Mkuu wa wilaya ya Arusha,John Mongela amesema changamoto zinazokabili vyama vingi vya Akiba na Mikopo na kusababisha kutokuwa na tija iliyokusudiwa ni kutokuheshimu katika za vyama vyao na kuendeshwa bila utaratibu.
Alisema hatua hiyo usababisha vyama kugeuka kuwa kama vyombo vya mtu au kundi la watu wachache wanaoweza kukiendesha kwa maslahi binafsi huku wengine wakiachwa pasipo kunufaika na vyama vyao.
Mongela alitoa kauli hiyo wakati akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa chama cha Akiba na Mikopo cha Fahari Yetu Saccos ambacho ni mali ya wafanyakazi wa taasisi ya fedha ya Pride Tanzania.
“Msingi mkubwa wa vyama vya Akiba na Mikopo ni kuwa na wanachama wanaofahamu vyema wajibu na majukumu yao kwenye chama,wakitimiza wajibu wao wa kuweka akiba mara kwa mara na kukopa kwa busara ili kurejesha mikopo kwa wakati”alisema Mongela
Alisema vyama vya ushirika vya akiba na mikopo hudhoofika na kuporomoka,pale ambapo taarifa za mahesabu ya chama haitolewi kwa wanachama kabisa au haitolewi kwa wakati.
Awali Mwenyekiti wa Fahari Yetu Saccos,Elias Ntambi alisema mafanikio waliyapata tangu kuanzishwa kwake mwaka 1996 ni pamoja na ongezeko la wanachama kutoka 22 hadi 615,mwaka 2013 chama kilipata faida ya zaidi ya Sh 70 milioni na wanachama kupata gawiwo la Sh. 38 milioni baada ya makato ya kisheria.
Alisema akiba za wanachama hadi mwishoni mwa mwaka 2013 zimefikia zaidi ya Sh. 900 milioni likiwa ni ongezeko la asilimia 12 ukilinganisha na akiba iliyokuwepo mwaka 2012,huku mikopo iliyotolewa mwaka 2013 ilikuwa na thamani zaidi ya Sh 1 bilioni jambo ambalo limewawezesha wanachama kunufaika na mikopo hiyo.
Kwa upande wake Afisa Ushirika wa halmashauri ya Jiji la Arusha,Huruma Kibendwa alisema vyama vya Akiba na Mikopo vilivyosajiliwa jijini hapa ni 142 lakini ni Saccos zilizo hai ni 110, huku akitoa rai kwa wananchi kuwa waangalifu wanapotaka kukopa kutoka kwenye taasisi za fedha kutanguliza faida.
Pia katika mkutano huo walichaguliwa viongozi ambao ni Mwenyekiti Elias Ntambi,Makamu Mwenyekiti Abeli Mwaisela,Mweka Hazina,Apolinary Mwijage wengine waliochaguliwa ni Katibu Adriano Msimwa huku wajumbe ni Sarwat Safari na Pascal Costantino


إرسال تعليق