Waziri wa Kilimo,chakula na Ushirika Steven Wassira amesema kosa alilolifanya la kufunga vifungashio vya koti limempa umaarufu mkubwa kiasi cha kumpa Urais.
Waziri huyo amesema amefurahishwa na
kosa hilo kwani sasa imekuwa staili mpya ya uvaaji wa makoti kwa vijana
wa ndani na nje ya nchi.
Wasira alikiri kwamba siku hiyo alikosea
kuvaa koti kiasi kwamba vishinikizo vyake kupishana lakini hajutii kosa
hata kidogo kwani limempa umaarufu.
“Ile
picha niliyopigwa kwenye mitandao ya kijamii ikinionyesha nimekosea
kuvaa koti ni ya kweli wala si ya kutengeneza kwa ajili ya
kunichafua,baada ya muda nikaona vijana nao wanavaa kwa staili ile na
kujita Wassira Staili..imenipa umaarufu mkubwa sana” Wassira.
Alisema hata watu ambao walikuwa
hawamjui sasa wanamjua kupitia kosa hilo na kosa kama hilo pia
lilishawahi kufanywa na Rais wa Rwanda Paul Kagame hivyo si jambo la ajabu.
Aliongeza kuwa kosa lile lilitokana na
haraka aliyokuwa nayo kuwahi kwenye kazi za uwaziri hata mkewe hakuwepo
kuhakiki kama ametoka vizuri.
MWANANCHI
Rais Jakaya Kikwete amesema baadhi ya wakuu wa wilaya walitemwa kutokana na upungufu, ikiwa ni pamoja na madeni mitaani.
Rais alisema baadhi yao walikuwa wakienda baa wanalewa na ili kuwaondoa ilibidi wake zao waitwe kuwachukua.
Rais Kikwete alisema hayo jana mjini
Dodoma alipokuwa akifungua semina elekezi kwa wakuu wa wilaya 27 wapya
walioteuliwa hivi karibuni.
Februari 18 mwaka huu, Rais Kikwete alifanya mabadiliko ya wakuu wa wilaya na kutengua uteuzi wa wakuu wa wilaya 12.
Rais Kikwete alisema waliotemwa
walikuwapo wenye upungufu mbalimbali na wengine walikuwa na madeni
mitaani huku baadhi yao wakiwa na tatizo la ulevi kiasi kwamba wakienda
baa hulewa kupita kiasi.
Aliwaasa wakuu wa wilaya wapya kuwa wengine ni wadogo kiumri lazima wafanane na madaraka waliyopewa.
“Pale ulipo ni role model (mfano wa kuigwa), lazima uwe na tabia njema kwa kauli, matendo, nidhamu na uadilifu usiotiliwa shaka,” Kikwete.
MWANANCHI
Wakati Taifa likijiandaa kwa ajili ya
Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, yamebainika mambo matatu mazito ambayo
yanaliweka njiapanda , hali inayosababisha viongozi na hata wananchi
kubaki na maswali lukuki wakihoji hatma ya nchi yao.
Mambo hayo ambayo hadi sasa hayajulikani
hatma yake ni Katiba Inayopendekezwa, Mahakama ya Kadhi na uboreshaji
wa Daftari la Wapigakura kwa vifaa vya kielektroniki vya Biometric Voter Registration (BVR).
Mambo hayo yamekuwa mjadala wa kitaifa
kwa muda sasa, hoja kubwa ikiwa ni endapo matukio makubwa ya kitaifa –
upigaji wa kura ya maoni kupitisha Katiba Mpya na Uchaguzi Mkuu wa
Oktoba yatafanyika kwa mafanikio au yanaweza kukwama na kusababisha
sintofahamu.
Hoja kubwa katika eneo hili imekuwa ni
iwapo kura ya maoni ya kupitisha Katiba itafanyika Aprili 30, mwaka huu
kama ilivyopangwa, lakini Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva mara kadhaa amesimamia msimamo wa Serikali kuwa uandikishaji unaendelea bila matatizo katika Mkoa wa Njombe kama ilivyopangwa.
