Tunapoelekea
kipindi hiki cha sikukuu za Krismas na mwaka mpya, wananchi wenye imani
ya Kikristo na hata madhehebu mengine hutumia muda huo kwenda kuabudu
pamoja na muendelezo wa sherehe hizo kwenye maeneo mbalimbali ya starehe
ambapo uzoefu unaonyesha baadhi ya watu hupenda kutumia fursa hiyo
kufanya vitendo vya uhalifu hasa wa kujipatia vipato na mali.Kufuatia
hali hiyo, Jeshi la Polisi nchini, katika mikoa yote limejipanga vizuri
kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuhakikisha
kwamba hakuna vitendo vyovyote vya uhalifu vitakavyojitokeza kipindi
hiki cha sikukuu na pale ambapo vitajitokeza vitadhibitiwa kwa haraka.
Ulinzi umeimarishwa kwenye maeneo yote ya kuabudia, fukwe za bahari,
sehemu za starehe na maeneo mengine yote ambayo yatakuwa na mikusanyiko
mikubwa ya watu. Hata hivyo, watu wote watakaoenda maeneo ya beach
wanatakiwa kuwa makini ili kuepuka kuzama kwenye maji.
Aidha,
tunawakumbusha wananchi kuwa makini katika suala zima la usalama wa
maisha na mali zao, hususani kuchukua hatua stahiki na za haraka kwa
kutoa taarifa pindi wanapoona viashiria vyovyote vya uhalifu katika
maeneo yao na sehemu mbalimbali za biashara, na watokapo kwenye makazi
yao wasiache nyumba wazi ama bila mtu na pale inapobidi watoe taarifa
kwa majirani zao. Wazazi wanakumbushwa kuwa makini na watoto kwa
kutokuwaacha watembee peke yao, ili kuepuka ajali na matukio mengine
yanayoweza kusababisha madhara juu yao ikiwemo kupotea. Aidha, wazazi
waepuke kuwapeleka watoto kwenye kumbi za disko toto ambazo siyo salama.
Vilevile,
wamiliki wa kumbi za starehe wazingatie usalama katika kumbi zao,
hawarusiwi kujaza watu kupita kiasi kwenye kumbi hizo, hususani kumbi za
disko toto. Aidha, wamiliki wa kumbi za starehe na maeneo mengine yenye
mikusanyiko mikubwa ya watu wanakumbushwa kufunga vifaa maalum vya
kufuatilia mienendo ya watu wanoingia na kutoka katika maeneo hayo (CCTV
kamera).
Pia,
Jeshi la Polisi linawatahadharisha wale wote ambao watakuwa wakitumia
barabara, kuwa makini na kuzingatia sheria za usalama barabarani na hasa
kwa madereva wa magari na pikipiki, kuepuka kwenda mwendo kasi na
kutumia vilevi wawapo kazini.
Mwisho,
tunawaomba wananchi waendelee kutoa taarifa za mipango yoyote ya
uhalifu watakayoiona ikiendelea mahali popote kwa kuwafichua wahalifu
hao ili hatua za kuzuia uhalifu huo ziweze kuchukuliwa mapema. Taarifa
zinaweza kutolewa kupitia namba ya simu 0754 78 55 57 au Simu za
Makamanda wa Polisi wa mikoa au katika kituo chochote cha Polisi.

Post a Comment