Na Filbert Rweyemamu, Arusha
Halmashauri ya Jiji la Arusha imepiga hatua kubwa katika utekelezaji wa
Mpango wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia (2024–2034) baada ya taasisi 25 kati
ya 239 kufanikiwa kuachana na matumizi ya nishati chafu ikiwemo kuni na mkaa.
Hatua hiyo imebainika wakati wa
mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mkoani hapa, ambapo Kiongozi wa Mbio hizo,Wazo
Michael Mwang’onda alizindua rasmi mradi wa nishati safi katika Shule ya
Sekondari Arusha iliyopo Kata ya Kati.
Akisoma taarifa ya utekelezaji mbele ya kiongozi huyo, Mkuu wa Shule
hiyo, Lorna Christopher Nteles alisema mradi huo umegharimu jumla ya Shilingi
12 milioni fedha zilizotokana na mapato ya ndani ya shule hiyo.
Uchunguzi wa kiteknolojia na kimazingira uliofanywa shuleni hapo
unaonyesha kuwa, kuhamia kwenye nishati safi kutaiwezesha shule hiyo kuokoa
wastani wa miti 4,500 kwa mwaka (sawa na ekari 15 za misitu) ambayo hapo awali
ingekatwa kwa ajili ya kuni za kulisha wanafunzi 1,000.
"Zamani tulikuwa tunatumia gharama kubwa kununua kuni na chakula
kilichelewa kuiva. Moshi na masizi vilikuwa vinachafua mazingira na
kuwasababishia wapishi wetu magonjwa ya macho na kikohozi. Sasa changamoto hizo
hazipo tena," alisema Nteles.
Akizungumza mara baada ya kukata utepe wa uzinduzi, Kiongozi wa Mbio za
Mwenge wa Uhuru Kitaifa,Wazo Michael Mwang’onda aliupongeza uongozi wa shule na
kuutaka mikoa mingine kuiga mfano huo wa Arusha.
"Mwenge wa Uhuru unamulika mabadiliko chanya ya kimazingira. Shule ya
Sekondari Arusha imeonyesha mfano wa kuigwa kwa kutumia mapato yake ya ndani
kulinda misitu yetu na kuokoa afya za wapishi. Hili ndilo lengo la Rais Samia
la kuifanya Tanzania kuwa ya kijani," alisema Mwang’onda.
Jiji la Arusha lina jumla ya taasisi 239 zinazolisha zaidi ya watu 100 kwa
wakati mmoja, na juhudi za kuzihamisha zote kwenda kwenye nishati safi
zinaendelea chini ya kauli mbiu ya Mwenge wa Uhuru: "Tanzania ni Yetu
Sote, Tushikamane kwa Pamoja Kuleta Maendeleo."
Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2026
wilaya ya Arusha umekimbizwa na kupitia miradi Saba ambayo ipo katika Kata Saba
za halmashauri ya Jiji la Arusha kwenye sekta ya maji, afya, barabara na
ujasiriamali kwa makundi ya vijana yenye thamani ya Sh.3.9 bilioni.
Mkuu wa wilaya ya Arusha,Joseph Mkude alisema
kuwa mwaka huu, utekelezaji wa shughuli za maendeleo utafanyika kupitia miradi
saba inayotekelezwa katika wilaya hiyo.
Alieleza kuwa miradi hiyo imejikita
katika kuboresha sekta muhimu za huduma za jamii na maendeleo ya kiuchumi,
ikiwemo maji, afya, barabara na kuwawezesha vijana kiuchumi kupitia miradi ya
ujasiriamali.
Aidha, aliongeza utekelezaji wa miradi
hiyo unalenga kuongeza upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi, kuchochea
maendeleo ya kiuchumi na kuboresha ustawi wa jamii katika maeneo husika.
„Tunataka kuona vijana wanachangamkia
fursa zilizopo katika wilaya yetu ya Arusha na mkoa wa ujumla wakinufaika
kupitia mikopo inayotolewa na kuwa kielelezo kwa vijana wengine kujiajiri ili
kukabiliana na changamoto ya ajira ambayo serikali imekua ikitumia mikakati
mbalimbali kuwawezesha vijana,”alisema Mkude
Alisema kuwa wilaya inaendelea kuweka mazingira
wezeshi ili vijana wanufaike na fursa mbalimbali zinazopatikana katika miradi
ya maendeleo inayotekelezwa na kwamba vijana wengi wameanza kujitokeza na
kutumia fursa hizo, huku baadhi yao wakinufaika moja kwa moja kupitia miradi ya
ujasiriamali na shughuli nyingine za kiuchumi.
Alisisitiza kuwa walionufaika
wanawakilisha kundi kubwa la vijana na kwamba juhudi zinaendelea kuhakikisha
idadi kubwa zaidi ya vijana inafikiwa na kushirikishwa katika programu hizo.
Miradi itakayotembelewa na mbio za
Mwenge wa Uhuru mwaka huu ni ujenzi wa tenki la maji la Lita 50,000 eneo la
Kimindorosi,ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari Kata ya Muriet eneo la Bondeni
City,mradi wa kikundi cha Vijana eneo la Njiro wanaojishughulisha na usindikaji
wa vyakula.
Miradi mingine ni kukagua jengo la
Upasuaji kwenye Kituo cha Afya Kata ya Moivaro,mradi wa nishati safi ya kupikia
katika Shule ya Sekondari Arusha,ufugaji wa kuku wa mayai unaotekelezwa na
vijana wawili na mradi wa ujenzi wa barabara ya kilometa 1.5 eneo la Metejoo
kwa Giriki ulioibuliwa na wananchi.
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Arusha wakionesha uzalendo wao wakati wa makaribisho ya Mwenge wa Uhuru.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Arusha,Lorna Christopher Nteles akisoma taarifa ya Mradi wa Nishati Safi ya kupikia katika shule hiyo.






إرسال تعليق