Ukiacha upungufu unaosababisha shughuli
hiyo kuchukua muda mrefu, Jaji Lubuva amekuwa akikwepa kuzungumzia madai
kuwa Serikali haikutoa fedha za kutosha kufanikisha shughuli hiyo,
lakini juzi alikiri kuwa Tume yake ilijaribu hata kuazima vifaa hivyo
Kenya na Nigeria bila mafanikio.
Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba
amekaririwa na gazeti hili jana akisema hata bajeti ya mchakato huo ya
Sh297 bilioni iliyopangwa haipo kwa kuwa katika kasma ya tume zilikutwa
Sh7.01 bilioni na fedha za maendeleo na fedha za tume hazikuonekana.
Profesa Lipumba alisema pia hata Sh144
bilioni za kura ya maoni zilizoelezwa na Tume hazikuonekana kwenye
vitabu vya bajeti na kuwa BVR 250 zilizopo badala ya 8,000
zilizokusudiwa haziwezi kufua dafu.
Kuhusu muda uliosalia wa siku 42 kabla
ya kura ya maoni, umeelezwa na wachambuzi kuwa hautoishi, ukilinganishwa
na Kenya iliyokuwa na BVR 15,000 na ikaandikisha wapiga kura milioni 14
kwa siku kati ya 45 hadi 60.
Kutokana na hali hiyo, kinachosubiriwa
na wananchi ni ama kuelezwa ni muujiza gani utafanyika hadi shughuli
hiyo kukamilika na kura ya maoni kupigwa bila matatizo au kuahirisha
kura hiyo hadi wakati au baada ya uchaguzi mkuu.
Saula jipya kabisa katika mjadala wa
uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi inayotambuliwa na Serikali ni kesi
iliyofunguliwa Mahakama Kuu na Mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila akitaka mahakama itamke kuwa Mahakama ya Kadhi na masuala ya Jumuiya ya Kiislamu (OIC) ni haramu na itamke kuwa ulinzi na uhai na utu wa binadamu nchini hauwezi kubaguliwa na Uislamu.
MTANZANIA
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ameibua ufujaji wa mabilioni ya fedha kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Katika ripoti ya ukaguzi wa CAG kwa
vyama hivyo aliyoikamilisha Septemba mwaka jana kwa mujibu wa sheria ya
vyama vya siasa namba tano ya mwaka 1992, sehemu ya 14 (1)(b) imeibua
madudu hayo.
Taarifa hiyo ya CAG imechambua hesabu za
Chadema na CCM na kusema wakati wa ukaguzi walibaini masuala mengi
ikiwamo kutotolewa taarifa sahihi za matumizi.
Kutokana na hali hiyo, CAG alilazimika
kutoa hati yenye shaka kwa chama tawala – CCM ambacho kilionyesha
kumiliki mali za kiasi cha Sh bilioni 19.5.
Hata hivyo, imebainika kuwa CCM haina
daftari la mali za kudumu, ambalo lingeweza kubainisha ukamilifu wa
taarifa kuhusu umiliki huo wa fedha za chama hicho.
CAG alisema chama hicho hakikufanya tathmini ya mali zake kwa kipindi kirefu, hivyo, fedha hizo haziwakilishi thamani halisi.
Alisema chama hakikutenganisha thamani
ya ardhi na majengo badala yake kikieleza kuwa na thamani ya Sh bilioni
11.4 ambapo alishindwa kubainisha kwa kutenganisha thamani za ardhi na
zile za majengo kama kinavyoagiza kifungu cha 58 cha viwango vya uhasibu
vya kimataifa (IAS) 16.
“Hatukuweza kupata taarifa za ukaguzi
zinazounga mkono uwekezaji wa CCM ulioelezwa kuwa na thamani ya Sh
bilioni 9.6 ambao umejumuishwa katika hali ya taarifa ya kifedha
iliyoishia Juni 30, 2013 zilizoelezwa katika vipengele 6 na 7 vya
taarifa za fedha.
