Jiji la Arusha jana lilikumbwa na taharuki kufuatia askari polisi kuzingira barabara na maeneo kadhaa ya jiji hilo baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutangaza kuendelea na maandamano hayo licha ya kuzuiwa na polisi.
Hata hivyo, maandamano hayo yaliyopangwa kupinga kuendelea kwa Bunge Maalumu la Katiba, mjini Dodoma, hayakufanyika.
Chadema jana ilitangaza kufanyika kwa maandamano katika mikoa ya Arusha,
Iringa na Morogoro ambapo Jumatatu yangefanyika mikoa ya Manyara,
Kilimanjaro, Mbeya , Mwanza , Musoma na Tanga.
Baadhi ya wafanyabiashara katika Jiji la Arusha waliamua kufunga maduka
hususani yaliyo katikati ya jiji kutokana na hofu ya kutokea vurugu.
Polisi walionekana kujizatiti kwa ulinzi mkali katika maeneo
yaliyopangwa kupita maandamano hayo huku wakiwa na silaha za aina
mbalimbali yakiwamo mabomu ya machozi, magari yenye maji ya kuwasha na
mbwa.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa
Arusha, Amani Golugwa, alisema pamoja na maandamano hayo kutofanyika
lakini wamefanikiwa kufikisha ujumbe kwa wananchi kupitia polisi hao.
“Kitendo cha polisi kuzingira kila kona ya mji kumewapa fursa wananchi kujua nini tulichokuwa tumekusudia kufanya,” alisema.
Alisema safari hii Chadema kimetumia namna mpya ya kuandamana kwa kuwatumia polisi kuandamana kwa niaba yao.
“Tumefurahishwa sana na safu mpya ya uongozi kwani hakuna mamluki
walioingia kwenye chama hali iliyowafanya polisi kushindwa kuelewa nini
chama kilipanga kufanya.”
Alisema kilichofanyika jana ilikuwa ni maandalizi ya maandamano yao ya Jumatatu.
Akiwa amezungukwa na magari ya polisi, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, alisema: “Tangu
nimeamka maafisa wa polisi walikuwa wakinifuatilia kila nilipokuwa
nikienda na kwa kuwarahishia kazi nimelazimika kukakaa jirani nao huku
nikiendelea kunywa soda.”
Alisema kimsingi maandamano yako pale pale na yatafanyika kesho (Jumatatu).
“Ila leo (jana), nimeshangaa kuona askari wengi kiasi hicho sijui
wametoka wapi. Lakini nashukuru kwamba wametusaidia kufikisha ujumbe
wetu kama chama,” alisema.
Chama hicho kilipanga kufanya maandamano hayo kuanzia saa 5:00 asubuhi
jana kwenye eneo la Phillips na kuishia viwanja vya Samunge vilivyopo
eneo la Kilombero.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alisema
kilichofanyika jana ni ulinzi wa kawaida na wananchi hawakupaswa kuwa na
hofu.
“Tumejitahidi kuhakikisha hakuna maandamano yaliyofanyika na askari walionekana ni wa kawaida,” alisema huku akicheka.
Wakati huo huo, hali katika mikoa mingine iliyotajwa kufanyika
maandamano hayo ilikuwa shwari baada ya polisi kuzima maandamano hayo
katika mkoa wa Morogoro juzi.
Kwa upande wa mkoa wa Iringa, Mwandishi Geofrey Lyimo, anaripoti kuwa
hakukuwa na dalili yoyote ya maandamano huku wananchi wakiendelea na
shughuli zao kama kawaida.
No comments:
Post a Comment