kaskazini,Ngerere Makoye akitoa taarifa ya mradi huo,alisema
zaidi ya wananchi 3,294 wanatarajiwa kuunganishiwa umeme katika vijiji mbalimbali
wilayani humo.
Hata hivyo
alisema moja ya changamoto ilikua ni gharama kuwa kubwa kutokana na umbali
kutoka Kijiji kimoja hadi kingine na mwitikio mdogo wa wananchi kuchangia gharama ya kiasi cha Sh 27,000 za
kuwekewa umeme majumbani mwao.
Mkazi wa Kijiji hicho,Stephano Ngaida alisema walikua wakitumia fedha zaidi kwaajili
ya kusaga nafaka kwa kutumia mashine zinazotumia Dizeli lakini wamepata unafuu
baada ya umeme wa gridi kufika Kijijini kwao huku Mwalimu Julius Sarwat
anayefundisha katika Chuo cha Ufundi Mbulumbulu alisema Chuo chao kitanufaika
kwa kuanzisha masomo ya Komputa na kufunga mashine za uchomeleaji.



إرسال تعليق