MTANZANIA
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu jana alionekana kumpiga kijembe Katibu MKuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana aliposema kuwa sasa atakuwa anazurura angani.
Nyalandu alitoa kauli hiyo Dar es Salaam alipozindua ndege nyepesi (Micro-Light, 5H – Hel), ambayo itatumika kupambana na ujangili katika Hifadhi ya Taifa ya Selous.
“Karibuni
wote, leo tunazururia hapa uwanja wa ndege na ninazindua ndege hii
nyepesi ambayo imetengenezwa Ufaransa, itatumika kupambana na majangili
katika Mbuga ya Selous.
“Kwa
maana hiyo sasa tunaanza kuzururia angani kupambana na majangili na
nasisitiza kwamba ndege hii ni mpya kabisa na gharama za uendeshaji wake
ni ndogo kwa vile inatumia petroli,” alisema.
Hivi karibuni Kinana akiwa ziarani mkoani Arusha alimsifia Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa (CCM) kuwa ni mchapakazi lakini Waziri Nyalandu ni mzururaji.
Akizungumza jana wakati wa uzinduzi wa
ndege hiyo ya kupambana na ujangili, Nyalandu alisema imetengenezwa kwa
gharama ya Dola za Marekani 2,040,000 na ina uwezo wa kubeba askari
mmoja na rubani.
Waziri Nyalandu alisema ndege hiyo
imeundwa kwa usalama wa hali ya juu kwa kuwekewa puto (parachute) ambalo
litatumika kushuka chini iwapo ndege itaishiwa mafuta angani.
“Itakapoanza
kutumika itasaidia kuwabaini majangili, inakwenda kwa mwendo mdogo
iwapo angani hali ambayo inawezesha kuwaona majangili na kila
kinachoendelea ardhini kwa wepesi,” Nyalandu.
MTANZANIA
Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Cecilia Mosha aliyejirusha
kutoka ghorofa ya tatu hadi chini kutokana na hofu ya moto uliotokea
katika Hosteli ya Mabibo, amevunjika mfupa wa bega.
Mwanafunzi huyo alijirusha kupitia
dirishani juzi katika harakati za kujiokoa na moto baada ya jengo la
wasichana, Block A kushika moto huku wanafunzi wakiwa vyumbani
wakiendelea na shughuli zao.
Cecilia ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa
pili wa Shahada ya Uhandisi wa Uchimbaji Madini, alisema alisikia
kelele akiwa chumbani na alipotoka nje akakuta moshi umetanda kila kona.
“Baada ya kuona hivyo niliona ni vema nijiokoe kwa kujirusha kutoka ghorofa ya tatu ya bweni hilo hadi chini kupitia dirishani,”Mosha.
Alisema baada ya kuruka hadi chini
alikimbizwa katika kituo kidogo cha afya karibu na hosteli hiyo ambako
alipoteza fahamu na kushtukia yupo katika Taasisi ya Mifupa na Mishipa
ya Fahamu Muhimbili (MOI).
Naye Meneja Ustawi na Uhusiano wa Taasisi ya MOI, Almasi Jumaa alisema hali ya Cecilia si mbaya na anaendelea na matibabu.
“Tumempokea
huyo mgonjwa jana na baada ya timu ya madaktari kumfanyia vipimo vya
kutosha wamebaini amevunjika mfupa wa bega la kulia na kupata mshtuko wa
mwili … alipata maumivu ya kiuno na mwili kwa ujumla,” alisema Jumaa.
Ajali hiyo ya moto ilitokea juzi katika Hosteli ya Mabibo iliyopo Mtaa wa Ubungo Kibangu, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam, Profesa Rwekaza Mukandala moto huo uliteketeza
ghorofa ya tatu ya jengo A linalotumiwa na wanafunzi wa kike.
HABARILEO
KATIBU Mkuu wa Umoja wa Mataifa(UN), Ban Kimoon amemteua Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman kuongoza Timu Huru ya Wataalamu kuchunguza kifo kilichotokana na ajali ya ndege cha aliyekuwa Katibu Mkuu wa UN, Dag Hammarskjöld na ujumbe wake Septemba 18, 1961 katika Jamhuri ya Kongo.
