Filbert Rweyemamu Arusha.
Meneja wa Shirika la Viwanda
vidogo (Sido)mkoa wa Arusha,Isdore Kiyenze amesema tabia ya uvivu na woga wa
kuchukua hatua waliyonayo wananchi wengi imekua kikwazo cha kujiletea maendeleo.
Akizungumza
kwenye mahojiano maalum na blog hii ofisini kwake eneo la Gereji Unga Limited ,amesema
fursa za kuwatoa katika hali ya umasikini zipo nyingi ila wananchi
wengi hawapendi kujishughulisha ili kufikia malengo wanayoyataka.
“Watu wengi ukiwauliza kwanini sio
wajasiriamali watakwambia hawana mitaji,na ukiwauliza wameshafika kwenye
taasisi ngapi za fedha kufatilia mikopo,
majibu yao ni kuwa hawakopesheki bila hata kwenda kuwaona maafisa wa mikopo,”alisema
Kiyenze
Amesema tabia hiyo imesababisha fursa
nyingi za kujiendeleza kuchukuliwa na wageni,huku wananchi wakibaki kuwa
watazamaji na kulalamikia ugumu wa maisha ambao hauondolewi kwa kukaa vijiweni
bali ni kuacha uvivu wa kufikiri na kuchukua hatua za ujasiri.
Kiyenze amesema katika kuwawezesha
wananchi Sido imekua ikitoa mafunzo ya ujasiriamali kwa wananchi mbalimbali na
kuanzisha Umoja wa wasindikaji Vyakula nchini(Tafova)ili kuwawezesha
kuunganisha nguvu zao kupata mashine za kutengeneza vifungashio.
“Sekta ya Vyakula hatujaifanyia kazi
ipasavyo,kwa muda mrefu tumekua tukiuza mali ghafi jambo ambalo halina tija
sana kwetu,jambo la msingi ni kusindika
bidhaa za vyakula ili kuongeza thamani na kipato,”alisema
Ameongeza kuwa changamoto ambayo
imekua ikiwakabili wajasiriamali nchini kukosekana vifungashio vyenye ubora wa
kumvutia mnunuzi na kwamba umoja walioanzisha utawawezesha kuanza kutengeneza
vifungashio ambavyo vitaongeza chachu ya uzalishaji.
Amesema lengo la kuanzishwa umoja huo
ni kuwawezesha wajasiriamali wadogo kupata nguvu ya kukopesheka kwenye taasisi za
fedha na kuwa na nguvu ya kushindana katika masoko.
No comments:
Post a Comment