Katibu
Mkuu Mstaafu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Fanuel Mbonde akijaribu
baiskeli ya mazoezi aliyokabiodhiwa kama zawadi katika hafla ya
kuwapongeza watumishi wa Wizara waliostaafu iliyofanyika mwishoni mwa
wiki jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Naibu Waziri wa Katiba na Sheria
Mhe. Angellah Kairuki na kulia ni Katibu Mkuu Bi. Maimuna Tarishi.
Naibu
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Angellah Kairuki (kushoto) akimkabidhi
zawadi Mtunza Kumbukumbu Mstaafu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Clara
Mlamlyingu katika hafla ya kuwapongeza watumishi wa Wizara waliostaafu
iliyofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam. Kushoto kwa Bi.
Mlamlyingu ni Katibu Mkuu Bi. Maimuna Tarishi na kulia ni Jaji Dkt.
Gerrald Ndika, Mkuu wa Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo
Tanzania.
Watumishi
Wastaafu wa Wizara ya Katiba na Sheria wakiwa na vyeti vyao katika
picha ya kumbukumbu na viongozi wa Wizara wakiongozwa na Naibu Waziri
Mhe. Angellah Kairuki na Katibu Mkuu Bi. Maimuna Tarishi. Hafla ya
kuwapongeza ilifanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.
Katibu
Mkuu Mstaafu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Fanuel Mbonde
akikabidhiwa cheti na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria katika hafla ya
kuwapongeza watumishi waliostaafu iliyofanyika mwishoni mwa wiki jijini
Dar es Salaam. Kushoto kwa Katibu Mkuu Mstaafu ni Katibu Mkuu Bi.
Maimuna Tarishi.
Baadhi
ya watumishi wa Wizara ya Katiba na Sheria wakisakata rhumba katika
hafla ya kuwapongeza Watumishi waliostaafu iliyofanyika jijini Dar es
Salaam mwishoni mwa wiki. (Picha: Wizara ya Katiba na Sheria).
Na Mwandishi Wetu
Watumishi
wa Wizara ya Katiba na Sheria wakumbushwa kuwa chachu ya mabadiliko
katika utumishi wa umma na kuondokana na utendaji kazi wa mazoea kwa
kila mtumishi kufanya kazi kwa malengo yenye kutoa matokeo yanayopimika.
Akizungumza
katika hafla ya kuwaaga watumishi waliostaafu katika Wizara hiyo
iliyofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa
Katiba na Sheria Mhe. Angellah Kairuki amesema utendaji kazi wenye
kujali matokeo unawezekana na kuwataka watumishi wote kubadilika
kimtazamo na kifikra ili kufikia lengo hilo.
Watumishi
waliostaafu na kuagwa katika hafla hiyo ni Bw. Fanuel Mbonde aliyekuwa
Katibu Mkuu. Bi. Christina Sonyi (Mkurugenzi wa Sera na Mipango), Bi.
Anna Mayawalla (Mkurugenzi Msaidizi – Sera), Bi. Mariam Mwaisabila
(Mtunza Kumbukumbu Mkuu Msaidizi), Bi. Giditha Peter (Mwendeshaji Mkuu
wa Mifumo ya Kompyuta) na Bi. Clara Mlamyingu aliyekuwa Mtunza
Kumbukumbu Mkuu Msaidizi.
Akifafanua,
Naibu Waziri Kairuki amesema ni muhimu kwa watumishi wote kujenga
uelewa wa pamoja wa majukumu ya Wizara ya kupanga mkakati wa
kuyatekeleza kwa ushirikiano.
“Hatuna
budi kujenga uelewa wa pamoja wa majukumu tuliyonayo katika Wizara yetu
na kujenga ushirikiano wa hali ya juu. Tunapaswa kuondokana na utendaji
kazi wa mazoea, lazima ukome sasa. Kila mmoja wetu kwa nafasi yake
anapaswa kufanya kazi kwa malengo yenye kutoa matokeo,” amesema Kairuki
katika hafla iliyohudhuriwa na Katibu Mkuu Bi. Maimuna Tarishi, wastaafu
na watumishi wengine wa Wizara hiyo na wawakilishi wa taasisi zilizo
chini ya Wizara.
Kuhusu
watumishi waliostaafu, Naibu Waziri Kairuki amesema watumishi wote
waliostaafu wanapaswa kupongezwa na kutimiza wajibu wao kwa uadilifu,
umoja na ushirikiano hadi kufikia hatua ya kustaafu kwa mujibu wa
sheria.
“Katibu
Mkuu alitufanya sote kujisikia kama timu moja iliyolenga kutekeleza
majukumu ya Wizara kwa ufanisi huku ikizingatia maslahi ya watumishi.
Kipekee, ninamshukuru sana kwa uongozi wake katika Wizara hii ambao
umeweka misingi ambayo sisi viongozi tuliopo tunaisimamia, tunaiendeleza
na kuiboresha,” alisema Naibu Waziri Kairuki na kuongeza:
“Katibu
Mkuu huwa hafanyi kazi peke yake. Ana Timu. Nyie wote kwa umoja wenu
ndiyo timu yake. Na kama mnavyofahamu, mchezaji mmoja akiwa mzembe basi
timu yote inaathirika. Kwa msingi huo, Ndugu Mbonde alikuwa na timu
ambayo baadhi ya wachezaji wake ni wastaafu tunaowaaga leo na sisi
tunaoendelea na utumishi,” aliongeza Mhe. Kairuki.
Aidha,
Naibu Waziri Kairuki alitumia hafla hiyo kuwakumbusha watumishi kuhusu
masuala mbalimbali ya kitaifa likiwemo la kushiriki katika Kura ya Maoni
kuhusu Katiba Inayopendekezwa na mapambano dhidi ya UKIMWI.
“Sisi
kama watumishi wa Wizara yenye dhamana ya mambo ya Katiba na Sheria,
tunapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuisoma, kuielewa na hatimaye
kushiriki katika kupigia Kura ya Maoni Katiba Inayopendekezwa ifikapo
tarehe 30 Aprili mwakani (2015)” alisema na kuongeza watumishi wa Wizara
wanapaswa kuwa waangalifu na kujikinga na maambuikizi ya virusi vya
UKIMWI.
“Sote
tunajua jinsi janga hili linavyoathiri nguvu-kazi ya taifa na hata
familia zetu. Sidhani kama kuna mtu kati yetu ambaye hajaguswa na tatizo
hili. Wito wangu ni kuwa waangalifu na kujikinga na maambukizi. Kwa
wale wanaoishi na virusi, Serikali itaendelea kuwahudumia kwa mujibu wa
miongozo iliyopo,” alifafanua.
Akizungumza
kwa niaba ya Wastaafu, Katibu Mkuu Mstaafu Mbonde aliwashukuru
watumishi wa Wizara kwa kutambua mchango wake na watumishi wastaafu
wengine na kuahidi kutoa ushirikiano pale utakapohitajika.
“Sisi
tupo na ujuzi wetu, wakati wowote mtakapoona mnatuhitaji tuwasiliane na
tupo tayari kutoa mchango wetu ili kufanikisha majukumu ya Wizara,”
alisema Bw. Mbonde.
Kuhusu
maadili, Katibu Mkuu huyo Mstaafu aliwakumbusha watumishi kuzingatia
maadili na kuepuka vitendo vya rushwa ili kulinda heshima ya Wizara na
utumishi wa umma.

Post a Comment