Taarifa iliyotolewa na UN jijini Dar es Salaam juzi imewataja wajumbe wengine wa timu hiyo kuwa ni pamoja na Kerryn Macaulay, raia wa Australia na Henrik Larsen wa Denmark.
Kuundwa kwa timu hiyo kwa mujibu wa
taarifa hiyo kunatokana na azimio namba 69/246 la Baraza Kuu la Umoja wa
Mataifa lilitolewa Desemba 29, mwaka jana lililomwomba Katibu Mkuu,
kuunda timu huru ya kuchunguza na kutathmini kifo cha Hammarskjöld na
ujumbe wake walipokuwa katika harakati za kuleta amani nchini Congo.
Baraza hilo kwa mujibu wa taarifa hiyo
pia lilizitaka nchi wanachama wa UN kutoa kumbukumbu zozote muhimu
walizonazo kuhusu na kifo hicho cha Hammarskjöld.
Taarifa imefafanua kwamba timu hiyo ya
wataalamu itaanza kazi yake rasmi Machi 30, mwaka huu na kukabidhi
ripoti yake kwa Katibu Mkuu wa UN si zaidi ya Juni 30, mwaka huu.
Dag Hammarskjöld, raia wa Sweden alikuwa
Katibu Mkuu wa pili wa UN kati ya Aprili 10, 1953 na Septemba 18, 1961
alipokufa katika ajali ya ndege nchini Congo pamoja
HABARILEO
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
imekamata bidhaa za magendo zenye thamani ya Sh milioni 228.4, ikiwa ni
katika jitihada za kudhibiti uingizaji wa bidhaa kwa njia ya magendo na
biashara ya magendo nchini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na
Idara ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi, bidhaa hizo zimekamatwa ndani ya
miezi mitatu tangu Januari hadi Machi katika mikoa minne pekee.
Bidhaa hizo zimekamatwa katika mikoa ya
Arusha, Kagera, Morogoro na Tanga katika operesheni inayoendeshwa kwa
ushirikiano kati ya TRA na Jeshi la Polisi nchini.
Taarifa hiyo imefafanua zaidi kuwa, kwa
upande wa Mkoa wa Kagera, viroba 675 vilivyosheheni katoni 2,043 za
pombe aina ya Signature Vodka kutoka Uganda ambazo ni sawa na lita
24,516 yenye thamani ya zaidi ya sh milioni 61.3 zilikamatwa kwenye
jahazi.
Kwa upande wa Mkoa wa Morogoro, taarifa
hiyo inabainisha kuwa madumu 1599 ya lita 20 za mafuta ya kupikia yenye
thamani ya zaidi ya Sh milioni 65.9 yalikamatwa eneo la Bwawani yakiwa
katika malori mawili yaliyokuwa yakitokea Bagamoyo kwenda Morogoro.
Taarifa hiyo inasema pia TRA wamekamata
madumu 888 ya lita 20 za mafuta ya kupikia yenye thamani ya zaidi ya Sh
milioni 15.8 yalikamatwa eneo la Kwame katika bandari bubu wilayani
Mkinga, mkoani Tanga.
Taarifa hiyo inabainisha kuwa kwa
kutumia taarifa kutoka kwa wasamaria wema, TRA imekamata jumla ya madumu
75 ya mafuta ya taa yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 2.9 mkoani
Arusha yakiwa yamepakiwa katika gari aina ya Toyota hiace yakisafirishwa
kutoka Holili kwenda Moshi kwa magendo.
NIPASHE
Wakati Tanzania ikitajwa kuwa kichochoro
cha kupitishia dawa za kulevya, wabunge wamehoji dawa hizo
zinazokamatwa kama ushahidi zimekuwa zikipelekwa wapi kwa kuwa
haionyeshi kama zimekuwa zikichomwa moto au la hali inayotia shaka
udhibiti wa biashara hiyo.
