SAKATA baina ya Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu na Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Singida Vijijini limechukua sura mpya baada ya kikao cha Baraza la Jumuiya hiyo kuazimia kuitisha mkutano mkuu ili kumjadili.
Mwenyekiti wa UVCCM Singida Vijijini, Shaban Mang’ola alisema kuwa Baraza limelazimika kuchukua hatua hiyo baada ya Mbunge Nyalandu kukaidi kwenda kuonana na vijana hao kama ambavyo iliamuliwa afanye ndani ya muda wa siku 14 tangu Desemba 23 mwaka jana kutokana na tuhuma mbalimbali zinazomkabili.
Aidha, jumuiya hiyo imeazimia kumvua heshima mbunge huyo kwa kususa kushiriki shughuli zake zote atakazoendesha jimboni humo, likiwemo suala la kumvisha skafu.
Kikao cha Baraza hilo kilichofanyika Desemba 23 mwaka jana, kilidai kuwa ahadi hewa za mbunge Nyalandu ndizo zilizochangia kuikosesha CCM ushindi katika baadhi ya maeneo wakati wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana.
Katika uchaguzi huo, kati ya vijiji 84 vilivyopo kwenye jimbo hilo, vijiji vinane vilichukuliwa na upinzani na vitongoji 49 kati ya 436 vilichukuliwa na upinzani tofauti na uchaguzi wa mwaka 2009 ambapo upinzani ulipata vijiji viwili tu katika wilaya hiyo bila kupata hata kitongoji kimoja.
Hata hivyo, mbunge huyo amekuwa akisisitiza kuwa hizo ni fitina tu za kisiasa na kwamba kiwango hicho kidogo cha ushindi kwa wapinzani si sababu ya kutosha ya kuanza kumshutumu yeye kuwa ndio chanzo.
Nyalandu alisisitiza hivi karibuni wakati akitangaza kugombea urais alisema amefanya kazi kubwa jimboni mwake, hali inayompa hamasa ya kuona anafaa kuwa rais wa nchi.
Alisema kwa kipindi cha miaka 15 ambayo amekuwa mbunge wa jimbo la Singida Kaskazini ametumia muda wake na Sh bilioni 2 katika kufanikisha kuchangia miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali zikiwemo za afya, maji na barabara.
Katibu wa CCM Wilaya ya Singida Vijijini, Mwamvua Quilo alikanusha madai hayo ya UVCCM na kueleza kuwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliomalizika karibuni, CCM ilipata ushindi wa asilimia 91.9 katika jimbo hilo na kupoteza vijiji vinane baada ya Chadema na CUF kubuika na ushindi.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa ni uongo kwamba Nyalandu ndiye alichangia wanyang’anywe viti hivyo na vyama hivyo vya upinzani.
“Kampeni tumefanya viongozi wote wa CCM wilaya tulishiriki na kupata ushindi huo mkubwa, hivyo hao wapinzani wa Nyalandu kisiasa wanaozunguka kupotosha alisababisha tukapoteza vijiji vinane siyo wa kweli…mbona kwenye majimbo mengine tumepoteza viti vingi sana lakini hawasemi,” alisema Quilo.
UVCCM katika madai yake wanadai kuwa Nyalandu ambaye pia ni Waziri wa Maliasili na Utalii anatuhumiwa kumtuma mkewe jimboni humo kuhamasisha na kuahidi vijana zaidi ya 9,000 wa jimbo hilo kuwapatia mikopo, ahadi ambayo haijatekelezwa hadi hivi leo.
Ili kupewa mkopo huo, ilidaiwa kuwa kila mmoja alilazimika kulipa Sh 8,000 ikiwa ni kiingilio na usajili wa kwenye kikundi.
Nyalandu pia anadaiwa kuitisha ligi ya mpira wa miguu kwa kata zote za jimbo hilo na kuahidi kuwapatia washindi zawadi, lakini kwa mshangao mkubwa baada ya ligi kumalizika alikataa kata kata kuhusika na ligi hiyo; hivyo kuwatia hasara washiriki waliojigharamia.
Kadhalika, mbunge huyo anadaiwa kuwatukana hadharani baadhi ya wapiga kura wake, akiwemo Mwenyekiti mstaafu wa halmashauri ya wilaya ya Singida, jambo ambalo baraza hilo lilisema ni cha dharau kwa jumuiya ya umoja huo.
Kutokana na sababu hizo, Baraza hilo lilimtaka aende kukutana na Jumuiya hiyo ili kutoa maelezo ya kuridhisha juu ya mustakabali wa ahadi zake na tabia yake ya kuwatusi baadhi ya wapiga kura wake hadharani.
Siku chache baadae, mbunge huyo ambaye mwishoni mwa mwaka jana alitangaza azma yake ya kuwania kugombea nafasi ya Urais, alilazimisha kuitishwa Kikao cha Kamati ya Siasa ya Wilaya kwa lengo la kumwadabisha Mwenyekiti wa UVCCM Singida Vijijini; jambo ambalo halikuwezekana.
Kikao cha juzi kilisema kuwa mbunge huyo hajatekeleza hata agizo moja lililotolewa kwenye kikao cha Desemba 23 mwaka jana cha Baraza hilo badala yake ameendeleza kauli zake za matusi, dharau na kejeli dhidi ya Jumuiya hiyo akisema vijana hao wanasumbuliwa na njaa na akataka walaaniwe na waende motoni.HABARILEO
No comments:
Post a Comment