Mbunge wa Viti Maalum, Rukia Ahmed,
akiuliza swali la nyongeza jana bungeni, alisema kumekuwa na
ucheleweshaji wa kesi za dawa za kulevya licha ya mtuhumiwa kukutwa na
dawa hizo tumboni na pia zilizokamatwa haionyeshi zinapelekwa wapi.
Alisema kesi nyingi za mauaji na dawa za
kulevya zinachukua muda mrefu kumalizika mahakamani na kusababisha
watuhumiwa kukaa zaidi ya miaka saba rumande na kuhoji kwa nini muda
wanaokaa rumande usijumuishwe kama sehemu ya hukumu wanapotiwa hatiani.
Mbunge wa Karagwe (CCM), Gosbert Blandess,
alihoji lini serikali itaanzisha mahakama maalum kwa ajili ya
kushughulikia kesi za dawa za kulevya na rushwa kama njia ya kudhibiti
tatizo hilo.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Ummy Mwalimu,
alisema mahakama inaendeshwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu
za nchi, hivyo suala la hukumu pamoja na kipindi cha mshtakiwa kutumikia
kifungo chake hufanyika kulingana na sheria inavyotamka kuhusu adhabu
ya kosa husika.
Kuhusu zinapopelekwa dawa za kulevya
zinazokamatwa, alisema kiutaratibu vidhibiti havirudishwi na hukumu
ikishatolewa vinateketezwa.
NIPASHE
Wakati Spika wa Bunge, Anne Makinda, akisema hawezi kumtangaza Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, kuwa siyo mbunge hadi atakapopata barua ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, amesema bado hawajaandika barua kuiarifu Nec, kwa kuwa hilo siyo jambo kubwa ambalo chama kinapaswa kuhangaika nalo kwa sasa.
Spika Makinda aliwaambia waandishi wa
habari nje ya viwanja vya Bunge mjini Dodoma jana kuwa ofisi yake
haiwezi kufanyia kazi taarifa za kwenye vyombo vya habari, badala yake
inasubiri taarifa za kiofisi kutoka Nec.
“Hatuwezi
kutangaza sasa kwa sababu hatujapata barua. Tumesikia kwenye vyombo vya
habari tu. Kwa hiyo hadi hapo tutakapopata barua ya Nec ndipo
tutakapotangaza,” Spika Makinda.
Hata hivyo, alisema kwa mujibu wa sheria, chama kikimvua mbunge uanachama anapoteza ubunge wake.
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu,
alisema hana taarifa kama barua ya taarifa ya kumvua Zitto uanachama
imekwishaandikwa kwa Nec au la kwa kuwa Ofisi ya Katibu Mkuu wa chama
hicho ndiyo inahusika kuiandika.
Dk. Slaa alisema hatua ya kuandika barua
hiyo itafuatia baada ya kikao cha Kamati Kuu ya Chama kuitishwa na
kufanyika. Hata hivyo, alisema suala la kuitisha kikao hicho linahitaji
mchakato na kwamba hivi sasa kuna vitu vikubwa na vyenye athari kubwa
kwa umma na siyo suala la uanachama wa Zitto ndani ya Chadema.
Alitaja vitu ambavyo Chama kinahangaika navyo kwa sasa kuwa ni pamoja na Daftari la Kudumu la Wapigakura.
“Sidhani kama waandishi wa habari mnahangaika nalo hilo, kama mnavyohangaika na suala hilo la uanachama wa Zitto,” Dk. Slaa.
Kitu kingine ambacho alikitaja kuwa ni
katika vitu wanavyohangaika navyo kwa sasa kuwa ni mamilioni ya shilingi
‘yanayoteketea’ kwa ajili ya kuandaa sherehe za ‘Wiki ya Maji.’
“Hatujaandika hiyo barua, tutaandika ratiba yetu ikituruhusu,” Dk. Slaa.
Zitto alitangazwa kupoteza uanachama
katika chama hicho wiki iliyopita baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania
Kanda ya Dar es Salaam kutupilia mbali kesi yake dhidi ya Chadema
iliyokuwa ikihoji uhalali wa uanachama wake ndani ya chama hicho.
No comments:
Post a Comment